Habari za Punde

Balozi Seif Azungumza na Mwakilishi wa Kampuni ya Kimataifa ya Ujenzi GARWARE ya Nchini India.

 
Kaimu Balozi wa Tanzania Nchini India Balozi Mohammed  Hijja kulia akifafanua jambo wakati wa mazungumzo na Kiongozi wa Kampuni za Kimataifa ya Ujenzi ya GARWARE na Taasisi inayojishughulisha na Masuala la Sekta ya Elimu ya Arun { U } ltd ya Nchini India walipokutana na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.

Mwenyekiti na Mkurugenzi Mkuu wa  Taasisi inayojishughulisha na Masuala la Sekta ya Elimu ya Arun {U}ltd ya Nchini India Bwana Jatinder Sehgal na wa kwanza kushoto ni Balozi Seif.
Balozi Seif akibadilishana mawazo na Ujumbe huo wa Makampuni na Taasisi za Uwekezaji kutoka Nchini India mara baada ya mazungumzo yao.
Picha na – OMPR – ZNZ.

Na Othman Khamis OMPR.
Mwakilishi wa Kampuni ya Kimataifa ya Ujenzi ya GARWARE ya Nchini India  Bwana Kedar Chapekar amesema Zanzibar ina uwezo wa kuwa kituo cha Kimataifa cha Kibiashara kinachofanana na Dubai kutokana na rasilmali ya kimazingira iliyonayo.

Bwana Kedar alieleza hayo akiambatana na Mwenyekiti na Mkurugenzi Mkuu wa  Taasisi inayojishughulisha na Masuala la Sekta ya Elimu ya Arun { U } ltd ya Nchini India Bwana Jatinder Sehgal wakati wakizungumza na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.

Viongozi hao wa Taasisi za Uwekezaji za Nchini wapo Zanzibar kwa ziara ya Wiki moja kuangalia fursa mbali mbali za Uwekezaji zilizopo Zanzibar kufuatia mualiko wa Balozi Seif wakati wa ziara yake ya hivi karibuni Nchini India.

Alisema Zanzibar iko katika mazingira mazuri ya Kibiashara ndani ya mwambao wa Afrika Mashariki pamoja na Ukanda wa Kusini Mashariki mwa Bara la Afrika ambayo bado haijatumika vyema kama ilivyokuwa katika miaka ya nyuma.

Bwana Kedar alimueleza Balozi Seif kwamba  Taasisi zao za uwekezaji zimepata fursa nzuri ya kuangalia hali halisi ya kimazingira iliyopo Zanzibar na Uongozi wa Taasisi hizo utaangalia maeneo ambayo wanaweza kuwekeza Visiwani Zanzibar.

Naye Mwenyekiti na Mkurugenzi Mkuu wa  Taasisi inayojishughulisha na Masuala la Sekta ya Elimu ya Arun { U } ltd ya Nchini India Bwana Jatinder Sehgal alisema upo uwezekano wa Zanzibar kuwa na Ukumbi mkubwa wa Kimataifa unaoweza kutoa huduma za Mikutano ya Kimataifa.

Bwana Jatinder Sehgal alisema ukumbi huo kwa upande mwengine unaweza kuhamasisha kasi ya uwekezaji ambayo tayari imeshachaguliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuwa muhimili wa Uchumi wake utakaoweza kusaidia kunyanyua Mapato ya Taifa.

Akitoa shukrani zake kufuatia ujio wa Ujumbe huo wa Wawekezaji kutoka Nchini India kufuatia ziara yake ya hivi karibu Nchini India Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Zanziba  imejiwekea malengo ya kuwa kituo na kitovu cha Utalii katika Ukanda wa Afrika Mashariki.

Balozi Seif alisema uimarishaji wa Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Zanzibar pamoja na miundombinu ya mawasiliani ya bara bara  ni jitihada za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuona Sekta hiyo inaanza muelekeo mzuri wa kuimarika Kiuchumi.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alizipongeza Taasisi na Makampuni ya Nchini India yaliyoonyesha nia ya kutaka kuwekeza miradi yao ya Kiuchumi Visiwani Zanzibar katika azma yao ya kuunga mkono jitihada za SMZ za kuimarisha mipango ya Maendeleo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.