Habari za Punde

Balozi Seif Azungumza na Balozi Mdogo wa China Zanzibar leo.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif  Ali Iddi Kushoto akibadilishana mawazo na Balozi Mdogo wa Jamuhuri ya Watu wa China aliyepo Zanzibar Bwana Xie Xiaolon Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.
Balozi Mdogo wa Jamuhuri ya Watu wa China aliyepo Zanzibar Bwana Xie Xiaolon  kati kati akimkabidhi zawadi Balozi Seif mara baada ya kumaliza mazungumzo yao Vuga Mjini Zanzibar.(Picha na – OMPR – ZNZ.)

Na. Othman Khamis OMPR. 
Wataalamu Watatu wa Fedha kutoka  Benki ya Kimataifa ya Exim ya Nchini Jamuhuri ya Watu wa China wanatarajiwa kuwasili Zanzibar  Mwezi ujao kukamilisha taratibu za ukamilishaji wa ujenzi wa eneo la Maegesho ya Ndege kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Aman Karume Zanzibar.

Balozi Mdogo wa Jamuhuri ya Watu wa China aliyepo Zanzibar Bwana Xie Xiaolon alieleza hayo wakati akizungumza na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi  Ofisini kwake Mtaa wa Vuga Mjini Zanzibar baada ya kupokea Barua ya ujio wa Wataalamu hao mapema leo asubuhi.

Balozi Xie Xiaolon alisema Benki ya Exim tayari imeshatoa baraka  za kutoa mkopo wa kukamilisha ujenzi wa mradi huo wa Maegesho ya  Ndege kufuatia maombi ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar yaliyotolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Nchini China Disemba mwaka 2016.

Alisema Uongozi wa Benki ya Kimataifa ya Exim utaidhinisha  Mkopo wa Fedha wa zaidi ya asilimia 50% kwa ajili ya kukamilisha mradi huo unaotarajiwa  kuchukuwa miezi Minane hadi kumalizika kwake.

Balozi Mdogo huyo wa China aliyepo Zanzibar alifahamisha  kwamba hatua hiyo iliyochukuliwa na Uongozi wa Benki ya Exim utaleta faraja kubwa kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na Wananchi walio wengi Visiwani Zanzibar.

Alimuhakikishia Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba China itaendelea kuiunga mkono Zanzibar na Tanzania kwa ujumla  kuendeleza uhusiano wa Kihistoria uliopo kati ya Wananchi wa pande hizo mbili rafiki.

Akitoa shukrani zake kwa Habari hiyo njema masikioni mwa Wananchi wa Zanzibar Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alimpongeza Balozi Mdogo wa China kwa jitihada zake za ziada zilizochangia kuharakisha suala hilo.

Balozi Seif alisema ukamilishaji wa ujenzi wa eneo la maegesho ya Ndege katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Aman Karume { Terminal Two}  ni muhimu kwa Uchumi wa Zanzibar katika harakati zake za kutafuta mbinu za kuongeza mapato.

Alieleza kwamba utanuzi wa Uwanja huo utatoa fursa na uwezo zaidi wa kuruhusu ndege kubwa zitakazoweza kushusha na kupakia idadi kubwa zaidi ya Mizigo na Wasafiri hasa Watalii wanaotegemewa kuongezeka mara dufu baada ya kukamilisha kwa mradi huo.

Balozi Seif alimueleza Balozi Mdogo wa China kwamba lengo la Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya kuimarisha miundombinu ya usafiri wa anga limeelekeza katika kuijenga mazingira mazuri zaidi sekta ya Utalii inayotegemewa kuwa muhimili Mkuu wa Uchumi wa Zanzibar badala ya Karafuu.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.