Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Afunga Sherehe za Miaka 100 ya Skauti Tanzania Mkoani Dodoma leo.


Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi, akifungwa kiskafu na Kijana wa Skauti Tanzania Jumanne Nyakai kutoka Mkoa wa Singida wakati wa hafla ya kudhimisha miaka 100 ya Skauti Tanzania yanayofanyika katika viwanja vya Chuo Kikuu cha Dodoma na kufunga sherehe hizo za maadhimisho leo
Picha na - OMPR - ZNZ


Na. Othman Khamis OMPR. 
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ametoa wito kwa Wazazi Nchini kuwahamasisha Vijana kujiunga na Skauti ili iwasaidie  kuondokana na vijiwe  ambavyo mara nyingi huwa ni mazalio ya vitendo vya kihuni visivyo hitajika katika Jamii na Taifa kwa ujumla.


Alisema Skauti ni Umoja ambao humjenga Kijana kuwa na tabia nzuri,ujasiri, uadilifu, uzalendo na kumfanya Kijana huyo huyo kuweza kukabiliana na mitihani yake ya  kimaisha.
Balozi Seif Ali Iddi alitoa kauli hiyo wakati akizifunga sherehe za Miaka 100 ya Skauti Tanzania zilizofanyika katika Kampas ya Chuo Kikuu  Mjini Dodoma sherehe zilizotanguliwa na Wiki ya maonyesho ya kazi mbali zinazotekelezwa na Vijana wa Skauti Nchini.

Aliwataka Vijana waendelee kuulinda Umoja wao kwa gharama zozote utakaowavusha tena Miaka mengine Mia Moja  ijayo ili wajenge Skauti yenye nguvu na inayoheshimika ndani ya Nchi na nje ya mipata ya Taifa la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.

Balozi Seif alisema katika kipindi hicho Vijana wa Skauti wamepambana na changamoto nyingi zilizotishia kuhatarisha ustawi wao lakini bado wako imara uliotokana na ushirikiano na mshikamano wao vyenginevyo wangekuwa wameshasambaratika.

Alisema Watanzania wamekuwa wakithaminiwa na kuwa na hadhi Duniani kote kwa kuwa na Tunu ya Amani ambayo Nchi nyingi zinatamani kuwa na Tunu kama hiyo huku zikiendelea kuitafuta kupitia njia mbali mbali bila ya mafanikio yoyote yale.

Balozi Seif alifahamisha wazi kwamba kukosekana kwa amani hakuna maendeleo isipokuwa vurugu, wasi wasi, chuki , visasi maradhi, njaa, ukimbizi,uharibifu kwa Nchi, Wananchi na Mali zao na huchukuwa Miaka mingi kuirejesha Amani iliyopotea.

Akizungumzia suala la Elimu, Balozi Seif  alisema kwa kuwa asilimia kubwa ya Vijana  wa Skauti ni Wanafuzi  waliwaasa kutoacha masomo yao ya kila siku maskulini.

Aliwataka wasome kwa bidii na kuwa mfano mwema kwa Jamii ili wale wanaoamini kujiunga na Skauti ni kupoteza muda  na njia ya kumfanya mwanafunzi asifaulu masomo yake , basi kauli hiyo ifutike katika fikra zao zilizokuwa finyu.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliupongeza Uongozi wa Chama cha Skauti Tanzania  kwa uamuzi wake wa kutoa Tuzo  Maalum kwa Marais Wastaafu pamoja na Watu waliofanya ushujaa na kuonyesha Uzalendo katika Ujenzi wa Taifa hili.

Balozi Seif alisema kitendo cha kuwakumbusha Marasia hao wastaafu inaashiria ni kiasi gani mchango wao umethaminiwa katika jitihada zao za kukiendesha Chama cha Skauti  Nchini Tanzania.

Alisema kwa nioaba ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar alitoa shukrani za dhati kwa Chama cha Skauti Tanzania kwa kuipa heshima Zanzibar ya kuandaa Jamboree ya Mwaka 2019 na kuahidi kwamba heshima iliyotolewa itaenziwa kwa kuandaliwa Jamboree ya aina yake.

Akitoa Taarifa ya Sherehe za Maadhimisho hayo ya kutimia Miaka 100 ya Skauti Tanzania Rais wa Chama cha Skauti Tanzania ambae pia ni Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Tanzania Profesa Joyce Ndalichako alisema sherehe hizo zilizoadhimishwa kwa siku Tisa zimeshuhudiwa na Vijana wa Skauti kutoka Kenya, Uganda, Rwanda, Comoro na Jamuhuri ya Kidemokrasi ya Congo {DRC}.

Profesa Ndalichako alisema Vijana wa skauti walipata mafunzo mbalimbali kama mapambano dhidi ya rushwa, Dawa za Kulevya pamoja na ukakamavu katika kuwajenga kizalendo, maadili pamoja na heshima.

Rais huyo wa Chama cha Skauti Tanzania alitoa wito kwa Vijana na Wanafunzi walioshiriki maadhimisho hayo kuzingatia mambo waliyojifunza pamoja na kuyapeleka kwa wenzao ili lengo la kuanzishwa Skauti Nchini liweze kufanikiwa vyema.

Naye akitoa salamu katika maadhimisho hayo Rais wa Skauti Zanzibar ambae pia ni Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mh. Riziki Pemba Juma alisema Wizara hiyo itahakikisha  katika kuona Vijana wa Skauti wanaendelea kukua katika maadili yanayotakiwa katika Jamii.

Waziri Riziki alisema ukuaji huo unaozingatia maadili ndio njia pekee itakayohakikisha kwamba Taifa linaelekea kwenye mfumo unaokubalika kiheshima, nidhamu pamoja na utiifu.

Mapema Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akikagua maonyesho mbali mbali ya Vijana wa Skauti kutoka Mikoa yoteya Tanzania Bara na Zanzibar, kutoa Nishani mbali mbali, Tuzo pamoja na vyeti vya shukrani.

Zaidi ya Vijana Elfu 4,500 wa Skauti kutoka Mikoa yote ya Tanzania walikuwepo Mkoani Dodoma tokea Tarehe 21 Julai kwenye wiki ya Maadhimisho hayo ya Miaka 100 ya Skauti Tanzania na kushiriki katika shughuli mbali mbali ikiwemo maonyesho.

Pia sherehe hizo zilishuhudiwa na Vijana wa Skauti kutoka  Mataifa Jirani na Rafiki ya Kenya, Uganda, Rwanda, Comoro pamoja na Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo {DRC}.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.