Habari za Punde

Alietorosha msichana asakwa, mnajisi mnyama ahojiwa Polisi

 NA HAJI NASSOR, PEMBA

JESHI la Polisi mkoa wa kusini Pemba, linamtafuta kijana Mohamed Nassor (25) mkaazi wa Changaweni wilaya ya Mkoani, akituhumiwa kumtorosha msichana (16), aliechini ya uangalizi wa wazazi wake.

Kamanda wa Polisi Mkoani humo, Shehan Mohamed Shehan, alisema kijana huyo, alitoroka baada ya kushitukia kuwa anafautwa na Polisi, baada ya kufanya kosa hilo.

Alisema kijana huyo alikwenda kijiji cha Makombeni Oktoba 23, na alipofika, alimtorosha msichana huyo na kumpeleka Changaweni kwa lengo la kumingilia.

Alisema baada ya mtoto huyo kuhojiwa, ndipo taarifa zilipowafikia na kuanza kumtafuta, ingawa taarifa za awali zilionyesha amekimbia.

“Jeshi ka Polisi linamtafuta kila kona, na limeshaweka mitego, ili kuhakikisha anapatikana na kufika mbele ya mkono wa sheria kujieleza”,alisema.

Hata hivyo amewataka wazazi na walezi, kuwa karibu na watoto wao, na kila baada ya muda kujua walipo, ili kuweza kutatua changamoto kama hizo zinapowatokea.

Wakati huo huo Jeshi hilo la Polisi Mkoani humo, linaendelea kumuhoji kijana Juma Abdalla Salum (29), mkaazi wa mjini Chakechake, kwa tuhuma za kumuingilia Ng’ombe jike.

Alisema kijana huyo alietenda kosa hilo Oktoba 23, majira ya saa 12:30 jioni eneo la Ngoma hazingwa nje kidogo ya mjini wa Chakechake,ambapo  alionekana na watu na kisha kufikishwa Polisi.

Kamanda Shehan alisema, baada ya kufikishwa Jeshi la Polisi linaendele kumuhoji na ikiwa ataonekana anahusika na tukio hilo, jalada lake litafikishwa kwa DPP kwa ajili ya uchunguzi na kisha kupanda mahakamani.

“Tukimaliza taratibu za kumuhoji, linalofuata ni kufikishwa mahakamani kwa ajili ya kujibu tuhuma zinazomkabili za kumuharibu mnyama”,alifafanua.

Hili ni tukio la pili kwa mwaka huu wa 2017, la kumuingilia mnyama, ambapo tukio la kwanza lililtokea miezi minne iliopita, shehia ya Vitongoji wilaya ya Chakechake.

                         

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.