Hotuba ya Mheshimiwa Makamu wa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, Katika Hafla ya Uzinduzi wa Sera ya Taifa ya Huduma Ndogo za Fedha ya Mwaka 2016,na Mkakati wa Utekelezaji wa Sera Hiyo Tarehe 23 Oktoba, 2017
Dodoma.
Mhe. Dkt. Philip
Isdor Mpango (Mb.), Waziri wa Fedha na Mipango;
Mhe. Suleiman Jafo; Waziri TAMISEMI;
Jabir Shekimweri;
Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma;
Mhe. Hawa Ghasia;
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge Bajeti;
Mhe. Ashatu Kijaji;
Naibu Waziri Fedha na Mipango;
Waheshimiwa
Wabunge na Wajumbe wa Kamati ya Bajeti;
Mhe. Mstahiki Meya
wa Dodoma;
Makatibu Wakuu na
Naibu Katibu Wakuu wa Wizara mliopo;
Mwakilishi wa Gavana
wa Benki Kuu ya Tanzania;
Viongozi mbalimbali
wa Chama na Serikali;
Watendaji Wakuu wa
Taasisi za Huduma za Fedha nchini;
Washirika wa Maendeleo mliopo hapa;
Waandishi wa Habari;
Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana;
Habari za mchana.
Awali
ya yote nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema na Amani kwa
kutujalia uzima na afya njema na hivyo kuniwezesha kujumuika nanyi katika
uzinduzi wa Sera ya Taifa ya Huduma Ndogo za Fedha ya mwaka 2017 na Mkakati wa
Utekelezaji wa Sera hiyo.
Nitumie fursa hii kumshukuru Mheshimiwa
Dkt. Philip Mpango (Mb), Waziri wa Fedha na Mipango na Kamati ya Maandalizi,
kwa kunialika kushiriki kwenye tukio hili muhimu kwa ustawi wa nchi yetu na mustakbali
wa sekta ya fedha nchini.
Vilevile nimpongeze
Dkt. Bilinith Mahenge kwa kuchaguliwa
kuwa Mkuu
wa Mkoa
wa Jiji
la Dodoma.
Asante kwa mapokezi mazuri na
nikutakie heri na mafanikio katika majukumu yako mapya na ninaamini utamudu
vyema majukumu haya.
Pia nichukue fursa hii kuwatakia kila
la heri wanafunzi wetu wa kidato cha nne wanaoanza mitihani yao leo. Ni imani
yangu mmetayarishwa na mmejitayarisha vya kutosha. Hivyo niseme kila heri and
all the best our dear students.
Sasa niruhusuni niendelee na hotuba
yangu kwa kuipongeza Wizara ya Fedha kwa kutoa kipaumbele na msukumo mkubwa
katika kufanyia mapitio na kuandaa sera hii. Niwasihi muendelee hivyo kwa
sababu bado tunalo jukumu la kuhakikisha tunaandaa sera nyingi zaidi kwa
masilahi mapana ya Taifa letu.
Kwa namna ya pekee, niwashukuru
Wahisani wetu wa Maendeleo walioshirikiana na Serikali katika kusaidia
ukamilishaji wa Sera hii. Kwa niaba ya Serikali ninawaahidi kwamba Sera hii
itatumika ipasavyo na kuwanufaisha zaidi walengwa wa Sera hii ambao ni wananchi
wa kipato cha chini.
Wageni
Waalikwa;
Mabibi
na Mabwana;
Siku ya leo ni siku muhimu sana kwa
Sekta ya Fedha Nchini. Hii ni kutokana na dhamira ya Serikali ya kuinua uchumi
wa wananchi wa kipato cha chini. Uzinduzi wa Sera hii ni mwendelezo wa
utekelezaji wa Ilani ya CCM inayosisitiza kupambana na umaskini hasa kwa
kuwekea mkazo kwenye urasimishaji wa biashara na kuwapatia wafanyabiashara
wadogo maeneo rasmi ya kufanyia biashara
ikiwa ni pamoja na kuwapatia mikopo yenye masharti nafuu. (kifungu 6 (d) cha flani).
Hivyo, tukio hili ni kudhihirisha
utayari wa Serikali kuweka mazingira wezeshi kwa wajasiriamali wadogo na
wananchi wenye mahitaji maalum ili kujiwezesha kiuchumi. Hivyo, tunayo kila
sababu ya kujivunia hatua hii, na nitumie fursa hii kuwasihi wadau wote wa
sekta ya fedha nchini, kuendelea kutuunga mkono ili tuweze kupeleka mbele
maendeleo ya nchi yetu.
Wageni
Waalikwa, Mabibi na Mabwana;
Kama alivyobainisha Mhe. Waziri wa Fedha na Mipango kuwa Serikali iliamua kufanya mapitio ya Sera ya
Taifa ya Huduma Ndogo za Fedha ya Mwaka 2000 kwa kutunga Sera ya Taifa ya
Huduma Ndogo za Fedha ya Mwaka 2017 na Mkakati wa Utekelezaji wa Sera hiyo kwa
kipindi cha miaka 10 ili kutatua upungufu na changamoto zilizojitokeza katika
sekta ndogo ya fedha. Changamoto hizo ni pamoja na:
i. Ongezeko la idadi ya watoa huduma ndogo za fedha
ikiwa
ni pamoja na Benki na Taasisi
za
Fedha,
Programu na
Mifuko ya Serikali, Vikundi vya Fedha vya Kijamii kama vile Village Community Banks -VICOBA na Vyama vya Akiba na Mikopo
Vijijini (VSLA), Kampuni za Simu, Asasi za Kijamii na Wakopeshaji binafsi;
ii. Ukosefu
wa mfumo wa sheria na kanuni wa kusimamia taasisi zisizochukua amana na vikundi
vya fedha vya kijamii;
iii. Uelewa
mdogo wa masuala ya fedha;
iv. Ukosefu
wa takwimu katika sekta ndogo ya fedha;
v. Kukosekana
kwa mfumo wa kumlinda mtumiaji wa huduma ndogo za fedha;
vi. Kutokuwepo
na uwazi katika vigezo na masharti ya
utoaji mikopo; na
vii. Viwango
vya juu vya riba.
Pamoja na changamoto hizo,
tafiti zilizofanywa kwengineko Duniani zimeonesha kwamba wakopaji maskini
wamekuwa wakiishi na mikopo baada ya mikopo bila kuweza kujiwekea akiba na
kukuza biashara zao.
Imeonekana kwamba mikopo
imewezesha angalau watu maskini kuweza kuweka akiba ya kuwasaidia wanapokubwa
na shida za familia zao.
Imebaini
pia kwamba katika maeneo kadhaa ya duniani mikopo nafuu haikuweza kutimiza
malengo yaliyowekwa na mkutano wa Umoja wa Mataifa uliozungumzia masuala ya
kuwezesha watu maskini kwa kutumia mikopo nafuu wa 1997.
Umoja
wa Mataifa uliweka malengo manne makubwa ikiwemo, mikopo iwafikie maskini wa
maskini (mafukara); Kuongeza kipato cha maskini kwa kuwawezesha kujiajiri,
Taasisi za Fedha ziweze kujijengea akiba kubwa ya kutosha kuendelea kukopeshana
na kufanikiwa na kuwawezesha wanawake hasa wa Vijijini. Vile vile, kuna maneno yaliyotumika bila kuwa
na tafsiri ya kueleweka na kila mtu, kwa mfano, "umaskini wa maskini"
- vipimo vyake ni vipi? "Uwezeshaji
wa Wanawake" - sio kiuchumi tu,
masuala ya mila Potofu,
Ujuzi wa Biashara,
Elimu
ya Afya na Afya ya uzazi, kujua kusoma na kuandika n.k. Taasisi za mikopo za faida na zisizo na faida
- mipaka yao ni ipi? Mambo haya
tunapaswa nasi tuyaangalie kwa makini katika Sera zetu.
Wageni
Waalikwa, Mabibi na Mabwana;
Kwa kutambua
umuhimu wa Sekta Ndogo ya Fedha katika
kupunguza Umaskini na Kukuza Uchumi, napenda kuchukua fursa hii kuwaomba wadau
mbalimbali kutoa ushirikiano kwa Serikali ili kufanikisha utekelezaji wa Sera
ya Taifa ya Huduma Ndogo za Fedha ya Mwaka 2017. Ili kutekeleza azma hii, ni
matumaini yangu kuwa Wizara ya Fedha na Mipango itaendelea kuratibu, kusimamia na
kutathmini maendeleo ya sekta ya fedha ikijumuisha sekta ndogo ya fedha kwa
kutenga fedha za kutosha kwa ajili ya utekelezaji wa Sera hii.
Kwa kuwa walengwa wengi wa Sera hii ni
wananchi wa kipato cha chini na wanafanya kazi katika maeneo na mifumo isiyo
rasmi, hivyo basi ni muhimu kutoa elimu ya fedha na ujasiriamali. Kwa
kulitambua hili, ningependa kuona
Mamlaka za Serikali za Mitaa zikiteleza yafuatayo:
i.
Halmashauri kutenga
asilimia 10 ya mapato yao kama inavyotakiwa vikundi vya kina mama (asilimia 5)
na vijana (asilimia 5) na kuhakikisha kuwa fedha hizi zinatumika ipasavyo na
kuwanufaisha wote;
ii.
Zinatenga maeneo na kuweka
mifumo rasmi itakayowawezesha wajasiriamali wadogo, vijana, wanawake na makundi
maalum ili waweze kujiajiri;
iii.
Zinahamasisha wananchi kuunda vikundi vya
fedha vya kijamii na SACCOS pamoja na kuhakikisha kuwa wanasajili vikundi hivi
rasmi; kufuatilia shughuli zao na kuhakikisha wanaweka fedha hizi kwenye mifumo
rasmi ya kibenki;
iv.
Zinajumuisha
masuala ya huduma ndogo za fedha kwenye mipango yao ya maendeleo; na
v.
Zinaratibu na kuandaa taarifa ya upatikanaji wa huduma
za fedha kuanzia ngazi za kata hadi Mkoa.
vi.
Kufanya tahthmini kila
baada ya muda ili kubaini maendeleo ya Changamoto za utekelezaji wa Sera hii.
Wageni
Waalikwa, Mabibi na Mabwana;
Ili kufanikisha lengo la Sera hii ambalo ni kuimarisha huduma jumuishi za fedha kwa
kujenga mazingira wezeshi yatakayoleta ufanisi wa utoaji wa huduma ndogo za
fedha nchini kwa wananchi wenye kipato cha chini na, ili kutekeleza azma hiyo,
nawasihi watoa huduma za fedha nchini kuangalia namna bora ya kupunguza riba za
mikopo na tozo mbalimbali zinazotozwa kwenye upatikanaji wa huduma za fedha.
Aidha, ninawaomba muongeze ubunifu
katika kutoa huduma zinazohitajika na wananchi wa kipato cha chini pamoja na
kupeleka huduma hizo katika maeneo
yaliyo karibu na makazi yao au biashara zao. Vilevile nazitaka taasisi
za huduma za fedha kuwaelimisha wananchi kabla ya kutoa huduma hizo ili
kupunguza athari wanazozipata wananchi.
Ni matarajio yangu kuwa,
Wizara ya Fedha na Mipango itashirikiana na wadau katika kutekeleza Sera
hii na kuhakikisha malengo ya Sera
ambayo ni kukuza uchumi na kupunguza
umaskini yanafikiwa. Nimefurahi kuwaona wadau wa FSDT wakitoa mada kwa kuwa ni
hivi karibuni tu walizindua Finscope Report ya mwaka 2017 ambayo ilionesha kuwa
tumepiga hatua kwenye suala zima la huduma jumuishi za fedha (financial
inclusion) na kufikia asilimia 72 kwa 2017,
na changamoto kuu waliyoianisha ni elimu/uelewa mdogo wa huduma za fedha. Hivyo basi nitoe rai kwa wadau wengine wa Serikali kuweza kusaidiana nasi katika kuhakikisha kuwa changamoto hii na zingine zilizobainishwa kwenye ripoti hii ya Finscope zinafanyiwa kazi ili kuboresha sekta ya fedha nchini iweze kuwa na maendeleo endelevu kiuchumi.
na changamoto kuu waliyoianisha ni elimu/uelewa mdogo wa huduma za fedha. Hivyo basi nitoe rai kwa wadau wengine wa Serikali kuweza kusaidiana nasi katika kuhakikisha kuwa changamoto hii na zingine zilizobainishwa kwenye ripoti hii ya Finscope zinafanyiwa kazi ili kuboresha sekta ya fedha nchini iweze kuwa na maendeleo endelevu kiuchumi.
Suala la utoaji elimu kwa
wananchi kuhusu usimamizi bora wa fedha llitakuwa endelevu na Serikali itazidi
kuboresha maslahi ya wataalamu wetu na
kufanya mapitio ya mara kwa mara kwenye sera zetu za fedha. Vilevile tutaweka
mazingira wezeshi kwa vikundi mbalimbali vya kijamii vya kuweka na kukopa ili
viweze kuinua kipato cha wafanyabiashara na wajasiriamali wadogo.
Hata hivyo, juhudi zetu hizo hazitakuwa
na maana endapo hakutokuwa na nidhamu ya matumizi ya fedha. Hivyo, natoa wito
kwa watumishi wa umma, wadau wa sekta ya fedha na jamii kwa ujumla kusimamia
kwa ukamilifu matumizi sahihi ya fedha za umma, ili tujenge Taifa la wananchi
wenye uchungu na rasilimali zetu na uzalendo kwa nchi yao.
Wageni
Waalikwa,
Mabibi
na Mabwana;
Nilipata fursa kidogo ya kupitia Sera
hii na nimefurahi kuona kuwa Sera hii imewapa kipaumbele makundi yenye uhitaji
maalum kama wanawake na vijana kwa kuhakikisha kuwa itahamasisha matumizi ya
teknolojia na ubunifu kwenye huduma za fedha zinazokidhi makundi haya; itatoa
elimu kwa makundi haya, pamoja na kuhakikisha kuwa itahamasisha ujumuishwaji wa watoa huduma
ndogo za fedha wasio rasmi kwenye mfumo ulio rasmi kwa kuunganisha vikundi vya
fedha vya makundi haya na Taasisi za Fedha
kama vile Benki;
Mifuko ya Jamii, Masoko ya Hisa na Mitaji na Bima.
Huduma hizi mara nyingi zimekuwa
zikiwaacha watu ambao hawapo kwenye mfumo rasmi wa ajira na hivyo kuachwa nyuma kimaendeleo. Kwa
kuweka huduma hizi itahakikisha hamna mwananchi atakayeachwa nyuma kwenye
maendeleo.
Jambo jingine lililonifurahisha kwenye Sera
hii ni kuhusu Huduma za kibenki kwa mitandao (Mobile Banking) ambayo naamini ni
huduma muhimu kwetu sote na hamna hata mmoja wetu hapa ambae hajaitumia wala
hajanufaika na huduma hii. Naamini wengi siku hizi hatuwapi tena watu fedha
mkononi wawapelekee ndugu na jamaa zetu waliopo vijijini bali tunatumia huduma
hii kutuma fedha hizo. Nimefarijika kuona kuwa kwenye tamko la Sera katika
Mobile Banking imezungumzia kuboresha kanuni za usimamizi wa sekta ndogo hii
ya fedha; kuwalinda watumiaji wa huduma
hii pamoja na kuboresha miundombinu ya ubadilishanaji taarifa kati ya
wasimamizi wa sekta hii ndogo ya fedha. Maana wote tunajua kuwa sekta hii
isipokuwa na usimamizi basi wengine hutumia mianya iliyopo kufanya yao.
Nihitimishe kwa kurudia tena kuwa Uzinduzi
wa Sera hii Mpya na yale yaliyomo katika sera hii ni ushahidi tosha wa dhamira
ya Serikali na ya wenzetu wote
tulioshirikiana nao katika kutayarisha sera hii kuona huduma za kifedha nchini
zinazidi kuimarika na kuwa bora zaidi. Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango,
najua wewe ni Bwana wa Mipango kama jina lako hivyo ni matumaini yangu kuwa
wewe pamoja na wadau wengine mtahakikisha kuwa sheria ya sekta ndogo ya fedha
inakamilika mapema iwezekanavyo. Hivyo
niwaambie kuwa tufanye ya wakati; wakati tuna wakati; utakuja wakati tukitaka
kufanya ya wakati, wakati hatuna wakati! Basi wakati ni huu wa kutekeleza haya
yote tuliyoyapanga.
Baada ya kusema haya machache, nirudie
kwa kuwashukuru kwa kazi kubwa ya kuandaa sera hii. Na sasa napenda kutamka kuwa Sera ya Taifa ya Huduma Ndogo za Fedha ya
Mwaka 2017 pamoja na Mkakati wa Utekelezaji wa Sera hiyo imezinduliwa rasmi.
ASANTENI
SANA.
No comments:
Post a Comment