Habari za Punde

Utambuzi wa Magonjwa Kuongeza Tija ya Uzalishaji wa Mazao ya Mifugo.

Na Ismail Ngayonga. Maelezo.Dar es Salaam.                                                                    
SEKTA ya Mifugo ina mkubwa katika kujenga uchumi imara wa Taifa, kuongeza kipato kwa Watanzania wanaotegemea mifugo, na kutoa fursa za ajira sanjari na kuhifadhi rasilimali za Taifa.

Kulingana na takwimu na Ofisi ya Taifa ya Takwimu mwaka 2013, sekta ya mifugo ilikua kwa asilimia 3.8 ikilinganishwa na asilimia 3.1 mwaka 2012 na kuchangia asilimia 4.4 katika pato la Taifa ikilinganishwa na asilimia 4.6 mwaka 2012.
Mkutano wa wadau wa tasnia ya mifugo uliofanyika Arusha mwaka 2001, ulibainisha matatizo makuu sita yanayoathiri ufanisi wa Sekta ya Mifugo kuwa ni pamoja na kuenea kwa magonjwa ya mifugo nchini ikiwemo magonjwa ya mlipuko, magonjwa yanayoenezwa na wadudu na magonjwa ya mifugo yanayoambukiza binadamu.
Magonjwa ya milipuko na yasiyokuwa na mipaka ambayo hutokea zaidi nchini ni pamoja na ugonjwa wa miguu na midomo, homa ya mapafu ya ng’ombe, sotoka ya mbuzi na kondoo, homa ya bonde la ufa, mapele ya ngozi na homa ya nguruwe.
Taarifa ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi ya mwaka 2013 inaelezwa kuwa wa  ugonjwa wa  mlipuko wa homa ya bonde la ufa uliotokea mwaka 2007 ulisababisha hasara ya Tsh. Bilioni 12 na kupoteza maisha ya watu 144 na kabla ya kudhibitiwa na Serikali kwa kuagiza chanjo dozi Milioni 5.5 na kuchanja ng’ombe, mbuzi na kondoo.
Licha ya magonjwa hayo kuleta hasara za kiuchumi na kijamii, pia magonjwa hayo yalisababisha maambukizi kwa binadamu, vifo na vizuizi vya biashara ya mifugo na mazao yake ndani na nje ya nchi.
Akiwasilisha Hotuba ya makadirio ya bajeti ya mapato na matumizi kwa mwaka 2017/18, Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi Dkt. Charles Tizeba anasema mwaka katika mwaka  2016/2017 Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) iliendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya utafiti katika kanda za ki-ikolojia nchini.
Anasema upitia miradi hiyo, Serikali ilitekeleza miradi ya Kipaumbele inayohusu utafiti na maendeleo ya uzalishaji wa ng’ombe wa maziwa, uboreshaji na uzalishaji wa malisho, mbuzi, kondoo na kuku katika kupitia vituo vyake saba vilivyopo Mpwapwa (Dodoma), Mabuki (Mwanza), Kongwa (Dodoma), Tanga, Naliendele (Mtwara), Uyole (Mbeya), na West Kilimanjaro.
“Katika mwaka 2016/17 Wizara kupitia Wakala wa Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) imefanya uchunguzi na utambuzi wa magonjwa ya mifugo nchini katika sampuli 4,908 zilizopokelewa” anasema Tizeba.
Anayataja magonjwa yaliyotambuliwa ni pamoja na ndigana kali, ndigana baridi, kimeta, kichaa cha mbwa, Mdondo, gumboro, sotoka ya mbuzi, homa ya nguruwe, minyoo, ugonjwa wa kutupa mimba na blue tongue.
Aidha Dkt. Tizeba anasema jumla ya sampuli 1,111 za vyakula vya mifugo zilifanyiwa uhakiki wa ubora na usalama wake ambapo asilimia 18 ya sampuli hizo zilibainika kuwa na   upungufu wa protini na nishati.
Aidha Waziri Tizeba anasema TVLA kupitia Taasisi yake ya utafiti na uzalishaji wa chanjo iliyopo Kibaha imezalisha na kusambaza chanjo dozi  30,055,100 za ugonjwa wa mdondo, dozi  680,900 za  ugonjwa wa Kimeta, dozi 121,550 za  ugonjwa wa Chambavu na dozi 10,000 za chanjo ya ugonjwa wa Kutupa Mimba.
Waziri Tizeba anasema TVLA ipo katika mpango wa kuzalisha chanjo za homa ya mapafu ya ng’ombe (CBPP) na chanjo ya sotoka ya mbuzi na kondoo (PPR) ili kutimiza lengo mafunzo yametolewa kwa mtalaam mmoja huko PANVAC nchini Ethiopia na pia imeshapokea mbegu ya chanjo hizo kama mchakato wa awali wa uzalishaji wa chanjo hizo.
Kwa mujibu wa Dkt Tizeba anasema TVLA kupitia vituo vyake vya utafiti wa teknolojia za kuangamiza mbun’go waenezao ugonjwa wa Nagana na Malale vya Tanga na Kigoma imeendelea kufanya utafiti wa njia nzuri za kupunguza au kumaliza mbung’o katika maeneo mbalimbali nchini.
“Utafiti huo pia umejikita katika kuangalia mwenedo wa mbung’o na ndorobo kati ya wanyama pori na wafugwao na uwezo wao wa kuambukiza wanyama na binadamu, ambapo hata hivyo ndorobo wote waliopatikana ni wale wasioambukiza binadamu. Ili kuendeleza tafiti za kudhibiti mbung’o, maabara imeendelea kuzalisha na kuhifadhi mbung’o wazima 506 na mabuu 556” anasema Waziri Tizeba.
Anasema Serikali itaendelea na tafiti za kudhibiti magonjwa mengine ya mifugo na kujenga uwezo wa kuyatambua na na kufuatilia mwenendo wa ugonjwa wa Sotoka ya Mbuzi katika wilaya za Handeni, Mbarali, Masasi, Ruangwa, Kiteto, Simanjiro na Ngorongoro ambapo uwepo wa ugonjwa wa Blue Tongue uligunduliwa.
Aidha Tizeba anasema katika mwaka 2017/18 TVLA itaendelea na uzalishaji na usambazaji wa chanjo dozi milioni 100 za Mdondo, 500,000 za Kimeta, 500,000 za Chambavu na 500,000 za ugonjwa wa Kutupa Mimba.
Serikali ya Awamu ya Tano inaingia katika mwaka wa pili wa utekelezaji wa Mpango wa Pili wa Maendeleo wa miaka mitano wa mwaka 2016-21 unaojitika katika uchumi wa viwanda wenye lengo la kuifikisha Tanzania katika uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.
Ili kufikia malengo hayo ni wajibu wa sekta binafsi kuunga mkono Serikali katika kuinua sekta mbalimbali za kiuchumi ikiwemo bidhaa za mazao ya mifugo ikiwemo nyama, ngozi na maziwa. 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.