Habari za Punde

RC Kaskazini Pemba asisitiza kutumnika kiswahili kwenye mikutano ya taasisi za serikali

Na Salmin Juma, Pemba

MKUU wa Mkoa wa Kaskazini Pemba  Omar Khamis Othman amewasisitiza wakuu wa taasisi za Serikali kutumia lugha ya Kiswahili kwenye mikutano yao ili kuendeleza kuitangaza na kuikuza lugha hiyo .

Amesema   sio jambo la busara kutumia lugha za kigeni kwenye mikutano na makangamano yanayoandaliwa na Taasisi au Idara zao kwani kunashusha hadhi ya lugha ya Kiswahili .

Akizungumza na Ujumbe kutoka Shirika linalohudumia watoto la Umoja wa Mataifa (UNICEF) ukiongozwa na mwakilishi wake nchini Tanzania Ren’e Van Dangen amesema iwapo kutakuwepo na utaratibu wa kutumia lugha ya Kisiwahili itakuwa ni zawadi kwa wageni wanaohudhuria mikutano hiyo .

Amesema jukumu la kukitangaza Kiswahili kimataifa ni kila mmoja , hivyo ni vyema kuhakikisha kinatumika ipasavyo na kuacha kukimbilia kutumia lugha za kigeni .

“Tumieni lugha ya Kiswahili kwenye mikutano yenu hii itasaidia kukieneza kiswahili  kimataifa acheni kutumia lugha za kigeni ”alisisitiza.

Aidha amesema Taifa linapigania kukieneza Kiswahili na kuifanya kuwa lugha inayotumika Duniani , na kuwataka kuliacha jukumu hilo kwa taasisi teule pekee katika kufanikisha suala hilo.

“Najua zipo taasisi zinazo husika na kukieneza Kiswahili , lakini tusiziachieni jukumu hilo pekee bali na sisi tupaswa kushiriki kufanikisha hilo ”alieleza.

Akizungumza baada ya kumalizika kwa kikao hicho Mratibu wa Kitengo cha Lishe cha Wizara ya Afya Pemba Raya Mkoko Hassan amesema kauli ya Mkuu wa Mkoa inapaswa kupewa kipaombele cha kipekee kwani imelenga katika kukikuza Kiswahili.

Amesema imekuwa ni jambo ma kawaida katika mikutano na makangamano kutumiwa lugha kigeni (Kiingereza) na wakati washiriki la  watanzania na hivyo kukwamisha juhudi za kukuitangaza na kukieneza Kiswahili.

Naye Katibu Tawala  Mkoa wa Kaskazini Pemba Ahmed Khalid Abdalla amesema pamoja na umuhimu wa lugha za Kigeni kutumika kimataifa , lakini ni vyema na Kiswahili kukitumia kwenye mikutano hata kama inawashirikisha wageni kutoka nje ya Nchi.

Ameeleza kwamba uwepo wa Raia wa Kigeni kwenye makangamano na mikutano isewe sababu ya kutotumika kwa lugha ya Kiswahili kufikisha ujumbe uliokusudiwa .

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.