Habari za Punde

Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani Awaasa Wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini Mwa Afrika (SADC) Kupambana na Matendo ya Uhalifu.

Na Mwandishi Wetu.                              
Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Balozi Hassan Simba Yahya, amewaomba washiriki wa Mkutano wa Kamati Ndogo ya Usalama wa Raia ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), kuhakikisha wanapambana kupunguza vitendo vya ujangili, biashara ya magendo, biashara ya binadamu, uhamiaji haramu kwani vitendo hivyo vinarudisha nyuma maendeleo ya nchi zilizopo katika jumuiya hiyo, hivyo kupelekea kurudi nyuma kwa shughuli za maendeleo na uchumi.

Balozi Simba aliyasema hayo alipozungumza katika Mkutano huo uliojadili masuala mbali mbali ya ulinzi na usalama katika maeneo ya nchi wanachama wa jumuiya hiyo, uliohusu masuala ya uhamiaji, ukimbizi, mbuga na wanyama pori katika maeneo ya nchi wanachama wa jumuiya ya SADC, leo jijini Dar es Salaam.
“Hatuwezi kuendelea kiuchumi katika nchi zetu za wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika, kama matendo ya ujangili, biashara ya binadamu, masuala ya wakimbizi, uhamiaji haramu hayajatafutiwa ufumbuzi, kwani haya yatazorotesha shughuli za kiuchumi ikiwepo utalii, hivyo ni bora tukayafanyia kazi maeneo hayo,” alisema Balozi Simba

Akizungumza wakati wa uchangiaji mada katika mkutano huo, Mkurugenzi wa Masuala ya Siasa, Ulinzi na Usalama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) Jorge Cardoso, alisema uhalifu katika mipaka ya nchi wanachama ikiwemo uwindaji haramu wa pembe za ndovu, uhamiaji haramu, biashara ya binadamu na dawa za kulevya lazima vidhibitiwe kwani vikiachwa mbeleni vitahatarisha  Amani na utulivu uliopo katika nchi wanachama.

“Amani na utulivu katika nchi wanachama ni kichocheo cha mabadiliko ili kupiga hatua za kimaendeleo kwenda mbele na kushirikiana kukuza uchumi katika nchi wanachama wa SADC, hivyo yatupasa wote kwa pamoja kuunga mkono harakati za kukomesha vitendo vya uhalifu katika nchi na mipaka yetu,” alisema Cardoso


Aidha washiriki wa mkutano huo kutoka katika nchi za Tanzania, Afrika Kusini, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Swaziland, Malawi, Zimbabwe kwa pamoja walikubaliana kupitia Kamati za Ulinzi na Usalama katika nchi zao kudhibiti matendo yote yanayohatarisha amani na utulivu.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.