Habari za Punde

Wasomi waagizwa kushirikiana na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya amali kuzifanyia tathmini za kitaalamu skuli walizosoma

Makamo wa pili wa rais Balozi Seif Ali Iddi akiweka jiwe la msingi la ukumbi wa kufanyia mitihani ikiwa ni kumbukumbu ya Skuli ya Nungwi kutimiza miaka 50 tangu kuanzishwa kwake. Makamo wa Pili alikuwa mwalimu Mkuu wa kwanza kusomesha skuli hiyo
Kikundi cha Sarakasi cha vijana wa Nungwi kikitoa burudani kwa mgeni rasmi na wageni waalikwa

Wanafunzi wa Skuli ya Nungwi wakifuatilia hafla hiyo ya uzinduzi wa chumba cha kufanyia mitihani kichofunguliwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ikiwa pamoja na kuadhimisha kusherehekea miaka 50 ya skuli yao tangu kuanzishwa

Na. Mwandishi OMPR.
Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amewaagiza wasomi nchini kwa kushirikiana na wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kuzifanyia tathmini za kitaalamu mara kwa mara skuli walizosoma kwa lengo la kuzisaidia kupata maendeleo endelevu ya elimu.

Balozi Seif ameyasema hayo wakati akiwahutubia wananchi wa Nungwi wakati wa kuadhimisha miaka 50 tangu kuanzishwa kwa Skuli ya Nungwi ambayo aliwahi kuwa mwalimu Mkuu wa kwanza.

Makamo wa Pili amesema tathmini ni nyenzo muhimu ya kielimu itakayozisaidia Skuli na wataalamu wa Elimu nchini  kurekebisha mapungufu yaliyopo kwenye Skuli hizo kwa wakati pamoja na kujipangia mikakati mipya ya kurekebisha mapungufu hayo. 

Amesema  utoaji wa elimu na tathmini ni vitu vinavyokwenda sambamba na kwa kuanzia amewagiza wasomi wa Nungwi kumpatia tathmini ya kitaalamu ya Skuli yao ndani ya wiki tatu.

Akizungumzia elimu kwa jumla katika kijiji cha Nungwi balozi Seif amewahimiza wanafunzi wa Skuli hiyo kupania katika masomo yao ili kuendelea na masomo ya juu.

Amesema Nungwi imebarikiwa na mazingira mazuri yanayowavutia wageni kuwekeza katika sekta ya utalii  jambo ambalo linatoa fursa nyingi za ajira kwa vijana. Hata hivyo Balozi Seif amesema fursa hizo hazitopatikana kwa wanaNungwi ikiwa hawatajibiidisha katika masomo yao. 

Amesema fahari ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ni kuona hoteli zote za Nungwi zinaendeshwa na vijana wa Nungwi, kwa hivyo amewataka vijana hao kujiunga na vyuo vya utalii nchini kwa wingi kwa mafunzo ya shahada ya utalii.

Wakati wa sherehe hizo za miaka 50 ya kuanzishwa Skuli ya Nungwi Makamo wa pili wa rais Balozi Seif Ali Iddi alipata nafasi kuweka  jiwe la msingi la ukumbi wa kufanyia mitihani mradi ambao unaendeshwa kwa nguvu za wananchi na wafadhili mbali mbali chini ya usimamizi wa Taasisi ya Maendeleo ya Elimu ya Kijiji cha Nungwi (TAMEN)

Akimkaribisha Makamo wa Pili wa Rais, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Mhe. Riziki Pembe Juma amewataka wananchi wa Nungwi kushikiana kwa hali na mali katika miradi mbali mbali ya skuli ikiwemo ujenzi wa ukumbi wa kufanyia mitihani, ujenzi wa mabanda ya madarasa na ujenzi wa ukuta ambao utakuwa ni uzio wa eneo linalozunguka skuli.

Amesema maendeleo ya elimu hayawezi kupatikana bila ya mashirikiano ya wanajamii na kuwasihi wanaNungwi kushikamana katika kuwasomesha vijana wao.

Aidha Waziri huyo wa Elimu amezitaka skuli zote nchini kuimba wimbo wa sisi sote wakati wa paredi  kama ilivyokuwa zamani na kusisitiza kuwa skuli itakayoshindwa kutii amri hiyo itachukuliwa hatua.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.