Habari za Punde

Madereva wengi wanaathirika kiafya

ALIEKUWA dereva wa gari ya wizara ya Afya kisiwani Pemba Suleiman Mohamed Suleiman (74), akizungumza na mwandishi wa habari wa makala wa Shirika la Magazeti ya Serikali Pemba, Haji Nassor Mohamed (kulia), juu ya hali ya afya yake baada ya kustaafu, (Picha na Habiba Zarali, Pemba) 

-Msongo wa mawazo, bawasili, kuchanika mifupa ni rundo la mgonjwa yanayowapata madereva

-Wa serikali watajwa kunyemelewa zaidi hasa wakinyimwa likizo

NA HAJI NASSOR, PEMBA
“KAMA dereva hawezi kufanya mazoezi, basi walau inapolala gari na yeye, pawe na masafa wa kuifuata walau dakika 30” ndio kauli ya mtaalamu wa magonjwa ya mifupa dk Rahila wa hospitali ya Chakechake Pemba.

Anasema, kinga kubwa ya magonjwa hayo, moja wapo kwa maderava hasa wa serikali, ni kufanuya mazoezi, lakini kama wanashindwa wanatakiwa kila siku, waifuate gari kutoka anapolala kwa dakika 15 hadi 30.
Sio sahihi dereva anapoishi, na nje ndio pana gari tena ya ofisi, dereva wa aina hii, ndie wa kwanza kukumbwa na magonjwa kati ya yale nane yanayoweza kuwapata.

Tena ogopa zaidi dereva hasa wa gari ya serikali, kisha anatumia vinywaji kama pombe, na kahawa kwa wingi au sigara, na kisha gari ya ofisini anaifanya kama ibada haishuki.

“Wapo madereva kwanza niwatumiaji wa pombe, kahawa kwa wingi, au wanavuta sigara, na gari ya ofisini anauhuru nayo wakati wowote, na kuwaona wenzake mabwege kwa kuny’ang’anywa gari baada ya saa za kazi, ajue kuwa magonjwa yanamnyelea’’,anasema dk Rahila.

Magonjwa matatu (3) ndio pekee ambayo yanaweza kumpata dereva hasa wa gari za serikali kwa kule, kukaa kwao sana kwenye usukani, moja ni msongo wa mawazo (stress).

Mtaalamu huyu, anasema msongo huu wa mawazo kwa madereva hasa wa serikali, husababishwa na mambo kadhaa, ikiwa ni pamoja na uchakavu wa gari, kukoseshwa likizo na hata kutopewa fedha za baada ya saa kazi ‘overtime’

“Dereva anamiaka zaidi ya mitano au zaidi yeye yuko kwenye usukani bila ya kupewa likizo, huku gari mbovu, hana fedha za ziada za muda wa saa baada ya kazi, kisha anamuendesha kiongozi hapa lazima ‘stress’imuandame”,anasema.

Lakini maradhi mengine ambayo yanaweza kuwapata madereva wote wakiwemo wa serikali, ni mifupa yake kuchanika bila ya kupata ajali, ambapo hili hujitokeza baada ya zaidi ya miaka mitano, ingawa inategemeana na afya ya dereva mwenyewe.

Imezoeleka kuwa, mtu hawezi kuvunjika mfupa mpaka apate ajali, ingawa kwa madereva wanaoendesha gari kwa muda mrefu bila ya kupumzika, ndio ambao hukumbwa na hali hii.

“Unajua madereva wa serikali kuanzia siku ya kwanza wanaoajiriwa hadi siku anastaafu, ofisi yake ni ndani ya gari, ambapo humu hapati kulala (wima), yaani mifupa na viungo havikunjuki, hivyo uwezekano wa kuvunjika na kuchanika upo”,anafafanua.

Njia ya uvujikaji wa mifupa ya mikono ni kule kuizungurusha mifupa ya mikono yake wakati anapoipindisha sukani ya gari au kakanyaga klachi, au hata kitufe cha breki.

“Wapo wamekaa kama magolkipa wa muda mrefu, maana kama waliopinda kwenye sehemu ya kuanzia nyongani hadi mikononi, kwa kule kuilalia sukani muda mrefu bila ya mapunziko”,anaeleza.

Dereva wa aliekuwa wizara ya Afya Pemba, Suleiman Mohamed Suleiman (74), mkaazi wa mjini Chakechake, anasema baada ya kustaafu, anajihisi maumivu makali, kwenye maoteo ya miguu miwili.

Anajihisi maumivu ambayo kwa sasa hayamruhusu kusimama wima, wakati anapotembea, akiamini kuwa kitako alichokaa tokea mwaka 1977, akiwa dereva wa wizara hiyo, hadi alipostaafu mwaka 2012 ndio sababu.

“Mimi nimeendesha gari kwa miaka 35 mfululizo bila ya likizo, hivyo ilifika wakati naendesha gari nikiwa na machofu, maana nilipoomba likizo, niliambiwa wafanyakazi ni haba sektaya udereva, hivyo nivumilie”,anasema.

Mzee Suleiman, ambae kwa sasa ni mkulima na akiwa na biashara ya vinywaji karibu na maegesho ya gari ya Gombani ndani ya mji wa Chakechake, anasema wala hakumbuki siku aliopewa fedha za baada ya saa kazi “over time” ingawa anasema hakuna siku aliorudi kwake mapema.

Kitaalamu kila dereva anapokuwa barabarani huwa anachunga gari nne moja ni ile ilio kuliani kwake, kushoto, mbele na nyuma, hukuwa pia akiwa na tahadhari kwa aliowabeba ili gari isiingie shimoni.

Ambapo hayo yote, kama nae hakuangaliziwa haki zake uwezekano wa kutokezea ajali au kuchoka mapema kwenye kazi yake hiyo huweza kujitokeza wakati wowote.

“Siku moja siisahu mwaka 1999 ilikuwa jioni, nilipata ajali nikiwa nimebeba madaktari, baada ya mpira wa mbele kupasuka “tairi”, tena kama jana nilishatoa taarifa ofisini, lakini unajua tena, mpaka litokee”,alinikumbusha mzee Suleiman.

Dk Rahila anasema uongonjwa mwengine ambao unaweza kumpata dereva hasa asiepata mapunziko ni bawasili, yaani kutoka mithili ya nyama kwenye sehemu ya haja kubwa, kunakosababishwa na mambo kadhaa ikiwa ni pamoja na kukaa kitako muda mrefu kwenye joto.

“Huu ugonjwa kila mmoja humpata, kwa sababu zake mbali mbali, lakini kwa madereva kule kukaa sana kwenye usukani na chini yao pana mashine inayozalisha joto wasilolihitaji ni sababu”, anabainisha.

Mtaalamu wa mashine za gari kutoka Wizara ya Miundombinu kisiwani Pemba, Mhandisi Khatib Mkubwa Khatib, anasema mashine zote za gari hutakiwa kuwa na joto la wastani wa 78 hadi 85 sentigredi.

Anasema gari isiofanyiwa matengenezo ya kila baada ya muda “service” joto lake aidha houngezeka au kupanda juu zaidi, ambapo kwa hali yoyote hiyo, inaweza kumuathiri dereva kwenye viungo vyake.

“Joto la kawaida analotakia kuwa nalo mwanadamu ni kati ya sentigrade 32 hadi 40, lakini kwa dereva alie na gari mbovu anakumbana na joto mara mbili, hivyo athari mwilini mwake humyemelea”,anafafanua.

Anasema kitaalamu gari hutakiwa kufanyiwa uchunguuzi wa mashine kila baada ya mwezi, ingawa hutegemeana na safari zake, yote hayo ni kumkinga dereva asipate madhara yatokanayo na kazi yake.  

Khamis Sultan Hemed (67) alieajiriwa udereva mwaka 1971 na kuendesha gari kwamiaka 29, anasema hadi anastaafu yeye bado kiafya anajihisi mzima, ingawa changamoto aliokumba nayo ni machofu ya kazi yake, kwakunyimwa likizo.

“Mimi namkumbuka nimeanza kushika usukani kwa miaka 30 mfululizo, na nilipewa likizo mwaka 2000 kwa ajili ya kustaafu, na hilo niliombwa kabla halijamalizika nirudi kazini, na nilirudi”,anasema.

“Mwendo wangu ni wa kusua sua kwa sasa, nahisi baadhi ya viungo havikunjuki hata nikivilamisha, lakini tokea nilipostaafu Kamisheni ya Utalii nimepewa gari ndogo aina ya “carry” na tajiri nadowea mwenye boksi au mzigo niusafirishe eneo jengine”,anasema.

Kumbe Khamis Sultan baada ya kustaafu mwaka huo wa 2000, alikaa mwaka mmoja tu nje, ndipo mwaka 2001 alipopewa kinua mgongo chake kisichozidi shilingi 5,000,000 (milioni tano), ambapo hakuweza kujiendeleza kimaisha.

“Nimemaliza kutumwa na serikali kwa miaka 30, na sasa natumwa na mtu binafsi mpaka niwe sijiwezi tena, kanipa kikeri (gari ndogo inayobeba nusu tani ya mzigo), hichi nazunguruka nacho mjini kutafuta kula”, anasema kwa unyonge.

Kimsingi wataalamu wa afya wanakubaliana kuwa, kila kazi inahitaji mapunziko, ambayo yataambatana na kuangaliwa kwa afya ya mfanyakazi husika, awe dereva au mwengine.

Lakini, kwa dereva wa alieanzia Idara ya Majenzi mwaka 1971 na kuishia Kamisheni ya Utalii mwaka 2000 mzee Khamis Sultan anasema, hakumbuki kwenda likizo hata mara moja, ukiachia lile la  kusataafu ambalo nalo lilikatwa.
Dereva mwengine wa Mkuu wa mkoa wa kaskazini Pemba Ali Massoud Ali (30) alieajiriwa mwaka 2011, anasema hadi sasa afya iko vizuri na wala hajahisi maumivu yoyote yanayosababishwa na kazi yake.

“Mimi niko sawa sana kiafya, ingawa sijaambiwa wapo kama leo niende hospitali kuchunguuzwa afya yangu, maana nakumbuka wakati nataka kuajiiriwa tu, ndio tulitakiwa kufanya hivyo”,anasema.

Tayari ameshapata mapunziko ya likizo kwa mara nne (4), tokea alipoajiriwa, jambo ambalo linampa kuchuma akili mpya ya kazi yake, na hadi sasa hakuna kiashiria chochote cha magonjwa mwilini mwake.

Mohamed Massoud Amran (30) dereva wa Shirika la Utangaazaji Zanzibar ZBC ofisiya Pemba, alieajiriwa mwaka 2000, anasema amekwenda likizo mara tatu pekee, ingawa hakumbuki  kuomba likizo na kukataliwa.

Kwa sasa dereva huyo, anaetimiza miaka 17 kwenye usukani, anasema tayari ameshaanza kupata mabadiliko ya mwili, ikiwa ni pamoja na maumivu makali ya kifua.

“Ingawa kifua sio kila siku, lakini hukaa na kinapokuja huwa na maumivu, naamini yanatokana na vumbi na kuvuta harufu ya mafuta machafu wakati nipoingia mvunguni kutengeneza gari”,anasema.

Lakini dereva huyo wa ZBC kisiwani Pemba, anasema ameshaanza kuona tofauti ya uoni wake, akiamini kuwa macho nayo yameshagonjwa kwa kuvaa miwani asioitarajia, yaani kioo cha gari.

Magonjwa mengine anayoyaona yanamnyelea ni pamoja na maumivu ya nyonga, miguu kuwaka moto bila ya sababu, mikono kuhisi maumivu kwenye mifupa mitihili ya mtu alievunjika.

Kanuni ya Utumushi wa umma ya mwaka 2014 kwenye kifungu chake cha 5 (1) na kwa kuzingatia sheria ya utumishi wa umma ya mwaka huo, kinaeleza wazi kuwa mtu yeyote atakaeingia katika utumishi wa umma, atalazimika kujaza fomu inayoitwa ‘ardhilihali’

Ambapo atafanyiwa uchnguuzi wa afya yake na kuthibitishwa iwapo afya yake, inaruhusu kufanya kazi husika, tena awe lazima ni daktari wa serikali, katika hospitali iliokubalika.

Ingawa moja ya mapungufu yaliomo kwenye kanuni hii na sheria yake, ni kutokuwepo kifungu kinamcholazimisha muajiri, kumfanyia uchunguuzi wa kiafya muajiriwa wake, kila baada ya muda, kama inavyokuwa wakati wa kutaka kumuajiri.

Mwenyekiti wa Tume ya Kurekebisha sheria Zanzibar Jaji Mshibe Ali Bakari, anasema mapungufu yaliomo kwenye sheria hiyo iliodumu kwa miaka 13 sasa, ndio yaliowasukuma kutaka kuifanyia marekebisho.

“Muajiri kwa mujibu wa sheria hii na kanunui yake, anawajibu wa kumchunguuza mtu anaetaka kumuajiri kwenye utumishi wa umma kwa kumfanyia uchunguzi, hili ni kunyume na sasa tunataka kuingiza kifungu cha kufanyia uchunguuzi hata akiwa kazini kila baada ya muda”,anasema.

Ingawa kununi na sheria hiyo, imetoa haki iwapo muajiriwa atajifanyia mwenyewe uchunguuzi na kujibaini ana magonjwa yaliosababishwa na kazi yake, hapo muajiri (serikali) inaweza kumtibu hadi nje ya nchi.

Nayo sheria afya na usalama kazini no 8 ya mwaka 2005 kwenye kifungu chake cha 58, kimeweka wazi kuwa ‘kila baada ya muda wafanyakazi, watachunguuzwa afya zao na daktari wenye sifa ambao wataidhinishwa na Mkurugenzi’

Aidha kifungu hicho kilifafanua kuwa, gharama za uchunguuzi huo zitalipwa na Muajiri (serikali), ingawa wastaafu hao waliozungumza na mwandishi wa makala haya, hawakumbuki kufanyiwa uchunguuzi huo, hadi kustaafu kwao.
Asha Muhidini muajiriwa wa wizara ya Afya Pemba, amesema yeye mwakani anastaaafu, ingawa hakumbuki hata siku moja kuitwa na muajiri wake, kwa ajili ya kufanyiwa uchunguuzi.

“Ukali na umakini wanaokuwa nao waajiri wakati wanapotaka kuajiri kwa kuwafanyia uchunguuzi wa afya zao, basi hata baada ya kuwaajiri watekeleze sheria ya kuwafanyia uchunguuzi”,alifafanua Asha.

Nae Mwajuma Hassan Kombo mwalimu katika skuli moja ya sekondari Wete, ambae hakupenda jina la skuli ichapishwe, alisema zaidi wao wanaoishi na vumbi la chaki, ndio walipaswa kuangaliwa haraka.

“Mimi niliomba kustaafu mapema, maana macho yalishaanza kupoteza nuru, kutokana na kuzidiwa na vumbi la chaki, ingawa sikumbuki kuambiwa nikachunguuzwe, na hata nilipoamua kujitibu gharama nilipoomba sikupewa”, alifafanua .

Afisa Mdhamini wizara  Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati Pemba, Juma Bakari Alawi, anasema anaelewa uwepo wa jukumu la kuwafanyia uchunguuzi wa kiafya wafanyakazi wao, ingawa tatizo ni ukosefu wa fedha za kugharamia.

“Kwenye bajeti ijayo ya mwaka 2018/2019, tunatarajia sasa tutenge bajeti maalumu kwa ajili hiyo, maana kweli wapo wafanyakazi wanatarajia kustaafu karibuni, lakini hawajawahi kufanyiwa”,alifafanua.

Afisa Mdhamini wizara ya Miundombinu na Mawasiliano Pemba, Hamad Ahmed Baucha, anasema kwa mara ya mwisho aliwafanyia wafanyakazi wake uchunguuzi wa afya zao, mwaka 2016, na bajeti yake aliitoa kupitia mfuko wa barabara.

“Sisi mwaka 2013, tuliwafanyia lakini na mwaka jana 2016 pia tuliwafanyia, ingawa wengine hupuuza tangaazo la kuwafanyia, lakini wengine hasa wanaofanyakazi kwenye mavumbi hulifurahia”,anabainisha.

Anakiri kuwa, kwenye bajeti ya mwaka 2017/2018 kifungu hicho cha fedha hakikuingizwa, ingawa kwenye bajeti ijayo ya mwaka 2018/2019, watahakikisha kunakuwa na kifungu kwa ajili gharama ya kuwafanyia uchunguuzi wafanyakazi wao.

Khamis Mohamed Maliki na Asha Mohamed Hilali ambao ni wafanyakazi wa wizara hiyo, wamekiri kufanyiwa uchunguuzi wa kiafya, bila ya malipo, ingawa sasa ni mwaka wa pili hawajafanyiwa tena.

“Mimi niligundulika na na tatizo la uoni hafifu, na kisha wizara yangu ikanipatiwa miwani na hadi sasa natumia miwani ambayo gharama ilitoka wizarani kwangu”,anafafanua.

Afisa Utumishi wizara ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Pemba, Mohamed Juma Rashid anasema wao kila mwaka huwafanyia uchunguuzi wafanyakazi wao wote 110, na wapo waliowagundua na maradhi kadhaa.

“Tulipokwishawagundua sasa faida yetu kubwa, wanapotuaga kwamba hawahudhurii kazini, tumeshajua wanakabiliwa na maradhi gani”,anabainisha.

Raya Ahmada wa wizara hiyo, anasema utekelezaji huo wa sheria ya Afya na Usalama Kazini no 8 ya mwaka 2005, ya wao kufanyiwa uchunguuzi, haupaswi kudharauwaliwa na wafanyakazi na hasa wale wanaofanyakazi sehemu za mionzi au vumbi.

Hata Afisa Mdhamini wizara ya Afya Pemba, Bakari Ali Bakar anasema tokea ateuliwe kushika nafasi hiyo mwaka 2016, hadi sasa hajawahi kuwafanyia uchunguuzi wafanyakazi wake, na sio kwa sababu ya  ukosefu wa bajeti.

“Mimi tokea nishike nafasi hii mwaka wa pili sasa, sijawahi kuwafanyia uchunguuzi wa kiafya wafanyakazi wangu 1,257, na hii inatokana na hatujajipanga sisi wenyewe tu ndani ya ofisi yetu”,anabainisha.

Katibu Mkuu wa Shirikisho la vyama vya wafanyakazi Zanzibar ZATUC Khamis Mwinyi, anasema wamekuwa wakilifuatili hilo na mengine, ingawa huelezwa kuna uhaba wa vitendea kazi kwenye kitengo cha afya na usalama kazini.

“Sisi ZATUC bado tunaiomba serikali kuhakikisha wanaitekeleza sheria hiyo halali, ili kuona wanawabaini wafanyakazi wanaohitaji kufanyiwa matibabu, ili wafanye kazi zao kwa ufanisi”,alieleza.

Alibainisha kuwa mfanyakazi, imara na mwenye uzalisha bora ni yule mwenye afya njema, iwe kwa kujifanyia uchunguuzi kwa gharama zake, au muajiri kama sheria no 8 ya mwaka 2005 ya afya na usalama kazini inavyoataka.

Waziri wa Nchi Afisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi wa Umma na Utawala Bora Zanzibar Mhe: Haroun Ali Suleiman, anasema ni wajibu kwa waajiri kuwafanyia uchunguuzi wa kiafya waajiriwa wao, kama alivyowahi kuwafanyia yeye.

“Japo kila baada ya miaka miwili, wanatakiwa wawafanyie uchunguuzi, wasiweke umuhimu na umakini wanapotaka kuwaajiri tu, hiyo sio halali”,alieleza.

Ali Makame Ali (76) aliekuwa mfanyakazi Kilimo kitengo cha Utibabu wa mimea tokea mwaka 1964 hadi alipostaafu mwaka 2008, hakumbuki hata siku moja kufanyiwa uchunguzi wa kiafya hadi anastaafu.

“Likizo nilikwenda mara 13, ingawa nimeitumikia serikali miaka 44 mfululizo, tokea nipoajiriwa mwaka 1964 hadi nilipomaliza utumishi kwenye kitengo cha utibabu wa mimea”,alinieleza.

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa sasa iko katika mchakato wa mwisho kuhakikisha wafanyakazi wake wote kwenye sekta za umma wanakuwa na Bima za Afya.
Mwisho



No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.