Habari za Punde

Rais wa Zanzibar Dk. Shein Azungumza na Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Kiswahili Afrika Mashariki. Ikulu Zanzibar.

STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
  Zanzibar                                                                                                               29.08.2017
---
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, viongozi pamoja na wananchi wake wataendelea kuiunga mkono Kamisheni ya Kiswahili ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa lengo la kuiimarisha lugha ya Kiswahili ambayo inaendelea kujipatia umaarufu mkubwa duniani kote.

Dk. Shein aliyasema hayo wakati alipokuwa na mazungumzo na Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Kiswahili ya Jumuiya ya Afrika Mashariki Profesa Kenneth Linyani Simala, Ikulu Mjini Zanzibar.

Katika Mazungumzo hayo, Dk. Shein alisema kuwa kuna kila sababu ya kuendelea kuiunga mkono Kamisheni ya Kiswahili ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ambayo kwa hivi sasa Makao makuu yake yapo hapa Zanzibar kwa kutambua kuwa asili na chimbuko la lugha ya Kiswahili ni Zanzibar.

Alieleza kuwa Zanzibar imefarajika kwa kiasi kikubwa kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki kufanya uwamuzi wa makusudi wa kuyaweka makao makuu ya Kamisheni hiyo hapa Zanzibar kwani Zanzibar inahistoria kubwa ya lugha ya Kiswahili.

Alisisitiza kuwa Afika Mashariki ndio wenye Kiswahili hivyo ni jambo la busara kuwepo kwa  Kamisheni hiyo ambayo itaendeleza na kukikuza Kiswahili ili kizidi kuimarika.

Dk. Shein alisema kuwa Kiswahili ni lugha tajiri na maarufu sana ulimwenguni hivyo kuna haja ya kuchukua juhudi za makusudi katika kuhakikisha lugha hiyo inazidi kuimarika na kupata mafanikio makubwa zaidi.

Aidha, Dk. Shein alieleza matumaini yake makubwa ya uongozi wa Katibu Mtendaji huyo Profesa Simala katika kuiendeleza na kuiongoza Kamisheni hiyo muhimu kwa nchi za Afrika ya Mashariki.

Sambamba na hayo, Dk. Shein alieleza haja ya kukiimarisha zaidi Kiswahili pamoja na kukipa hadhi yake katika kukizungumza hasa katika mikutano ikiwemo ya Jumuiya hiyo na mengineyo huku akieleza kusikitishwa kwake na baadhi ya mikutano inayowashirikisha wahusika wengi waswahili hapa nchini lakini huendeshwa kwa lugha ya kiengereza kwa kisingizo cha udhamini wa mikutano hiyo.

Dk. Shein alieleza kuwa hali hiyo ni kinyume na nchi nyengine duniani ambazo zinakuza, zinathamini na kuimarisha lugha zao ambazo huzipa kipaumbele kwa kutambua umuhimu wake katika kuzipa hadhi lugha zao.

Kutokana na hali hiyo, Dk. Shein alieleza haja ya kukizungumza Kiswahili ili kizidi kuimarika na kukijengea heshima na hadhi yake kama ilivyo kwa baadhi ya nchi nyengine duniani ambazo hutumia lugha zao kama lugha za taifa ambapo hutumia hata kusomeshea katika vyuo vyao vikiwemo vyuo vikuu.

Nae Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Kiswahili ya Jumuiya ya  Afrika Mashariki Profesa Kenneth Linyani Simala  alitoa shukurani za dhati kwa Dk. Shein kwa juhudi kubwa zilizochukuliwa na Serikali yake anayoiongoza kwa kuipokea Kamisheni hiyo pamoja na kuipa jengo ambalo kwa sasa ndio makao makuu ya Kamisheni hiyo.

Kutokana na juhudi hizo za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, pamoja na zile za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Katibu Mtendaji huyo alieleza kuwa mafanikio makubwa yatapatikana katika kukiimarisha Kiswahili kutokana na mashirikiano hayo.

Aidha, Profesa Simala alimueleza Dk. Shein kuwa Kamisheni hiyo imeweza kukutana na wadau mbali mbali na kuunda  mpango mkakati  ambao utazinduliwa  katika Kongamano la Kiswahili la kwanza linalotarajiwa kufanyika hapa Zanzibar.

Aliongeza kuwa Kongamano hilo linatarajiwa kuwashirikisha wajumbe 150 kutoka nchi wanachama zote za Jumuiya ya Afrika Mashariki pamoja na wajumbe kutoka Uturuki, Burundi, DRC Congo, Burundi, Rwanda, Namibia, Wanahabari, wanasiasa na washiriki wadau wengine kutoka nchi mbali mbali duniani.

Alieleza kuwa miongoni wma mambo ambayo wajumbe hao watajifunza ni pamoja na kuijua historia ya Zanzibar na baadae ripoti itatolewa kwa viongozi wa nchi zote za Jumuiya ya Afrika Mshariki.

Profesa Simala alitumia futsa hiyo kumueleza Rais Dk. Sheinazma ya Kongamano hilo la kwanza la Jumuiya ya Afrika Mashariki ambalo linatarajiwa kufanyika hapa Zanzibar kwa mara ya kwanza kuanzia tarehe 6 hadi tarehe 8 mwezi ujao.

Sambamba na hayo, Profesa Simala alimueleza Dk. Shein miongoni mwa majukumu ya Kamisheni hiyo kuwa ni kuwaweka pamoja wadau wa lugha hiyo ya Kiswahili huku akieleza kuwa tayari kwa upande wa nchi za nje ya Jumuiya ya Afrika ya Mashariki zimeshatambua umuhimu wa lugha ya Kiswahili ikilinganshwa na nchi husika za Jumuiya hiyo.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 
 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.