Habari za Punde

China Yakabidhi Msaada wa Vifaa Tiba na Dawa Zanzibar

Waziri wa Afya Zanzibar Mhe. Mahmoud Thabit Kombo akitiliana saini makubaliano ya makabidhiano ya Madawa na Vifaa Tiba kutoka China na Balozi wa Jamuhuri ya Watu wa China Xie Xiaowu, hafla hiyo imefanyika katika Bohari Kuu la Madawa Maruhubi Zanzibar. 
Balozi wa Jamuhuri ya Watu wa China  Xie Xiaowu akibadilisha Hati za makabidhiano Vifaa Tiba na Madawa na Waziri wa Afya Zanzibar Mhe. Mahmoud Thabit Kombo, hafla hiyo ya makabidhiano imefanyika katika viwanja vya Bohari Kuu la Madawa Maruhubi Zanzibar. 
Balozi wa Jamuhuri ya Watu wa China Balozi Xie Xiaowu akizungumza baada ya kutiliana saini ya makabidhiano ya Vifaa Tiba na Madawa, kwa ajili ya Matumizi ya Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja hafla hiyo imefanyika katika viwanja vya Bohari Kuu Maruhubi Zanzibar, kulia Waziri wa Afya Zanzibar Mhe. Mohmoud Thaibi Kombo.
Waziri wa Afya Zanzibar Mhe. Mahmoud Thabit Kombo akitowa shukrani kwa Serikali ya China kwa Msaada wao huo wa Madawa na Vifaa Tiba, hafla hiyo imefanyika katika viwanja vya Bohari Kuu ya Madawa Maruhubi Zanzibar. kulia Balozi wa China Xie Xiaowu na kushoto Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Afya Halima Maulid Salum.
Balozi wa Jamuhuri  ya Watu wa China Xie Xiaowu akimkabidhi dawa na vifaa tiba Waziri wa Afya Mhe,Mahmuod Thabit Kombo huko Bohari Kuu ya dawa Maruhubi Zanzibar.
Baadhi ya Dawa na Vifaa tiba zilizotolewa na Balozi wa Jamuhuri ya Watu wa China Xie Xiaowu zenye thamani shilingi bilioni 1.4 huko Bohari Kuu ya dawa Maruhubi Zanzibar
Picha na   Kijakazi Abdalla Maelezo Zanzibar


Na Ramadhani Ali – Maelezo.17.10.2017
Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China imeikabidhi Serikali  ya Mapinduzi ya Zanzibar msaada wa dawa na vifaa tiba vyenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 1.4 kwa ajili ya kuimarisha afya za wananchi.

Balozi mdogo wa China Zanzibar Xie  Xiaowu alimkabidhi Waziri wa Afya Mahmoud Thabit Kombo msaada huo katika hafla fupi iliyofanyika Bohari kuu ya dawa Maruhubi.

Waziri Mahmopud aliishukuru China kwa misaada inayotoa hasa katika sekta ya afya ikiwemo kuleta madaktari kufanyakazi katika Hospitali kuu ya Mnazimmoja na Hospitali ya Abdalla Mzee ya Mkoani Pemba.

Aliwaomba madaktari wa China wanaoendelea kufanyakazi  Zanzibar kuwapa mafunzo madaktari wazalendo kutumia vifaa tiba vya kisasa vilivyowekwa katika hospitali ya Mkoani na Mnazimmoja ili watakapoondoka waweze kuvitumia.

Waziri wa Afya aliwashauri madaktari hao kuanzisha utaratibu wa kwenda hospitali za vijijini kutoa huduma  ambazo hazipatikani katika vituo hivyo ili kuwapunguzia gharama za kuzifuata Hospitali kuu.

Waziri Mahmoud aliwataka wafanyakazi wa Bohari kuu ya dawa kuzitunza vizuri dawa zinazowekwa bohari na kuhakikisha zinafika kwa wananchi bila ya kutoa malipo.
Balozi Xie ameahidi kuwa Serikali ya China itaendelea kuwasaidia  wananchi wa Zanzibar katika sekta mbali mbali za maendeleo ikiwemo sekta ya afya katika kuimarisha ushirikiano wa wananchi wa nchi hizo.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi wa Bohari kuu ya dawa Zanzibar Zahran Ali Hamad aliahidi kuwa dawa hizo watazisambaza katika hospitali na vituo vya afya Unguja na Pemba na zitatolewa bila malipo.

Baadhi ya dawa zilizokabidhiwa ni kwa ajili ya maradhi ya kawaida, dawa za shindikizo la damu, kisukari, vidonda vya tumbo na vifaa tiba vya kufanyia upasuaji mkubwa. 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.