Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt.
Harrison Mwakyembe (kulia) akifafanua jambo kwa waandishi wa habari (hawapo
pichani) wakati akisitisha uteuzi wa Mwenyekiti pamoja na wajumbe wa Baraza la
Michezo Tanzania (BMT) mapema hii leo jijini Dar es Salaam, katikati ni Mkurugenzi
wa Idara ya Michezo Yusuph Singo na
kushoto ni Msajili wa Vyama vya Michezo nchini Bw. Ibrahim Sapi Mkwawa.
Picha na Eliphace Mrawa - Maelezo
Na. Shamimu Nyaki WHUSM
Waziri wa Habari
Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Dkt Harrison Mwakyembe, amesitisha uteuzi wa Mwenyekiti na Wajumbe
wote wa Baraza la Michezo la Taifa kuanzia leo Julai 10 2017 kufuatia Baraza
hilo kushindwa kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta ya Michezo.
Akizungumza na
Waandishi wa Habari Jijini Dar es Salaam
leo Dkt Mwakyembe ameeleza kuwa, amelivunja Baraza hilo kwa mamlaka aliyopewa
na Sheria ya BMT Na.12 ya mwaka 1967 iliyofanyiwa marekebisho na Sheria Na.6 ya
mwaka 1971 pamoja na kanuni zake za mwaka 1999.
Waziri Mwakyembe
amechukua uamuzi huo kutokana na maagizo aliyopewa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.
Kassim Majaliwa katika hotuba yake ya kuahirirsha Bunge Mjini Dododma Julai 5
mwaka huu, ya kufanya mapitio na kulitathmini upya Baraza hilo.
“Mhe. Waziri
Mkuu Kassim Majaliwa aliniagiza
nilifanyie mapitio na kulitathmini upya Baraza la Michezo la Taifa (BMT) ili
kujiridhisha na usimamizi wake wa shughuli za michezo nchini, na kwamba ikidhihirika kwamba usimamizi wa BMT
wa michezo nchini si imara basi ninaweza kulivunja Baraza lililopo na kuunda
upya.” Alisema Waziri Mwakyembe.
Aidha Waziri
Mwakyembe ameeleza kuwa Baraza hilo limeshindwa kutafuta njia bora za kuondoa
changamoto ambazo zilikua zinahitaji utashi na dhamira ya kujituma, ikiwemo Viongozi wa michezo kushika nafasi
zaidi ya moja, kushindwa kusimamia ushiriki wa wanamichezo wa Tanzania na wa nje
katika michezo mbalimbali.
Pia Waziri Mwakyembe
alizitaja sababu nyingine za kuvunjwa kwa BMT kuwa ni Uchaguzi wa vyama vya michezo nchini kugubikwa
na ubabe na rushwa, mapromota wa mchezo wa ngumi nchini kuendesha shughuli zao
bila kusajiliwa, pamoja na kanuni za vyama vya michezo kukosa uhakiki wa kubaini upungufu kuhusu masuala ya fedha.
Hata hivyo
Sektretarieti ya Baraza itaendelea
kufanya kazi katika kipindi hiki kwa kushirikiana kwaukaribu na Wizara ya
Habari Utamaduni Sanaa na Michezo wakati taratibu za kumpata mwenyekiti na
wajumbe wapya zikiendelea kufanyika kwa mujibu wa Sheria.
No comments:
Post a Comment