Habari za Punde

Zaidi ya Makocha 30 Kushiriki Kozi ya Makipa Zanzibar.

Na: Abubakar Khatib Kisandu. Zanzibar.
Kozi ya awali ya makocha wa Magilikipa Visiwani Zanzibar inatarajiwa kufanyika July 5 na kumalizika July 11, 2017 chini ya Mkufunzi Gwiji  Saleh Ahmed Seif “Machupa”.

Kozi hiyo imeandaliwa na Chama cha Soka Zanzibar “ZFA” ambayo itawashirikisha zaidi ya makocha 30 kutoka Unguja na Pemba na makocha hao wakimaliza kozi hiyo watapata fursa ya kutambuliwa na Shirikisho la Soka Barani Afrika “CAF”.

Mtandao huu umemtafuta Mkufunzi huyo Machupa na kutaka kujua matayarisho yanaendeleaje ya Kozi hiyo ambapo amesema kila kitu kipo sawa mpaka sasa na yeye baada ya kuhitimu kozi ya Ukufunzi aliagizwa na CAF kuendesha kozi popote nchini Tanzania.

“Matayarisho yanaendelea vizuri mpaka sasa, mimi niliagizwa na CAF niendeshe kozi kama hizi maana makocha wengi wanafundisha lakini hawana taaluma ya ukocha wa makipa”. Alisema Machupa.

Machupa ni Mkufunzi pekee nchini Tanzania aliyehitimu Kozi ya CAF ya Wakufunzi wa Makocha wa Magolikipa wa ndani kozi ambayo aliisomea nchini Cameroon mwanzoni mwa mwezi Mei mwaka huu,  Machupa pia ameshahitimu kozi ya FIFA ya Ukocha wa Magolikipa ya hatua ya juu (Advanced Level) ambayo aliipata kwenye kozi iliyofayika tarehe 01 Agost, 2016 na kumalizika tarehe 05 Agost 2016, na pia Machupa ana Leseni “B” ya Ukocha inayotambuliwa na CAF.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.