Habari za Punde

Viongozi Wabadhirifu Wasipewe Nafasi Katika Vyama Vya Ushirika..


Na Ismail Ngayonga.Maelezo Dar es Salaam.
USHIRIKA ulimwenguni umekuwa ndio njia pekee na rahisi ya kuwawezesha watu mbalimbali kuungana na kuweza kuwa na sauti moja katika kutetea haki na maslahi yao.

Mara baada ya Uhuru, Serikali ilitoa msukumo mkubwa wa kuanzishwa vyama vikuu katika mikoa na kuufanya ushirika kuwa ni nyenzo ya maendeleo ya uchumi vijijini na kutekeleza Sera ya Ujamaa na kujitegemea

Vyama vya Ushirika vimekuwa sehemu muhimu ya maendeleo ya Tanzania kwa miaka 75, kwani katika kipindi chote hicho hakuna taasisi nyingine yoyote zaidi ya Ushirika iliyowaunganisha pamoja watu wengi katika azma na lengo linalofanana.

Uzoefu wa Nchi mbalimbali Duniani umeonyesha kuwa mafanikio na mapinduzi ya Kilimo huchangiwa  kwa kikubwa na uwepo kwa Vyombo imara vya Wakulima vikiwemo Vyama vya Ushirika.

Kuanzia miaka ya 2000 Serikali iliweka mkazo katika kuvisaidia vyama vya ushirika ambavyo vinamilikiwa na kusimamiwa na wanachama wenyewe kwa mujibu wa maadili na misingi ya ushirika inayotambuliwa kimataifa.

Vyombo hivi ndivyo vinavyoweza kuwatafutia na kuwapatia Wakulima mahitaji yao muhimu ikiwa ni pamoja na pembejeo, mikopo, mitaji, teknolojia bora, masoko ya mazao yao nataarifa mbalimbali za kuwasaidia katika uzalishaji.

Ushirika unatoa fursa kwa Wakulima na Wazalishaji wengine wenye uwezo mdogo kuunganisha nguvu zao pamoja ili kuwa na nguvu kubwa kiuchumi ambazo ni muhimu katika kukabiliana na ushindani wa soko.

Katika kutekeleza Programu Kabambe ya Mageuzi na Modenaizesheni ya Ushirika (CRMP) nchini na pamoja na kuvijengea uwezo Vyama vya Ushirika kufanya biashara, Serikali ilifuta madeni ya Vyama vya Ushirika yenye thamani ya Shilingi Bilioni 15 yaliyokuwa yanadaiwa na Serikali na Taasisi zake.
Kutokana na Serikali kulipa madeni hayo, uwezo wa Vyama hivyo kukopesheka umeongezeka hivyo kuweza kupata mikopo kutoka Taasisi za Fedha kwa ajili ya ukusanyaji na ununuzi wa mazao ya  Wakulima ikiwemo, Korosho, Pamba na Kahawa.

Hali ya ushirika nchini imeendelea kuimarika kutokana na utekelezaji wa CRMP, ambapo Idadi ya wanachama wa Vyama vya Ushirika imeongezeka kutoka milioni 1.8 mwaka 2009 hadi milioni 2.1 mwaka 2010. Aidha idadi ya Vyama vya Ushirika wa Mazao imeongezeka kutoka 2,616 mwaka 2006 hadi vyama 2,821 mwaka 2009
Pamoja na umuhimu wa Ushirikavyama vingi vimeshindwa kufanya kazi vizuri kutokana na baadhi ya Viongozi kutumia vibaya mamlaka yao kwa kujinufaisha na kuwanyonya wanachama.
Akijibu Swali Bungeni Mjini Dodoma, Naibu Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, William Tate Ole Nasha anasema mwaka 2012 Serikali kupitia Ofisi ya Mrajis wa Vyama vya Ushirika nchini ilifanya ukaguzi ukaguzi katika Vyama vya Ushirika wa Korosho katika Mkoa wa Pwani na kubaini upotevu wa fedha wa Tsh. Bilioni 2.6.
Anasema ubadhirifu huo ulisababishwa na viongozi na watendaji 822 wa Vyama vya Ushirika vya zao la korosho katika Mkoa wa Pwani, ikiwemo Viongozi 41 wa Wilaya ya Rufiji ambapo kwa kutumia kifungu cha 95 cha sheria ya ushirika, aliwaandikia hati ya madai Viongozi hao na kuwataka kulipa fedha zilizopotea.
Aidha Ole Nasha anasema kuwa pia uhakiki uliofanywa Mrajisi unaonesha kuwa wakulima wa korosho wa Mkoa wa Pwani wanavidai vyama vya msingi jumla ya Tsh. Bilioni 3.1 , deni  lililotokana na sababu mbalimbali za kibiashara kama vile anguko la bei ya korosho katika soko la dunia.
“Mchanganuo wa deni hilo kwa kila Wilaya ni kama ifuatavyo; Mkuranga ni shilingi 1,931,224,587, Rufiji shilingi 1,215,018,100, Kibaha Mjini shilingi 758,880, Bagamoyo ni shilingi 10,275,960 na Mafia shilingi 7,857,576” anasema Ole Nasha.
Kwa mujibu wa Ole Nasha anasema hadi tarehe 5 Novemba, 2015 ni viongozi 79 tu kati ya 822 wa Mkoa wote wa Pwani waliokuwa wamerejesha jumla ya shilingi 24,260,163.19, ambapo Serikali imeandaa taratibu kuwafikisha katika vyombo vya sheria Viongozi walioshindwa kurejesha fedha hizo.
Aidha Naibu Waziri huyo anasema hadi tarehe 8/06/2016 tayari majalada 11 yalikuwa yamefunguliwa polisi na kufikishwa katika Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Mkoa wa Pwani.
Waraka wa Mkakati wa Taifa wa Kukuza Uchumi Kupunguza Umaskini (MKUKUTA) unasisitiza kuwa Serikali itajitahidi kuhakikisha kuwa vyombo vya wananchi maskini kama vile, Vyama vya Ushirika vinakuwa katika mstari wa mbele katika kuanzisha na kuendeleza taratibu na mipango inayofaa.
Serikali imeendelea kuchukua hatua za muda mfupi na mrefu kukabiliana na matatizo mbalimbali ya vyama vya ushirika ikiwa ni pamoja na kutungwa  kwa Sheria ya Vyama vya Ushirika Namba 6 ya Mwaka 2013 ambayo imeanzisha Tume ya Maendeleo ya Ushirika.
Kwa kutumia sheria hiyo viongozi wabadhirifu katika Vyama vya Ushirika wamechukuliwa hatua ikiwemo kusimamishwa kazi na kufikishwa mahakamani. Aidha kupitia sheria hiyo vyama vimekatazwa kukopa zaidi ya asilimia 30 ya mali zake ili kuzuia vyama kuingia kwenye madeni makubwa yasiyolipika.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.