Habari za Punde

MATUMIZI YA TEHAMA KUONGEZA KASI YA UKUSANYAJI MAPATO TAMISEMI.

Na Ismail Ngayonga. Maelezo Dar es Salaam.                                                                     
SERA ya Taifa ya TEHAMA ya mwaka 2003, pamoja na mambo mengine inasisitiza juu ya Serikali kutumia fursa za TEHAMA katika utendaji kazi wa kila siku na utoaji huduma kwa wananchi.
Katika kutekeleza Sera hiyo, mwaka 2004 Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma ilianza kuchukua hatua mbalimbali kuongeza matumizi ya TEHAMA katika kuimarisha mifumo ya utoaji habari na huduma kwa wananchi.
Baadhi ya hatua hizo ni pamoja na kuanza dhana ya utekelezaji wa Serikali Mtandao iliyokuwa sehemu ya program ya mabadiliko katika utumishi wa umma, iliyolenga kuongeza ufanisi katika utendaji kazi na uboreshaji huduma kwa umma.
Programu hiyo iliziwezesha Wizara, Idara zinazojitiegemea, Wakala za Serikali, Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka ya Serikali za Mitaa kuwa na mifumo imara ya menejimenti ya Habari ambapo Serikali ililenga kutumia TEHAMA katika utoaji wa habari na huduma kwa wananchi.
Hatua hizo zimesababisha matumizi ya TEHAMA kuongezeka kwa kasi Serikalini na kupanua wigo wa uwazi, ufanisi, uwajibikaji na tija katika utoaji wa huduma kwa wananchi.
Akiwasilisha Hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya bajeti kwa mwaka 2017/18, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais- TAMISEMI George Simbachawene anasema matumizi ya mifumo ya TEHAMA imesaidia kupunguza mianya ya ufujaji na uvujaji wa mapato kwa kuwezesha malipo kufanyika moja kwa moja Benki. 
Anasema Ofisi yake imefanikiwa kufunga mifumo saba (7) ya TEHAMA ambayo inafanya kazi katika Mamlaka za Serikali za Mitaa, ikiwemo Mfumo Funganishi wa Usimamizi na Udhibiti wa Matumizi ya Fedha (IFMS- EPICOR 9.05), mfumo wa malipo unaojulikana kama “Tanzania Interbank Settlement System - TISS”).
Anaitaja mifumo mingine kuwa ni pamoja na Mfumo wa Uandaaji wa Mipango na Bajeti (PlanRep), Mfumo wa Takwimu za Elimumsingi (BEMIS), Mfumo wa Taarifa za shule (SIS), Mfumo wa ukusanyaji mapato (LGRCIS) na Mfumo wa Uendeshaji na Usimamizi wa Vituo vya kutolea huduma za afya (GoTHOMIS). 
Anasema mfumo wa Uendeshaji na Usimamizi wa vituo vya kutolea huduma za afya umesaidia katika upatikanaji wa taarifa sahihi na kwa wakati kutoka ngazi za kituo, usimamizi wa dawa na vifaa tiba, usimamizi wa rasilimali watu na mapato yatokanayo na uchangiaji wa huduma za afya.
“faida za mifumo ya kielektroniki ni kuongeza ufanisi katika utendaji kazi, kupunguza gharama, kuongeza uwajibikaji, upatikanaji wa taarifa sahihi na kufanya maamuzi kwa wakati” anasema Simbachawene.
Simbachawene anasema Mfumo Funganishi wa Usimamizi na Udhibiti wa Matumizi ya Fedha za Mamlaka za Serikali za Mitaa (IFMS) – Epicor 9.05 umefungwa katika Halmashauri 169 kati ya 185 zilizopo sawa na asilimia 91.3, ambapo umesaidia yamesaidia kuongeza uwazi na uwajibikaji katika usimamizi wa fedha za umma.
Aidha Simbachawene mfumo huo pia umesaidia kuboresha utendaji katika kutekeleza bajeti zilizopangwa ili kuondokana na hoja za matumizi nje ya bajeti, kudhibiti uhamishaji wa fedha kutoka mradi mmoja kwenda mwingine kinyume na utaratibu, pamoja na kurahisisha utendaji kazi katika shughuli za malipo.
Kwa mujibu wa Simbachawene anasema Serikali kupitia OR-TAMISEMI na Wizara ya Fedha na Mipango imefanikiwa kufunga mfumo wa TISS katika Halmashauri za Mikoa ya Dar es Salaam, Arusha, Mwanza, Mbeya, Dodoma, Tanga na Morogoro na Mikoa iliyobaki itafungiwa mfumo huo katika mwaka wa fedha 2017/18.
“Mfumo huu unasaidia kuimarisha usimamizi na udhibiti wa malipo kutoka kwenye akaunti ya Halmashauri kwenda kwenye akaunti ya mlipwaji (mteja) na malipo yanafanyika moja kwa moja kutoka kwenye akaunti zilizopo Benki Kuu (BoT)” anasema Simbachawene.
Anaongeza kuwa uwekaji wa mifumo ya kielektroniki upo katika hatua mbalimbali za utekelezaji ikiwa ni pamoja na ununuzi wa vifaa na uwekezaji wa miundombinu lengo likiwa ni kuweka mifumo hiyo katika Mikoa, Halmashauri na vituo vyote vya kutolea huduma nchini.
Matumizi ya TEHAMA yatawezesha wananchi kupata huduma mbalimbali za Serikali kwa wakati, uwazi na ufanisi pamoja na kupunguza gharama za utendaji, hivyo kusaidia nchi kufikia maendeleo kwa haraka.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.