Habari za Punde

Serikali za Wananchi ziko wapi?Waziri Mkuu wa Tanzania, Mhe Kassim Majaliwa hivi karibuni alipokuwa ziarani mkoani Lindi alikaririwa na vyombo vya habari akihoji hali tete ya usalama iliyoshuhudiwa na kuendelea kushuhudiwa Kibiti. 

Hata hivyo yanayotokea Kibiti si mageni ingawa huenda yakawa yanatafautiana kimtindo na yanayotokea sehemu zengine nchini. 

Hakika hali iliyopo Kibiti inazua masuali mengi na ningependa kama mwananchi niizungumzie kwa upande wa ulinzi na usalama ukizingatia dhana ya utawala. Na ili kujenga hoja yangu sitaki kujikita katika nadharia pekee bali kuoanisha tukio hili na hali halisi.

Nina eneo langu hapo Bunju A, Mtaa wa Kisanga.  haoa jiji Dar es salaam. Eneo hilo nimelipata toka mwaka 1991. 

Wakati nalipata eneo hilo jirani zangu walikua watu wane tu na wala walikua hawako karibu. Kwa vile tumekuwa hatuna mwelekeo wa kifisadi tumekuwa tunaendeleza sehemu zetu kadri mifuko yetu ilivyoruhusu.

Hafla ilipoingia milenia, tukashuhudia wimbi la watu wenye pesa za ajabu na kibri cha ajabu wanakuja kutafuta maeneo. Nimeshuhudia misitu ikikatwa ili kutoa viwanja hata sehemu za makaburi. 

Kamwe Serikali za Kijiji na hata Mamlaka za Mtaa, Kata au Wilaya hazijaingilia kati ingawa kukata mti bila kibali ni kosa. 

Sijaona Idara ya Misitu au Mamlaka zinazosimamia Mazingira kuhoji au kuchukua hatua ingawa binafsi nimefanya bidii ya kuwaarifu. Hivyo wananchi wamejijengea ujasiri wa kufanya uharibu wa mazingira kwa vile hakuna mamlaka inayosimamia, kufuatilia au kuhoji hata pale sheria zinapovunjwa waziwazi.

Hivi karibuni kumeanzishwa zoezi la ulinzi shirikishi sambamba na polisi jamii mtaani kama ilivyo kwa maeneo mengi nchini. Wahusika wa kuhakikisha ulinzi ni wakaazi wa eneo husika. Waratibu ni Serikali za Mitaa husika na hususan kamati za Ulinzi na Usalama. Wananchi wanatakiwa kuchangia zoezi hili ili kuhakikisha uendelevu wake. Mwisho wa siku wakaazi wanachangia kwa mategemeo ya uhakika wa usalama.

Suali linazuka je tunalindwa dhidi ya wahalifu wanaotoka nje na Mtaa wetu au tunajilinda dhidi ya Uhalifu wa kila aina?

Juzi jirani yangu aitwaye Bw. Costa Mushi, mtu anayesemekana ni mzee wa Kanisa, na mtu aliyehudumu katika ofisi si kama ni jahili, kaingia kwangu na kujimegea sehemu ya ardhi ambayo mpaka tarehe 6 Julai 2017 ilikuwa ndani ya uzio wangu. 

Ili kufanikisha uroho wake kafyeka michongoma yangu na miarubaini mipevu nilopandisha toka nimehamia hapo na kupaendeleza. Lengo lake kupoteza ushahidi wa mpaka uliopo.

Mroho huyu kalirubuni Baraza la Kata, Jeshi la Polisi na wananchi wengine kutimiza azma yake eti kwa kuniwekea 'Stop Oder' inayomruhusu yeye kunivunjia, kunibomolea na kujenga ndani kwangu bila idhni, bila taarifa bila fidia. Kaamua kutwaa wamemruhusu na kumlinda kufanya hivyo.

Najiuliza serikali za wananchi ziko wapi? Hakuna Mwenyekiti wa Mtaa aliyeona na kutambua kuna jambo ovu linatokea? Polisi walipoletwa kusimamia  uvamizi huu hawajaona kuwa kinachofanyika ni dhulma na ni kinyume na sheria wanaotakiwa kuilinda? Baraza la Kata lilikuwa na Mamlaka gani kisheria kuidhinisha ukataji wa miti na uporaji wa eneo la mtu bila ya anayechukua kuonyesha yeye kapapata vipi?

Aidha itambulike kuwa Baraza la Kata likijua kuwa mporaji huyo ni Mvamizi kwani alikwisha kiri mbele ya Baraza hilo kuwa hiyo sehemu si yake alipojaribu kupandikiza nguzo sehemu husika na kusutwa kwa kufanya hivyo.

Watu wengi waliokuja kukagua kilichotokea wameshauri kwenda mahakamani. Kweli? Kwa lipi? Kwani serikali ya mtaa hawajaona kuwa haramu imetendeka? Serikali ya Kata haijaona kuwa haramu imetendeka? Kamati ya Ulinzi na Usalama hawajaona kuwa haramu imetendeka?
Hivyo, ziko wapi hizo serikali za wananchi? Mbona haziwajibiki?

Kwa nini suala likaamuliwe na taasisi iliyo mbali na tukio wakati zipo taasisi na mamalaka karibu na tukio, ndani ya himaya yao kiutawala, taasisi na mamlaka ambazo kisheria ndizo zinazohusika? Ndio maana kesi hazishi mahkamani maana hata kwa masuala ya kiutawala jibu ni kwenda  mahkamani!

Kweli tutegemee kuwa vyombo vya mbali ndio vitasimamia haki wakati vyombo vya kuhakikisha na kusimamia utawala bora katika makaazi yetu havijitambui kimajukumu, kiweledi na havioni haja ya kusimamia haki kwa uadilifu?

Kazi kweli!

Mategemeo yangu ni kuwa mwenye jukumu la mkoa atasimamia watendaji wake;  mwenye jukumu la wilaya atasimamia na kuwawajibisha watendaji wake, kuwa waliopewa dhamana ya Serikali ya Mtaa/Kijiji na wale wote walioshiriki katika haramu hii wajibu kwa raia wanaotii sheria imekuwaje wameamua kuizamisha jamii ya Kisanga Bunju A katika ujangili wa ardhi? 

Ndio kutakuwa na amani na usalama hapa? Ndio kutakuwa na mshikamano wa wakaazi? Baya zaidi funzo gani kwa raia waliobaki? Sasa tunaruhusu kila mtu kujisaidia/kupora cha mwenzake bila kujali tabu aliyoipata mwenze kupata1

Tanzania tunayoitaka ni pepo ambamo watu  wanaheshimu sheria na haki za wengine na pia ni nchi ambamo taasisi na wananchi kwa ujumla, zinawajibika kuhimiza na kuhakikisha utawala bora. Pia ni pepo ambamo haki hazibaki kuwa dhana. Badala yake zinageuka kuwa matumaini hai na  halali kwa kila mwananchi ikiwa ndio kipimo/kielelezo cha kujitawala kwa wananchi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.