Habari za Punde

Hutuba ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Uzinduzi wa Tamasha la 22 la Mzanzibar Zanzibar.

HOTUBA YA MHE. BALOZI SEIF A. IDDI, MAKAMU WA PILI WA RAIS WA ZANZIBAR KATIKA SHEREHE ZA UFUNGUZI WA TAMASHA LA UTAMADUNI WA MZANZIBARI LITAKALOFANYIKA TAREHE 19 JULAI, 2017 KATIKA UWANJA WA MNARA WA KUMBUKUMBU MICHENZANI - ZANZIBAR

Mhe.  Waziri wa Habari, Utalii, Utamaduni na Michezo,
Mhe. Naibu Waziri wa Habari, Utalii, Utamaduni na Michezo,
Mhe.  Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi,
Ndugu Katibu Mkuu, Wizara ya Habari, Utalii, Utamaduni na Michezo,
Ndugu Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Habari, Utalii, Utamaduni na Michezo,
Ndugu Viongozi mbali mbali,
Wageni Waalikwa Mabibi na Mabwana,
Assalamu Aleikum Warahmatullahi Wabarakatu,
Awali ya yote natumia fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujaalia kufika hapa leo tukiwa wazima wa afya.  Pia natoa shukrani za dhati kwenu Wizara ya Habari, Utalii, Utamaduni na Michezo kwa kunialika kuwa Mgeni Rasmi katika shughuli hii adhimu ya Ufunguzi wa Tamasha la Utamaduni wa Mzanzibari. Naomba nieleze kuwa nimefarijika kwani hii ni hatua muhimu sana katika kukuza na kuendeleza utamaduni wetu.   Ninajua mnaelewa kuwa mimi ni miongoni mwa watunza na waendelezaji wa utamaduni wetu hamkufanya makosa kunialika katika shughuli hii muhimu ya Kitaifa.

Ndugu Wananchi,
Nimeelezwa kuwa kauli mbiu ya sherehe ya mwaka huu ni Tulinde maadili yetu kupinga udhalilishaji.  Kauli mbiu hii ina umuhimu sana katika kukuza mustakbali wa ustawi wa jamii yetu kwani jamii yenye maadili mema huepuka kufanya vitendo vya udhalilishaji wa jamii vyenye kukiuka maadili mema inaweza kuangamia.
Serikali yetu imeandaa mikakati kadhaa kuhakikisha kwamba wale wote wanaodhalilisha watoto na wanawake wanachukuliwa hatua za kinidhamu na kisheria.  Taasisi maalumu zilizomo katika Wizara ya Kazi, Uwezeshaji, Vijana, Wazee, Wanawake na Watoto wakishirikiana na Asasi za Kiraia kama vile TAMWA, ZAFELA pamoja na Madawati ya Watoto zinasimamia kadhia hizi ambazo zinapigwa vita katika Taifa letu na dunia kiujumla.  Ni wajibu wa wazazi kwa ujumla kushirikiana na Serikali na Taasisi zinazohamasisha na kusimamia haki za watoto na wanawake  kuwafichua waovu na sio kuwatetea.
Ni muhimu  kwa jamii, wazee na hata walimu wa skuli na Vyuo vya Quraan kusimamia ipasavyo malezi ya vijana wetu kwa pamoja.   Walimu, ndugu na majirani wana nafasi kubwa ya kusaidiana katika malezi na utoaji wa miongozo kwa watoto.  Ni vyema jamii kuwa tayari kukosoana na kushauriana ili kulinda maadili mema.  Jamii yetu iliishi kwa utamaduni wa “mtoto wa mwenzio ni wako”, na walezi walisaidiana katika malezi bila ya kulaumiana wala kugombana  jambo ambalo liliashiria kuwepo kwa maadili mema katika jamii zetu na kupunguza matatizo ya udhalilishaji.

Ndugu Wananchi,
Wakati akilizindua Baraza la Tisa la Baraza la Wawakilishi, Mhe. Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein alisema, nanukuu:
“Kwa kutambua kuwa utamaduni ni nyenzo muhimu katika kulinda na kudumisha mapenzi, umoja, mila, desturi na silka njema katika jamii, Serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi ilichukua juhudi mbali mbali za kuendeleza na kulinda utamaduni wetu.
Katika kipindi hiki cha pili, Serikali itaendelea na juhudi za kuulinda, kuudumisha na kuutangaza utamaduni wa Mzanzibari kwa kuendelea kuandaa matamasha ya utamaduni.  Aidha, tutawaelimisha wananchi hasa vijana juu ya matumizi bora ya mitandao pamoja na kufanya ukaguzi wa kazi za sanaa mbali mbali.
Tutaendelea na jitihada za kuimarisha lugha ya Kiswahili na kuzifanya lahaja za Zanzibar kuwa ni chimbuko la Kiswahili fasaha.  Vile vile, tutaendelea kuimarisha tasnia ya sanaa kwa kuongeza kasi ya kutafuta na kukuza vipaji vya wasanii pamoja na kuimarisha maslahi yao kwa kuimarisha mfumo uliopo wa matumizi ya hakimiliki”.  Mwisho wa kunukuu.

Suala la kukuza utamaduni wetu sio jambo geni.  Hapo zamani wazee wetu waliuenzi utamaduni huo kwa namna mbali mbali zikiwemo kufanya sherehe za jando na unyago; mfumo ambao ulimtayarisha kijana wa kike na wa kiume namna ya kukabiliana na maisha yake ya baadae.  Pia wazee walitumia hadithi, nyimbo na hata misemo katika kujenga tabia za vijana zinazokubalika katika jamii na Taifa kiujumla.

Ndugu Wananchi,
Nimearifiwa kuwa Wizara ya Habari, Utalii, Utamaduni na Michezo mara hii imeandaa shughuli mbali mbali za kitamaduni, wiki ya tamasha hili ambazo ni imani yangu mtaburudika na kujifunza.

Pia, nimeelezwa kuwa katika tamasha hili kutakuwa na maonesho yatakayoshirikisha vikundi mbali mbali vya wajasiriamali wa kazi za mikono.  Wajasiriamali wanafuata kauli isemayo “utamaduni wako ajira yako”.

Hii ni dhahiri kuwa ndani ya utamaduni wetu tuna hazina itakayotusaidia sana kuongeza kipato.   Ni vyema tuthamini utamaduni wetu na kazi zetu kwani Waswahili wanasema “mkataa kwao mtumwa”.  Utamaduni ni sehemu ya maisha yetu na utalii unaendana na utamaduni. Hivyo, kufanya maonesho ya bidhaa zetu na utamaduni ni njia ya kuutangaza utalii wetu nje ya mipaka ya nchi yetu.

Naelewa kuwa Wizara ya Habari, Utalii, Utamaduni na Michezo imekuwa na desturi ya kushirikiana na Taasisi nyengine zenye kufanya matamasha ya utamaduni kwa lengo la kwenda sambamba na kasi ya kuulinda utamaduni. Matamasha kama vile Tamasha la Filamu la Kimataifa (ZIFF), Tamasha la Mwaka Kogwa, Tamasha la Jahazi na Tamasha la vyakula vya asili la Makunduchi. Hakika Matamasha haya yana mchango mkubwa katika kukuza utamaduni wetu na ni vyema yakadumishwa.

 Ndugu Wananchi,
Napenda nitumie fursa hii kwa mara nyengine kuwapongeza Wizara kwa jitihada zao za kuendeleza urithi tulioupata kwa wazazi wetu. Ninawaomba wanajamii na washiriki wote wa tamasha hili kushirikiana na Wizara katika harakati mbali mbali za kuuenzi utamaduni wetu hasa kwa kuihamasisha jamii kuepuka tabia zisizofaa hasa zile za kuwadhalilisha watoto, wanawake na wenye mahitaji maalumu.
Nami naahidi kuwa niko tayari kuwaunga mkono na kuwa bega kwa bega na Wizara katika kuhakikisha kuwa tunakuwa na mikakati na mipango madhubuti itakayosaidia uendelezaji wa utamaduni wetu kwa faida ya Taifa letu lakini pia kwa urithi wa vizazi vyetu.

Mwisho kabisa, napenda kuwasisistiza tena kuhusu suala la ukuzaji wa maadili na kujiepusha na vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia ili tuweze kurudisha heshima ya Zanzibar ambayo haikuwa tu ni kituo muhimu cha biashara katika karne zilizopita bali ilikuwa ni kitovu cha elimu, heshima, ustaarabu na ukuzaji wa silka, mila, desturi za utamaduni wetu.

Vile vile, ninawaomba watendaji wa Idara ya Utamaduni wawe tayari kushirikiana na Taasisi zote zinazohifadhi, kutunza na kurithisha utamaduni kwa lengo la kukuza na kuendeleza tamasha letu.

 Ndugu Wananchi, Baada ya kusema hayo machache naomba sasa kwa heshima na taadhima kutamka rasmi kwamba Maonyesho ya Tamasha la Utamaduni wa Mzanzibari nimeyafungua rasmi.
Ahsanteni sana kwa kunisikiliza.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.