Habari za Punde

Vyombo 71 vya nchi kavu vyakamatwa kwa bima ‘feki’


NA HAJI NASSOR, PEMBA
ZOEZI la utambuzi wa bima halali, lililofanywa na watendaji wa jeshi la Polisi na wakuu wa vitengo vya Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania ‘TIRA’ kisiwani Pemba, limekamata vyombo vya moto 71 vikiwa na bima zisizotambulika kati ya vyombo 168 walivyovikagua.
Zoezi hilo lilifanyika hivi karibuni kwenye barabara ya Chakechake - Wete, mara baada ya ‘TIRA’ kuwapa mbinu za kielektroniki watendaji hao wa jeshi la Polisi, jinsi ya kugundua bima bandia zilizotolewa na mawakala au mashirika yasiosajiliwa.
Kwenye zoezi hilo lililoongozwa na wakuu wa kikosi cha usalama barabarani wa miko miwili ya Pemba, wakishirikiana na watendaji wakuu wa Mamlaka hiyo Tanzania bara na Zanzibar, lilikagua vyombo vya moto 168, ambapo 91 pekee ndivyo zilizogundulika kuwa na bima halali.
Aidha kwenye zoezi hilo, ambalo lilidumu kwa saa zaidi ya nne, lilikamata mtoto Fauz Mohamed Subeit akiendesha gari aina ya ‘spacio, akiwa hajatimiza umri wa mika 18, pamoja na baadhi ya gari za abiria kusajiliwa kama gari binafsi.
Wakizungumza kwenye zoezi hilo, baadhi ya madereva na abiria walilamikia Mamlaka hiyo, kwa kufanya ukaguzi huo pasi na elimu ya uhakiki wa namba za bima kufanyika.
Dereva wa gari ya abiria Abdalla said, alisema pamoja na zoezi hilo kushitukia, lakini pia wenye makosa juu ya ubabaishaji wa namba za bima ni makampuni na wakala, kwa kushindwa kujisajili kwenye Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania ‘TIRA’.
“Mimi gari nimepwa na tajiri niende kazini, na inaonyesha bima imo, sasa kama ni ‘feki’ hili mimi sio kosa langu, maana ilikonunuliwa panajulikana sasa wakamatwe hao wenye vibanda vya kukatia bima”,alieleza.
Aidha dereva Abass Khamis Ali wa gari ya Konde, alisema kosa la madereva bado yeye hajaliona, na kilichojitokeza ni kupotezewa muda wao wa kazi.
“Mimi nadhani hawa Polisi na ‘TIRA’ wengekwenda piga hodi ofisi zote zinazouza bima, na kuangalia namba zao kama zimesajiliwa au la lakini sio kuwakamata madereva”,alishauri.
Kwa upande wake abiria alielazimika kukatisha safari yake, Asha Mzula Khamis wa Kisiwani kwa binti Abeid, alisema kama kuna ukaguzi, Polisi wengewaruhusu madereva kushusha abiria na kisha gari kuzifikisha kituoni.
Akizungumza kabla ya zoezi hilo, mkuu wa kikosi cha usalama barabarani Mkoa wa kusini Pemba, Shawali Abdalla Ali, alisema lazima jambo la kuuza bima isiotambulika likomeshwe, maana linaweza kuikosesha serikali mapato.
“Bima ikiwa haitambuliki kwenye gari ya abiria, hata abiria wenyewe wakikumbwa na ajali, hawana pahala pa kudai fidia”,alisema.
Nae Meneja wa ‘TIRA’ kanda ya Zanzibar Mohamed Ameir, alisema kwa sasa wanaendelea kuwapa elimu polisi, maderava na wananchi wote, kwamba kabla ya kufanya malipo, wanapokata bima za vyombo vya moto, wajihakiki wenyewe.
“Ukishandika neno stika na kuingiza namba ya bima, na kutuma kwenda namba 15200, basi hapo utapa majibu na kuamua kununua bima hiyo au laa”,alisisitiza.

Katika zoezi hilo miongoni mwa gari zilizogundulika kuwa na bima zisizotambulika ni pamoja na gari za abiria na za kutembelea zenye namba za usajili Z 850 AU, Z620 BH, Z197 FT, Z139 FH, Z799 GX, Z626 EK, Z259 EP, na Z 218 FS ambapo baadhi zilikubali kukata bima hapo hapo, na nyengine kuishia mikononi mwa Jeshi la Polisi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.