Habari za Punde

Zanzibar Kuwabana Kisheria Wavuta Sigara Hadharani.

Naibu Waziri wa Afya Zanzibar Bi. Harusi Said Suleiman akikata utepe kuashiria uzinduzi wa kitabu cha kanuni ya kuzibiti matumizi ya tumbaku Zanzibar (kushoto alieshika kitabu) ni Mwakilishi wa Shirika la Afya Duniani Dr. Matthieu Kamwa.
Naibu Waziri wa Afya Zanzibar Bi. Harisi Said Suleiman na Mwakilishi wa Shirika la Afya Duniani Dr. Matthieu Kamwa wakionyesha Kitabu cha kanuni ya kuzibiti matumizi ya tumbaku Zanzibar kilichozinduliwa leo Wizara ya Afya Zanzibar.
Katibu Mkuu Wizara ya Afya Zanzibar Bi. Asha Ali Abdallah akizungumza na walikwa katika uzinduzi wa kanuni ya udhibiti wa tumbaku uliofanyika ukumbi wa Wizara ya Afya Zanzibar. Kulia mwakilishi wa Shirika la Afya Duniani Dr. Matthieu Kamwa.
Naibu Waziri wa Afya Zanzibar Bi. Harusi Said Suleiman wa (katikati) katika picha ya pamoja na viongozi wa WHO pamoja na watendaji wa Wizara ya Afya Zanzibar.

Picha na Makame Mshenga.

Na Mwashungi Tahir.Maelezo 
Wizara ya Afya imezindua kanuni ya udhibiti wa matumizi ya Tumbaku ikiwa ni mkakati wa kupambana na ongezeko la Matumizi ya Tumbaku kwa jamii ya Zanzibar.
Hafla ya uzinduzi huo imefanywa na Naibu Waziri wa Wizara hiyo Harusi Saidi Suleiman huko Wizara ya Afya mnazi mmoja.

Akizungumza katika hafla hiyo Naibu huyo amesema jamii  ya kizanzibari inakabiliwa na changamoto kubwa ya matumizi ya tumbaku ikiwemo uvutaji wa sigara.
Amesema Sigara ni bidhaa halali inayoingizia Serikali mapato kupitia kodi, hata hivyo mbali na mapato yanayopatikana , matumizi yake yamethibitika kuwa ni athari kubwa mno kwa mtumiaji pamoja na wanaomzunguka .

“Ifahamike kuwa tumbaku ina aina nyingi ya sumu ikiwemo NIKOTIN ambayo  inasababisha uraibu na husafirishwa kwa njia ya mzunguko wa damu na kuathiri sehemu mbali mbali za mwilini” alisema Naibu huyo.

Alisema tafiti zilizofanywa ulimwenguni zinafahamisha kuwa matumizi ya tumbaku ikiwemo uvutaji wa sigara hupelekea kupata maradhi yasiyoambukiza ikiwemo Saratani za mapafu, kinywa, shingo ya kizazi , ugonjwa wa shinikizo la damu  na kisukari .

Aliongeza kuwa matumizi yake huathiri pia mfumo mzima wa mishipa ya damu, maradhi sugu ya kuziba njia ya hewa kusababisha maradhi ya kiharusi.

Akielezea kuhusu Utafiti uliofanyika Zanzibar mwaka 2011 Naibu huyo alisema asilimia 7.3 ya watu katika jamii ni watumiaji wa Sigara na bidhaa zitokanazo na tumbaku, na kwa upande wa wanafunzi tafiti ndogo zilizofanyika imebainika skuli zaidi ya nane zilizomo wilaya ya mjini  asilimia 9.5 ya wanafunzi wanatumia bidhaa zitokanazo na tumbaku ikiwemo sigara.

Akizitaja changamoto katika jamii alisema ni matumizi holela ya tumbaku hususan uvutaji wa sigara katika maeneo ya uwazi kama vile  majengo yanayotoa huduma za kijamii, maeneo ya burudani, sokoni, viwanja vya mpira.

Naibu huyo alieleza kuwa Zanzibar inashuhudia watoto chini ya umri wa miaka 18 wakishirikishwa kwa njia moja au nyengine katika matumizi hayo na kwamba ipo haja wazazi na walezi kuwa na hadhari kwa watoto wao.

Ameviomba vyombo vya habari na vyombo vya sheria kuzipitia na kuzisimamia kanuni hizo ili kuweza kukabiliana na changamoto za matumizi hayo ikiwa ni pamoja na kuhakikisha mtu atakayeuza bidhaa ya tumbaku ikiwemo sigara lazima bidhaa hiyo iambatane na onyo la afya liililochapishwa kwa wino mwekundu na inayosomeka vizuri.

Kanuni hizo pia zinakataza mtu yeyote chini ya umri wa miaka 18 kutoruhusiwa kujishughulisha na kuuza sigara au kushiriki katika bidhaa ya tumbaku na kanuni inakataza kudhamini na kuhamasisha bidhaa hii ikiwa nchini au nje ya nchi kupitia vyombo vya habari na matangazo yanayohamasisha matumizi ya tumbaku.

Nae Mwakilishi wa Shirika la Afya duniani WHO Dr Matthieu Kamwa  amesema tumbaku ni miongoni mwa bidhaa zinazoongoza kusababisha vifo kwa watumiaji wake ambapo zaidi ya watu million saba hufariki duniani kote kutokana na matumizi yake.

Mwakilishi huyo amesema Tumbaku ni janga kubwa ambalo linagharimu uchumi wa dunia ambapo takriban dola za Marekani Tirion 1.2 hutumika kwa ajili ya matibabu ya watumiaji wa tumbaku.

Ameongeza kuwa  Shirika la afya ulimwenguni litaendelea na mashirikiano yake na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kutengeneza kanuni zake dhidi yamatumizi ya tumbaku .

“Malengo endelevu ya dunia ni kuona dunia iko salama dhidi ya matumizi ya tumbaku ifikapo 2030  na ni jambo linalohitaji mashirikiano ya kila mdau katika kuhakikisha wanaepukana na matumizi hayo” alisema Kamwa.

Kwa upande wake Katibu mkuu wa wizara ya Afya Asha Ali Abdullah akizungumza katika uzinduzi huo alisema tumbaku ni miongoni mwa Madawa ya kulevya hivyo ameomba elimu itolewe ili watumiaji waelewe athari zake hasa kwa vijana ambao ni nguvu kazi ya taifa la kesho.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.