Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Azungumza na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje Tanzania Dkt. Suzan.Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akizungumza na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wac Afrika Mashariki Dkt. Suzan Alphonce Kolimba, alipofika Ofisi ya Makamu Jijini Dar es Salaam Magogoni

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ameiagiza Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kutatua changamoto zilizopo nchini ambazo huwasababisha mahujaji wa Tanzania kushindwa kushiriki na kutekeleza ibada ya Hija kikamilifu.

Balozi Seif ameyasema hayo katika ofisi yake iliyopo Dar es salaam mtaa wa Magogoni baada ya kutembelewa na Naibu waziri wa Mambo ya nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mheshimiwa Dkt. Susan Kolimba.

Mheshimiwa Balozi Seif ameagiza  wizara hiyo na kusisitiza ufuatiliaji wa karibu wa taratibu zote zinazopaswa kufuatwa kwa ajili ya  matayarisho na maandalizi ya Ibada Hijja kwa waumini wa dini ya Kiislamu. Ameyasema hayo kwa kujua kuwa Wizara hiyo ndiyo yenye mamlaka kamili ya kufuatilia na kushughulikia utaratibu kwa watu wote wanaoenda nje ya nchi.

 Hivyo wizara haina budi kulifuatilia suala hilo na kutatua changamoto zilizopo ambazo zimekuwa ni kero kwa waumini wa dini ya Kiislamu kila ifikapo kipindi cha kushiriki na kuitekeleza ibada hiyo, ambayo ni nguzo ya tano kwa waislamu na ni faradhi kutekelezwa kwa kila mwenye uwezo.

Balozi Seif amesema  kumejitokeza ishara mbali mbali kwa waandaaji wa safari hizo ambazo zinaashiria dalili za kitapeli jambo ambalo husababisha hasara kwa mahujaji au kushindwa kutimiza azma zao.

Aidha Balozi Seif amesema imekuwa ni kawaida sasa kwa viongozi wa vikundi mbali mbali wanaondaa safari hizo kuwa na malumbano na misuguano ya mara kwa mara kila ifikapo kipindi cha kutekeleza ibada hiyo hasa wanapofika nchini Saudia Arabia jambo ambalo linaitia fedheha nchi yetu.

Naye Naibu waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Africa Mashariki Dkt. Susan Kolimba amethibtisha kwamba changamoto zilizopo ni za muda mrefu na zimekua zikijirudia kila ifikapo wakati wa matayarisho ya kutekeleza Ibada ya Hija kwa waislamu. … Mheshimiwa Susan Kolimba ameahidhi kuitisha kikao haraka iwezekanavyo kwa wadau wote wanaojishughulisha na safari za hija nchini.

Na kutoa ahadi mbele ya Mheshimiwa Makamu wa pilli wa Zanzibar kuzitatua changamoto zilizopo haraka iwezekanavyo kabla ya kuanza taratibu za kujiandikisha kwa ajili ya kutekeleza ibada hiyo.

Amesema imekuwa ni kawaida sasa kwa waandaji wa safari za Hija hasa wa Tanzania Bara kwa kuwa na misuguano ya mara kwa mara kila ifikapo kipindi cha kutekeleza ibada hiyo sambamba na kushindwa kutekeleza taratibu zinazofaa kabla ya kuelekea nchini Saudia Arabia. Changamoto hizo zimekuwa kero kwa waumini wa dini ya kiislamu hususan kwa Mahujaji.

Aidha amesema kupitia kikao hicho Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki inategemea kujifunza kwa waandaji wa Safari hizo kutoka Zanzibar kwani wamebaini kuwa Zanzibar ina ueledi na uelewa mkubwa wa maandalizi hayo ya safari za Hija.

“kuna makundi ambayo hayaelewi jinsi ya kufanya taratibu za hija ndio maana wanapata usumbufu wakati wa safari zao”

Sharifa Barki Juma
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.