Habari za Punde

Bodi ya Mikopo yawakumbusha waliokopa kurejesha

Na.Haji Nassor. Pemba.
BODI ya Mikopo Elimu juu Zanzibar ‘BMEJZ’ imewataka wadaiwa ambao wameshaajiriwa kwenye taasisi za umma au binafis, kufanya hima kurejesha mikopo hiyo, ili kutoa furasa kwa wengine kuiomba ili kujiendeleza kielimu.
Kauli hiyo imetolewa na Mraibu wa Bodi hiyo Kisiwani Pemba, Ahmada Omar Juma, wakati alipokuwa akitoa taarifa ya urejeshaji wa mikopo kwa wakopaji kuanzia mwaka 2011 hadi mwezi Mei mwaka huu, afisini kwake jengo la Wizara ya elimu Chakechake.
Alisema inawezeka wakopaji, mara baada ya kumaliza masomo hujisahau kwamba fedha hizo zinahitajika kurejeshwa, ili na wengine waombe, hivyo ni vyema wakajihimu.
Mratibu huyo alieleza kuwa, sio vyema kwa wadaiwa hao kungojea Bodi kutumia sheria yake ikiwemo kuwafikisha mahakamani, kuwafuatilia wadhamini au waajiri wao, bali wajihimu kurejesha kwa hiari.
Aidha Mratibu huyo, alisema idadi ya wanafunzi wanaopatiwa mikopo inaweza kuongeza Zanzibar kutoka 594 hadi kufikia 1,600, ikiwa hata kasi ya urejeshaji wa fedha nao haitokuwa wa kusua sua.
“Kama kukopa ni harusi, basi hata kurejesha iwe ni harusi, maana wakichelewa kurejesha au kujificha ndio ni sawa na kuwakosesha wengine’’,alifafanua.
Hata hivyo Mratibu huyo alisema uombaji wa mikopo kwa mwaka huu wa 2017/2018 umeshaanza tokea Mei 2 mwaka huu, na unatarajiwa kumalizika Julai 30 na hadi sasa ni wanafunzi 65 pekee kisiwani Pemba wameshajitokeza kuomba.
Katika hatua nyengine Mratibu huyo wa Bodi ya Mikopo Elimu juu Zanzibar kisiwani Pemba, Ahmad Omar Juma, aliwataka wadhamini na waajiri kuendelea kutoa taarifa za uajiri mpya kila wanapofanya, ili bodi hiyo iweze kufuatilia iwapo kuna aliesoma kwa njia ya mkopo.
Baadhi ya wanafunzi wenye nia ya kuomba kwenye bodi hiyo, walisema ni vyema kuwepo kwa ufuatiliaji mkubwa kwa wanaopatiwa mikopo, ili kuanza na kundi la wale wanaoishi mazingira magumu.
Hassan Mjaka Omar, alisema yeye anatarajia kuomba mkopo kwa mwaka huu, na anasema kama akipatiwa hana wasi wasi wa kurejesha, pindi akishaajiriwa.
“Mimi nikipata mkopo na kisha nikimaliza chuo nikiajiriwa, wala sina kificho, maana najua na wenzangu wanataka kuomba mkopo, ambao uwezo wao mdogo kama mimi”,alieleza.
Kwa upande wake mwanafunzi Sheikh Rashid Seif anaendelea na masomo yake Chuo Kikuu huria Tanzania tawi la Pemba ambae alipata mkopo, alisema changamoto kubwa inayojitokeza ni kuchelewa kidogo kuingiziwa fedha.
“Lakini hata fedha za kujikimu ni vyema zikaingizwa, maana mwanafunzi anapokuwa chuoni anamahitaji kadhaa, na akikosa fedha za mtirirko wake wa masomo hautokuwepo”,alisema.

Bodi ya Mikopo ya elimu ya juu Zanzibar ‘BMEJZ’ ambayo imeanzishwa chini ya sheria no 3 ya mwaka 2011, ilianza kazi zake Julai mwaka huo, na kurithi kazi zilizokuwa zikifanywa na uliokuwa Mfuko wa elimu ya juu Zanzibar, ambapo hadi sasa wanafunzi 5,293 wanaendelea kusomomeshwa na bodi hiyo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.