Habari za Punde

Rais Dk Shein: Dhamira njema ya serikali kuwapa wananchi ekari tatu yaanza kuharibiwa


STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
  Zanzibar                                                             10.10.2017
---
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema kuwa katika kipindi cha hivi karibuni dhamira njema ya kuwapa eka tatu wananchi kwa ajili ya kilimo iliyooneshwa na uongozi wa Serikali tangu awamu ya Kwanza hadi hii ya Saba, imeanza kuharibiwa na baadhi ya wananchi kwa kuziuza eka hizo na wengine kuzikata viwanja vya kujenga nyumba na kuwauzia watu.

Dk. Shein aliyasema hayo leo katika ufunguzi  wa maonesho ya Siku ya Chakula Duniani, yaliofanyika huko Kizimbani na kuhudhuriwa na wananchi pamoja na viongozi mbali mbali akiwemo Makamo wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Idd, Mama Mwanamwema Shein na viongozi wengine wa vyama vya siasa na Serikali.

Katika hotuba yake, Rais Dk. Shein alisema kuwa kitendo hicho si kizuri kwani kinavunja mwelekeo wa azma ya Mapinduzi matukufu ya Januari 12, 1964 sambamba na kupelekea vizazi vijavyo kukosa sehemu za kilimo na hatimae kuagiza vyakula nje ya nchi.

Aliongeza kuwa ipo haja ya kuzingatia matumizi mazuri ya ardhi ndogo iliyopo kwa kutenga maeneo ya kilimo, maeneo ya makaazi na shughuli nyengine za kiuchumi sambamba na kuzingatia sheria za Mipango Miji na Vijiji.

Aliongeza kuwa hivi sasa Zanzibar ina watu milioni 1.4 hali hiyo inachangia kuwa na matrumizi makubwa ya ardhi hasa kwa ajili ya makazi na kupnguza ardhi ya kilimo, hivyo wananchi wanapotaka kujenga ni vyema wakapeka maombi yao katika Wizara ya Ardhi, Maji, Nishati na Mazingira ili waelekezwe taratibu ziliopo.

Alisema kuwa hivi sasa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeamua kufanya Mapinduzi ya Kilimo kwa kukifanya kilimo kuwa cha kisasa na cha kitaalamu hatua ambayo imeanza kuzaa matunda kwa kuongezeka kwa kiwango cha mavuno na mazao mbali mbali hasa mazao ya chakula yanayolimwa hapa nchini.

Alieleza kuwa mavuno ya mpunga yameongezeka kutoka wastani wa tani 33,655.06 mwaka 2013 hadi tani 39,000, zilizovunwa mwaka huu, 2017 kiwango ambacho hakijawahi kufikiwa kwa takriban miaka kumi iliyopita.

Dk. Shein alieleza kuwa kwa upande wa mazao ya matunda mavuno yake yameongezeka kutoka wastani wa tani 15,000 mwaka 2015/2016 hadi wastani wa tani 27,000 mwaka 2016/2017, mafanikio haya yametokana na matumizi ya mbinu za kilimo cha kisasa na kuzingatia maelekezo ya wataalamu wa kilimo.

Rais Dk. Shein alieleza kuwa Serikali inazingatia umuhimu wa kilimo cha umwagiliaji maji hasa kwa zao la mpunga ambapo kwa kushirikiana na Benki ya Exim ya Korea, Serikali itatumia wastani wa Dola za Kimarekani milioni 50 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji wa hekta 1,524.

Alisisitiza kuwa lengo la Serikali ni kuongeza mavuno ya mpunga nchini, kupunguza na hatimae kuondoa kabisa utegemezi wa kupata mchele kutoka nje ya nchi ambapo hivi sasa kwa kila mwezi Serikali inaingiza wastani wa tani 7,259 za mchele.

Kwa upande wa zana za kilimo, Dk. Shein alisema kuwa katika kuziendeleza na kuziimarisha huduma za matreka, Serikali imeandaa Mpango madhubuti wa Kiwanda cha Matrekta cha Mbweni kuwa Wakala kwa mujibu wa sheria na kukipa hadhi yake inayostahiki katika kilimo ambapo imekubaliana na Kampuni ya Mahindra Mahindra ya India kwa lengo la kuleta  matrekta mapya 100, zana nyengine za kilimo na hivi karibuni Serikali imesaini matrekta 20 kwa kuanzia na tayari yamepokewa matrekta 10 kutoka Serikali ya Libya.

Kwa maelezo ya Dk. Shein alisema kuwa Serikali inaendelea na dhamira yake ya kujenga soko kubwa jipya la kisasa la uvuvi katika eneo la Malindi kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Japan (JICA).

Kadhalika, Dk. Shein alsiema kuwa Serrikali imeanzisha kampuni ya Uvubvi ya Zanzibar (ZAFICO) kwa mtaji wa TZS Bilioni 7 kutoka kwenye mashirika ya Serikali na katika muda mfupi ujao Serikali inatarajia kuansiha shughuli za uvuvi kwa kununua meli 2 za kisasa kwa kuanzia ambazo zitatoa ajira kwa vijana.

Pamoja na hayo, Dk. Shein alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kushirikiaja na Serrikali ya Korea chini ya usimamizi wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) inajenga kituo cha kutotolea vifaranga vya samakli huko katika eneo la Beit Ras.

Dk. Shein pia, aliwataka vijana kuzitumia fursa zilizopo za kujiajiri katika sekta ya kilimo kwani kilimo kinatoa fursa kubwa na ya pekee inayompa mwananchi fedha nyingi kwa kipindi kifupi sambamba na kuwa na uhakika wa chakula na maendeleo ya nchi.

Baada ya hotuba hiyo Dk. Shein alipata fursa ya kutembelea mabanda ya maonesho na kujionea shughuli za kilimo, ufugaji na uvuvi huku akisisitiza haja ya Taasisi ya uvuvi wa Bahari Kuu kushirikiana na Taasisi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuimarisha uvuvi wa Bahari Kuu.

Mapema Waziri wa Kilimo , Maliasili, Mifugo na Uvuvi Hamad Rashid Mohamed alisema kuwa maonyesho hayo ni katika kutekeleza maagizo waliyopewa na Dk. Shein katika kutayarisha maonyesho hayo yanayoendana na sikukuu ya wakulima ya nanenane huku akieleza haja ya kuwepo kiwanja kama hicho huko kisiwani Pemba kwa madhumuni kama hayo.

Katibu Mkuu wa Wizara Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi Joseph Abdalla Meza alisema kuwa eneo hilo limetengwa kuwa ni eneo la kudumu lenye heka 16 ambapo miongoni mwa shughuli zilizofanyika ni kwuez uzio, njia, miundombinu ya maji, umeme na kugharimu TZS milioni 89 na hadi kukamilika kwa majengo ya kudumu kutagharimu TZS milioni 223.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 
 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.