Habari za Punde

Mashindano ya Kimataifa ya 25 Kuhifadhi Quran Ukumbi wa Diamond Jubillee Dar es Salaam.

Makamu Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akizungumza katika hafla ya Tuzo ya Kimataifa ya Mashindano ya Kuhifadhi Quran yaliyofanyika katika Ukumbi wa Diamond Jubilee Mjini Dar es salaam. 
Balozi Seif akimkabidhi cheki ya Dola za Kimarekani 5,000 Mshindi wa kwanza wa Mashindao ya Tuzo ya Kimataifa ya Kuhifadhi Quran Kijana Abdullmajid Mujahid kutoka Nchini Yemen.
Mshindi wa Pili wa Mashindao ya Tuzo ya Kimataifa ya Kuhifadhi Quran Mwanafunzi Omar Abdullah wa Tanzania akipokea zawadi ya Dola  Elfu 4,000 na Shilingi Laki 60,000 za Kitanzania kutoka kwa Mgeni rasmi Balozi Seif.
Mlezi wa Taasisi ya Kuhifadhisha Quran Mkoa wa Dar es salaam Rais M,staafu wa Tanzania Dr. Ali Hassan Mwinyi akipokea Tuzo Maalum kutokana na mchango wake mkubwa ndani ya Taasisi hiyo kutoka kwa Msomaji Quran Maarufu wa Kimataifa kutoka Saudi Arabia Sheikh Abdullah Ali Basfar.
Washiriki wa mashindano ya Tuzo ya Quran kutoka Nchi 18 Duniani waliofikia fainal ya mashindano hayo.

Balozi Seif Ali Iddi akisalimiana na Msanii Nguli Nchini Tanzania Ahmed  Chilo {Maarufu Mzee Chilo } mara baada ya kumalizika kwa Mashindao ya Tuzo ya Kimataifa ya Kuhifadhi Quran yaliyofanyika katika Ukumbi w Diamond Jubilee Jijini Dar es salaam.

Na. Othman Khamis OMPR. 
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Quran ambayo ndio Kitabu na Muongozo sahihi unaotakiwa kufuatwa na kila Muumini wa Dini ya Kiislamu ina nafasi kubwa katika kujenga Jamii na Taifa lenye raia wema na Waadilifu.

Alisema Muumini aliyehifadhi Quran na kuifanyia kazi kamwe hawezi kuwa mlevi, mzinzi, mbadhirifu na fisadi kwa vile muda wake wote wa maisha huitumia Elimu hiyo katika kupigania maslahi ya Umma uliomzunguuka, akielewa kwamba hiyo ndio sifa ya Waumini na Taifa lililo bora lenye Amani na Maadili mema.

Balozi Seif Ali Iddi alieleza hayo wakati wa Fainali ya Tuzo ya Kimataifa ya Usomaji Quran ikiwa ni mashindao ya 25 tokea kuanzishwa kwake Mwaka 1992 yanayoandaliwa na Uongozi wa Dini ya Kiislamu wa Mkoa wa Dar es salaam yaliyofikia kilele chake katika Ukumbi wa Diamond Jubilee.

Alisema kwa vile Serikali inatambua mchango mkubwa unaotolewa na kuchukiliwa na Viongozi wa Taasisi za Kidini katika kuwalea Vijana kupitia msingi Imara wa Vitabu Vitukufu ni lazima Jamii yote ikumbuke kwamba tabia zao zinatakiwa ziendane na mafundisho ya Vitabu hivyo.

Alieleza kwamba Jamii hivi sasa inapita katika kipindi kigumu ambacho inashuhudia matukio mbali mbali yanayoashiria mmong’onyoko wa maadili hapa Tanzania na ukichunguza chanzo chake kikuu ni kundi kubwa lililokosa mafunzo ya Dini na kutumbukia katika vitendo viovu.

Balozi Seif  alisema ipo mifano ya matukio ya ajabu yanayofanywa na Vijana waliokosa  mafunzo ya Dini mambo ambayo yamewakosesha  adabu na utii kwa Wazazi wao, kukithiri kwa vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia na ulawiti uliokithiri unaoshuhudiwa katika mitaa mbali mbali  nchini.

Alifahamisha kwamba matendo hayo yanaonekana kwenda sambamba na baadhi ya Watu hasa wale wenye uwezo wa kifedha kuwatumikisha kazi ngumu Watoto wadogo ambao pia hupewa adhabu zisizostahiki, Mauaji ya Kikatili kwa Watoto Wachanga wasio na hatia yoyote.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar  alitoa wito kwa walimu wa vyuo vya Quran Nchini  ambao ndio waliochukuwa juhudi za kuwafinyanga vijana  walioshiba Kitabu Kitukufu kwamba wanapaswa waongeze juhudi katika kukisomesha na kukihifadhisha Kitabu hicho.

Alisema Walimu hao ni vyema wakaelewa kuwa wao ndio Watu Bora katika Ulimwengu huu kwa mujibu wa mafundisho ya Kiongozi wa Dini ya Kiislamu Duniani Mtume Muhammad {SAW} pale aliposema mbora wenu ni yule mwenye kujifunza Quran Tukufu na yeye baadae akaifundisha kwa wengine.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwanasihi Vijana ambao wameonyesha uwezo mkubwa wa kuhifadhi Quran Tukufu waendelee kuidurusu kila siku ili Quran hiyo iendelee kubakia katika Vifua na nyoyo zao vyenginevyo wasipofanya hivyo bila ya shaka Quran waliyoihifadhi kwa juhudi kubwa itatoweza kwenye vifua vyao.

Balozi Seif alielezea faraja yake kuona Vijana wa Mataifa mbali mbali wanavyoshindana katika kusoma Quran Tukufu akisema hiyo ni ishara kwamba Quran inatosha kuwaunganisha Waislamu mahali popote Duniani pasi na kuzingatia tofauti zao za rangi, lugha nahata  kipato.

Aliwapongeza waandaaji wa Tuzo hiyo Jumuiya ya kuhifadhisha Quran kwa kushirikiana na Taasisi ya Tanzania Muslim Hajj Trust licha ya kukumbana na changamoto kadhaa za maandalizi yake lakini waliweza kusimama imara katika kufanikisha jukumu hilo na hatimae kufikia ngazi hiyo ya Tuzo ya Kimataifa.

Mapema Mwenyekiti wa Taasisi ya Kuhifadhi Quran Tanzania  Sheikha Othman Ali Kiporo alisema Ulimwengu hivi sasa unaelekea katika Quran jambo ambalo Waumini wa Dini hiyo kwa sasa wanalazimika waendelee kuipenda Qurana katika maisha ya kila siku.

Sheikha Kaporo alisema njia pekee kwa sasa ni jamii ya Kiislamu kukabiliana na utatuzi wa matatizo  yanayowakumba kwa kuelekeza nguvu zao katika kuwafunza Watoto Quran ikilenga kutafsiriuwa katika matendo ya kila siku.

Akitoa salamu Msomaji Maarufu wa Quran wa Kimataifa ambae pia ni Katibu Mkuu wa Taasisi ya kuhifadhisha Qurana kutoka Nchini Saudi Arabia Sheikh Abdullah Ali Bashaf amewashukuru Viongozi na Taasisi mbali mbali za Kitaifa na Kimataifa zilizosaidia harakati za uhifadhi ya Quran kwa Vijana wa Kiislamu.

Sheikh  Abdullah alisema juhudi hizo zimepelekea Taasisi yake kushawishika na kugharamia Ujenzi wa Chuo Kikuu kitakacholenga kuwapatia Taaluma Wanafunzi wote waliobobea katika uhifadhi wa Quran katika vyuo na Madrasa mbali mbali Nchini ambao kwa sasa wanakadiria kufikia zaidi ya Wanafunzi 1,000.

Naye Mufti Mkuu wa Tanzania Sheikha Abubakar Zubeir alisema watoaji muhadhara na mawaidha ni vyema yakalenga katika njia njema iliyoainishwa katika Quran na Mafunzo ya Mtume Muhammad {SAW}.Sheikha Abubakar alisema hiyo ndio  njia sahihi itakayoivua salama Jamii na Waumini wa Dini ya Kiislamu pamoja na Wananchi wa Mataifa yote yaliyomo ndani ya ulimwengu huu.

Akitoa nasaha katika hadhara hiyo Mlezi wa Jumuiya ya Uhifadhi wa Quran Tanzania Rais Mstaafu wa Tanzania  Dr. Ali Hassan Mwinyi kuwashukuru wale wote waliochangia kufanikisha mashindano hayo jambo ambalo limempa faraja katika maisha yake ya kila siku.

Mzee Mwinyi Quran imekuwa na maajabu mengi yasiyohifadhika kiasi kwamba Jamii inapaswa kuyatumia maajabu hayo katika njia ya kujifunza kila wakati ili kupata fadhila zaidi kama alivyosisitiza Muumba wa Dunia kwamba Kitabu hicho ataendelea kukilinda katika muda wote wa uwepo wa Ulimwengu huu.

Katika Mashindao hayo Ustadhi Abdullmajid Mujahid kutoka Nchini Yemen ameibuka mshindi wa kwanza na kupata tuzo ya Dola za Kimarekani Elfu 5,000 na pamoja na Shilingi Milioni 1,000,000/- za Kitanzania.

Mshindi wa Pili ni Mwanafunzi Omar Abdullah wa Tanzania aliyepata Elfu 4,000 na Shilingi Laki 60,000 za Kitanzania, Watatu Ubeid Mohamed kutoka Umoja wa Falme za Kiarabu aliyepata Dola Elfu 3,000, Wanne Jamal Abdi kutoka Uingereza aliyepata Dola Elfu 2,000 na Abdullah Alghuriyi kutoka Nchini Libya aliyepata Dola 1,000.

Mashindano hayo ya 25 ya Kimataifa yaliyojumuisha washiriki 19 kutoka Mataifa 18 Duniani yalianza siku ya Ijumaa ambapo washindanaji hao walikuwa katika mchakato mkali uliowezesha kupatikana kwa washindi Kumi Bora walioingia Fainal za mashindao hayo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.