Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Awatunuku Wahitimu wa Chuo Cha Taifa

Wahitimu wa Chuo cha Taifa cha Ulinzi Tanzania wakiingia kwa maandamano kwenye viwanja vya mahafali ya Tano ya mafunzo yao hapo Kunduchi Jijijini Dar es salaam.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiongoza Timu ya Wahadhiri wa Chuo cha Taifa cha Ulinzi wakingia kwenye viwanja vya Mahafali ya Tano ya Chuo hicho.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akimkabidhi Nishani ya Mwanafunzi bora  Sabrina Seja kutoka Tume ya Takukuru Tanzania baada ya kufaulu vyema katika Shahada ya Uzamili ya Usalama na Strateji.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akihutubia wakati wa hafla ya Mahafali ya Wahitimu wa Chuo cha Taifa cha Ulinzi Tanzania katika Mahafali ya Tano ya Chuo hicho tokea kuanzishwa kwake mwaka 2013.
  Baadhi ya Wahitimu wa Chuo cha Taifa cha Ulinzi waliomaliza mafunzo yao ya mwaka Mmoja.

Baadhi ya Wahitimu wa Chuo cha Taifa cha Ulinzi waliomaliza mafunzo yao ya mwaka Mmoja. Picha na – OMPR – ZNZ.


Na.Othman Khamis OMPR.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema mafunzo makini yanayozingatia nidhamu na uadilifu katika kuwapatia mafunzo ya Uongozi Watendaji wa Serikali na Taasisi mbali mbali za Umma ndio kigezo pekee kitakachoendelea kulinda heshima ya Taifa kwa kuzingatia misingi ya amani na utulivu.


Balozi Seif  alitoa kauli hiyo wakati akiyafunga mafunzo ya Stashahada na Shahada kwa wanafunzi wa mkupuo wa Tano wa Chuo cha Taifa cha Ulinzi Tanzania { NDC } yaliyofanyika katika Kampas ya chuo hicho kiliopo Kunduchi Jijini Dar es salaam.

Alisema uwajibikaji uliotukuka ambao hupatikana ndani ya Taasisi za Umma huongezeka pale Viongozi husika wanaopata mafunzo ya kuwajengea uwezo katika utekelezaji wa dhama wanazokabidhiwa na Umma.

Balozi Seif alisema yapo mabadiliko makubwa ya kiutendaji yaliyokwishapatikana ndani ya Taasisi mbali mbali  za Umma ambazo Viongozi wake wameshapata mafunzo ya kuwajengea uwezo tokea kuanzishwa kwa Chuo cha Taifa cha Ulinzi Nchini.

Alifahamisha kwamba Serikali zote mbili iloe ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na ya Mapinduzi ya Zanzibar zinaendelea kukiunga mkono Chuo cha Taifa cha Ulinzi Tanzania {NDC}katika azma yake ya kuwafinyanga Viongozi na watendaji wa Taasisi za Umma kuwa na utumishi uliotukuka.

Akizungumzia suala la amani Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliviagiza vyombo vya Ulinzi Nchini kuendelea kulinda mipaka, mali na usalama wa Wananchi ili Tanzania iendelee kubakia kuwa kisiwa cha Amani Duniani.

Balozi Seif alisema amani iliyopo Nchini hivi sasa ambayo hata baadhi ya Wananchi wa Mataifa jirani wanaitumia kwa kutafuta usalama wao kutokana na migogoro wanayoikimbia inafaa kulindwa na kuenziwa kwa nguvu zote.

Alisema Serikali zote mbili hazitakuwa na mjadala na kikundi au Mtu yeyoyete katika kuzingatia usalama wa Taifa ambao  juhudi zitachukuliwa wakati wote katika kuhakikisha maisha ya wananchi na raia zake wanaendelea na harakati zao za kimaisha bila ya bughudha yoyote.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliupongeza Uongozi mzima wa Chuo cha Taifa cha Ulinzi Tanzania kwa jitihada unazochukuwa na hatimae kupelekea wanafunzi kutoka Mataifa mbali mbali Duniani kuhamasika na kuamua kujiunga na Chuo hicho.

Mapema Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Ulinzi Tanzania Meja General Yaqoub Hassan Mohamed alisema Chuo hicho kimekuwa kikitoa mafunzo ya Stashahada na Shahada kwa wanafunzi mbali mbali ndani na nje ya Nchi tokea kuanzishwa kwake miaka Mitano ilitopita.

Kamanda Yaqoub alisema mafunzo yanayotolewa chuoni hapo yamejikita katika usalama na Mikakati pamoja na Stashahada ya Uzamili ya Usalama na Mikakati nayayokwenda sambamba na mafunzo ya muda mfupi katika kuwajengea uwezo Makatibu Wakuu , Wakuu wa Mikoa, Wilaya na Wakurugenzi wa Taasisi za Umma.

Mapema Katibu wa Chuo cha Taifa cha Ulinzi Tanzania Brigedia General Mabongo alisema jumla ya wahitimu 10 wa Stashahada ya Usalama na Stratejia wamefanikiwa kutunukiwa tuzo katika Mkupuo huo wa Tano baada ya kufaulu vyema kwenye mafunzo yao.

Brigedia General Mabongo alisema kwa upande wa Shahada ya Uzamili ya Usalama na Stratejia jumla ya wahitimu 35 wamehitimu mafunzo yao miongoni mwao wakapatikana wanafunzi bora waliotunukiwa medani kutokana na umahiri wao.

Alisema wanafunzi hao mchanganyiko na makamanda wa Vikosi tofauti vya Ulinzi wametoka katika Mataifa mbali mbali duniani ikiwemo Rwanda, Afrika Kusini,Zamziba, Zimbabwe, Nigeria, Burundi, Malawi, Kenya, Namibia, Botswana, China na wenyeji Tanzania.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.