Habari za Punde

Naibu Waziri wa Elimu Apokea Cheti cha Shukran kutoka Taasisi ya Rafiki

Na Ali Othman.

Naibu waziri wa Elimu na mafunzo ya Amali Mh. Mmanga Mjengo Mjawiri amepokea Cheti cha shukrani kutoka kwa Taasisi ya Rafiki Network kutokana na juhudi na mchango wake mkubwa aliotoa katika kufanikisha Bonanza la kihistoria la kimichezo lililoandaliwa na taasisi hiyo kisiwani Pemba.

Akizungumza mara baada ya kukabidhiwa cheti na  Rais wa Taasisi ya Rafiki Network Bw. Hamad Hamad ofisini kwake Mazizini nje kidogo ya mji wa Zanzibar, Mh Naibu Waziri amesema ipo haja ya kufufua michezo iliyosahauliwa ya Kipemba ili kuibua burudani ambazo amesema kwasasa zimekua adimu.

“Watu wanataka burudani kwasababu zimekua adimu hivyo ni vizuri kuendelea na kufufua michezo iliyosahauliwa ikiwemo michezo ya kivita ya kipemba (martial arts) kama vile Ngware na Kirumbizi” Amesema Mh. Mmanga.

Akielezea juu ya kuridhishwa kwake na juhudi za Taasisi ya Rafiki Network katika kuandaa na kusimamia Tamasha la kimichezo kisiwani Pemba lijulikanalo kama “Pemba Weekend Bonanza”, Mheshimiwa Naibu Waziri amesema Taasisi ya Rafiki Network imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kuamsha hisia za watu kiburudani zinazohusiana na michezo yao ya kiasili.

Aidha Mh. Waziri amesema burudani zimekua adimu kisiwani Pemba ambapo ametumia kigenzo cha wananchi kujitokeza kwa wingi katika tamasha la Pemba Weekend Bonanza kuwa ni ishara tosha ya kuadimika kwa michezo na burudani kisiwani Pemba. Ameongeza kua michezo ni muhimu sana kwa kuwaunganisha watu.

Taasisi ya Rafiki Network iliandaa tamasha kubwa la Kimichezo Kisiwani Pemba ambalo lilifanyika kuanzia tare 28 hadi 30 Julai ambapo michenzo mbalimbali ikiwemo mchezo wa Ng’ombe, Resi za Baiskeli, Mashindano ya Kuogelea na Resi za Ngalawa yalifanyika ambapo washindi na washiriki walizawadiwa.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.