STATE
HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF
THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 19.08.2017
RAIS wa Zanzibar
na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ameeleza kuwa
kutokana na kasi ya Serikali anayoiongoza katika kuimarisha miundombinu ya
michezo ana matumaini makubwa kuwa sekta hiyo itazidi kuimarika na kuitangaza
zaidi Zanzibar katika medali ya michezo ndani
na nje ya nchi.
Dk. Shein aliyasema hayo leo alipofanya mahojiano
na waandishi wa Habari mara baada ya kukagua ujenzi wa Uwanja wa Mpira wa
MaoTse Tung, uliopo mjini Unguja, ambao unajengwa upya kwa msaada wa Serikali
ya Jamhuri ya Watu wa China, wakati akiwa katika ziara yake katika Mkoa wa
Mjini Magharibi.
Katika maelezo yake, Dk. Shein alisema kuwa Serikiali
ya Mapinduzi ya Zanzibar imo katika juhudi kubwa za kuimarisha miundombinu ya
michezo vikiwemo viwanja vya mpira ambavyo vitajengwa katika Wilaya zote Unguja
na Pemba pamoja na kuvifufua vya zamani kama kiwanja hicho cha Mao Tse Tung.
Dk. Shein alisema kuwa uwanja huo utakapokamilika
mbali ya kuwa na viwanja vya mpira wa miguu viwili pia, kutakuwemo na viwanja
vyengine vya michezo ya ndani pamoja na viwanja vya mpira wa kikapu, mpira wa mikono,
mpira wa meza kiwanja cha mazoezi ya kunyajua vitu vizito na mashine zake pamoja
na michezo mingine midogo midogo.
Aidha, Dk. Shein alisema kuwa kiasi cha TZS
Bilioni 11 zinatarajiwa kutumika kati ujenzi wa kiwanja hicho hadi kumalizika
kwake ikiwa ni msaada kutoka Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China.
Dk. Shein alitumia fursa hiyo kutoa pongezi kwa
Jamhuri ya Watu wa China kwa kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha
miradi ya maendeleo ukiwemo mradi huo wa
ujenzi wa uwanja wa Mao Tse Tung na kusisitiza kuwa China ni marafiki wa kweli.
Alieleza kuwa Serikali ya Jamahuri ya Watu wa China
imezidi kuvutika na ujenzi huo hasa kutokana na historia ya uwanja huo ambao
una jina la kiongozi wa kwanza wa Taifa hilo marehemu Mao Tse Tung.
Dk. Shein alieleza kuwa ujenzi wa uwanja huo ni
miongoni mwa mafanikio ya utekelezaji wa ahadi za Serikali ya China iliyotokana
na ziara yake aliyoifanya nchini humo ambapo mbali ya mradi huo pia, kulikuwemo
na miradi mingine ukiwemo mradi wa ujenzi wa Bandari ya Mpaigaduri pamoja na jengo
la abiria katika uwaja wa ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume.
Aliongeza kuwa kukamilika kwa uwanja huo kutatoa
nafasi kubwa ya kutekeleza azma ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuimarisha
sekta ya michezo hapa nchini.
Pamoja na hayo, Dk. Shein alieleza kuwa michezo ina faida kubwa ikiwa ni pamoja na
kupelekea watu kujuana, kupendana pamoja na kushirikiana sambamba na kujenga
udugu.
Mapema Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni,
Utalii na Michezo Omar Hassan King alieleza kuwa katika eneo hilo kutakuwa na
viwanja viwili vya mpira wa miguu ambavyo viwanja hivyo vitakuwa na sifa zote
za kimataifa vitakavyokuwa na urefu wa mita 105 kwa 68.
Aidha, aliongeza kuwa kiwanja hicho kitakuwa na
eneo la Wageni Mashuhuri (VIP), uwanja ambao utakuwa na milango sita pamoja na
majukwa ambayo yatakuwa na uwezo wa kuchukua watazamaji 1500.
Katibu Mkuu huyo alieleza kuwa uwanja huo
unatarajiwa kumalizika mwezi Machi mwakani kwa mujibu wa makubaliano na Kampuni
ya Ujenzi kutoka nchini China iitwayo ZHENGTAI GROUP huku akisisitiza kuwa
ujenzi huo unaendelea vizuri.
Nae Balozi Mdogo wa China anaefanya kazi zake hapa
Zanzibar Xie Xiuowu alimuhakikishia Dk. Shein kuwa uwanja huo utamalizika kwa
wakati.
Rajab Mkasaba, Ikulu
Zanzibar
Postal Address:
2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment