Habari za Punde

Wanaokodi mikarafuu wapewa darsa Pemba

Na. Haji Nassor, Pemba.
WANANCHI wenye dhamiria ya kukodi mashamba ya mikarafuu kutoka kwa wamiliki wa mashamba hayo, wametakiwa kutokukubali kufanya hivyo, pasi na kuwepo kwa wamiliki wa mashamba waliopakana nayo, ili kujikinga na utapeli unaofanywa na baadhi ya wamiliki, kwa kuongeza idadi ya mikarafuu.
Ushauri huo umetolewa na baadhi ya matajiri waliokodi kisiwani Pemba, na kujikuta kukodi shamba lililokodishwa na watu zaidi ya mmoja au kuongezewa idadi ya mikarafuu, iliompakani, ambayo sio ya mwenye shamba husika.
Walisema haipendezi kwa mtu anaetaka kukodi shamba la mikarafuu, bila ya kuwepo kwa wamiliki wa pembe nne za shamba husika, vyenginevyo migogoro ya makusudi inayoweza kuibuka wakati wa kuvuna zao hilo.
Mmoja kati ya waliokumbwa na utapeli huo, Hamad Ali Ramadhan wa Wete alisema, yeye alionyeshwa shamba eneo la Kigope Mkoani, kwa lengi la kulikodi, wakati shamba hilo tayari lilishakodiwa na mkwe wake, wiki tatu zilizopita.
Alisema, shamba hilo ambalo tayari limeshakodishwa lilikuwa la familia, hivyo warithi hao kila mmoja alikuwa na dhamira ya kulikodisha kwa wakati wake, jambo ambalo lingeweza kuleta migogoro wakati wa uvunaji.
“Mkwe wangu alikodi shamba hilo kwa shilingi milioni 8, (8,000,000) na kisha kuwakabidhi watu na yeye kurudi anakoishi Nairibi Kenya, lakini juzi nusura likodishwe tena mara mbili”,alifafanua.
Shamba hilo linalomilikiwa na familia ya watu sita, tayari wameshakutana na kujadili namna kwa aliekodi kurejeshewa fedha zake, chini ya uongozi wa sheha na mrithi mmoja aliwageuka wenzake na kulikodisha inasemekana alipewa shilingi milioni 6.
Aidha Hassan Haji Vuai wa mjini Chakechake, yeye alisema alikubali kukodi shamba liliopo eneo la Ngomeni, na wakati siku anakwenda kukabidhi fedha, ndipo alipotokezea mtu waliepakana na hatimae mikarafuu 10, ilishakodishwa wakati sio halali kwa mwenye shamba.
“Baada ya kuona hivyo alitaka kunikodisha ugomvi, niliamua kurejea na fedha zangu shilingi milioni 5,000,000 na kwenda Mgelema na huko nimeshakodi shamba chini ya wamiliki wa wote wanne waliolizunguruka shamba hilo.
Nae mmiliki wa shamba hilo, liliopo Ngomeni Ahmed Al-hassan Mohamed, amesema ni kwa muda mrefu alikuwa hajalikagua shamba lake, na wala hakuwa na nia ya kuichukua mikarafuu hiyo.
“Mimi hili shamba analo mtu kwa miaka kadhaa, sasa juzi akaja akanionyesha lakini hii mikarafuu 10 iliingia kwa bahati mbaya, wala sio nia yangu”,alisema.
Kwa upande wake, sheha wa shehia ya Mgelema Omar Iddi Zaina, aliwatahadharisha wananchi wanaotaka kukodi mashamba hasa ndani ya shehia yake, wasikubali kufanya hivyo, pasi na kuwepo uongozi wa shehia.
“Kama wakihisi sheha hawamuhitaji, basi kabla ya kukodi wawapate waliopakana na shamba wanalotaka kulikodi, ili kuepusha utapeli unaoweza kufanywa”,alifafanua.
Maeneo ambayo tayari kumesharipotiwa ukiukwaji wa mipaka au shamba moja kukodishwa zaidi ya mara moja ni pamoja na Mtambile, Jungani, Mkanyageni, Wambaa, Mgelema, Ngomeni na Ziwani.

Msimu mpya wa uvunaji wa zao la karafuu unatarajiwa kuanza wakati wowote kuanzia sasa, huku ukitajwa kuwa ni miongoni mwa msimu mkubwa wa uvunaji ambao haujawahi kuwepo miaka 10 iliopita .

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.