Mwenyekiti wa kamati ya Ardhi na
Mawasiliano wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar Mhe. Hamza Hassan Juma (mwenye
koti jeusi) akielezea jambo wakati wa ziara ya kamati hiyo ilipokutana na
mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri-TMA na menejiment ya TMA (hawapo pichani),
kwenyea ukumbi wa mikutano wa TMA, Ubungo Plaza.
Siku
ya Ijumaa, tarehe 25/08/2017, Kamati ya Ardhi na Mawasiliano wa Baraza la
Wawakilishi la Zanzibar ilitembelea Makao Makuu ya Ofisi za Mamlaka ya Hali ya
Hewa Tanzania (TMA) yaliyopo jengo la Ubungo Plaza Dar es salaam ili kuona na kupata taarifa mbali mbali za
taasisi hiyo.
Taarifa
ya utendaji ya TMA iliwasilishwa na ndugu Selemani Selemani (Mchumi) pamoja na
mambo mengine aliwafahamisha wajumbe wa kamati hiyo kuwa Mamlaka imepokea
‘Certificate of Appreciation’ toka Idara ya kukabililiana kamisheni ya
kukaliana na maafa na Mamlaka ya usafiri
wa majini (ZMA) kwa kazi nzuri inayofanywa ya kutoa huduma za hali ya hewa
katika visiwa vya Unguja na Pemba.
Akizungumza
kwa niaba ya wajumbe, Mwenyekiti wa kamati hiyo ya Ardhi na Mawasiliano wa
Baraza la Wawakilishi Zanzibar Mhe. Hamza Hassan Juma alisifu kazi nzuri inayofanywa
na mamlaka katika kutoa huduma za hali ya hewa Zanzibar. Aliielezea menejiment
ya TMA kuwa, huduma za hali ya hewa nchini zinazidi kuimarika hususan kwenye
usahihi wa taarifa zinazotolewa kama vile utabiri wa kila siku na tahadhari,
hivyo kuongeza imani kwa wananchi katika ufuatiliaji wa taarifa za hali ya hewa
ukilinganisha na hapo awali ambapo jamii
ilikuwa na hulka ya kupuuzia taarifa hizo.
Mhe.
Juma alifahamisha mchango wa TMA unatambuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
(SMZ) akitolea mfano wa pongezi zilizotolewa kwa Mamlaka na Makamu wa Pili wa
Rais Mhe. Balozi Seif Ali Iddi kwenye Baraza la Wawakilishi la Zanzibar
Kwa
upande mwengine, Mwenyekii wa Bodi ya Ushauri ya TMA Dkt. Buruhani Nyenzi
aliwashukuru wajumbe hao kwa pongezi zilizotolewa na kuahidi kuisaidia Mamlaka
kufikia malengo ya juu zaidi katika utoaji huduma kwa kuboresha miundo mbinu.
Aidha aliwaeleza wajumbe hivi karibuni alikuwa na ziara ya kutembelea vituo vya
hali ya hewa vya unguja na pemba ili kujionea hali halisi, hivyo wananchi
wategemee huduma bora zaidi kwa kuwa lengo la Mamlaka ni kuongeza na
kuviboresha vituo vyake na kuongeza usahihi wa takwimu za hali ya hewa
zinazokusanywa.
Nae
Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dkt. Agnes Kijazi aliwashukuru wajumbe na kueleza
utendaji kazi wa Mamlaka kwa kuzingatia weledi na ushirikiano uliopo baina ya
wafanyakazi wenyewe na wadau wa hali ya hewa, Aidha, Dkt. Kijazi alijivunia
uwepo wa wataalam wa sayansi ya hali ya hewa wenye sifa za kitaifa na kimataifa
ambao mchango wao mkubwa umeonekana katika kuongeza usahihi wa taarifa
zitolewazo.
IMETOLEWA NA: MONICA MUTONI, AFISA
HABARI, MAMLAKA YA HALI YA HEWA TANZANIA.
No comments:
Post a Comment