Habari za Punde

Wananchi Watatu Kisiwani Pemba Tayari Wahojiwa kwa Tuhuma za Mauwaji

Na.Haji Nassor - Pemba.
JESHI la Polisi Mkoa wa kusini Pemba, tayari limeshawahoji watu watatu kwa tuhuma za mauwaji ya kijana Kheri Ali (30) mkaazi wa Chanjamjawiri wilaya ya Chakechake kisiwani humo, alieuwawa kwa tuhuma za wizi wa karafuu.
Kamanda wa jeshi hilo mkoani humo, Shehan Mohamed Shehan, alisema kifo cha marehemu kilitokezea hospitali kuu ya Chakechake kisiwani Pemba, ambapo alipelekwa kwa ajili ya matibabu.
Alisema kijana huyo, baada ya kuokotwa akiwa taabani mabonde ya Mperani shehia ya Chanjamjawiri akiwa na majereha kadhaa mwilini mwake, yanayonyesha kukatwa kwa kitu chenye ncha kali, alifikishwa hospitali ambako alifariki.
Kamanda huyo wa jeshi la Polisi Mkoa wa kusini Pemba, alieleza kuwa, marehemu alifariki kutokana na kumwagika damu isio na ya kawaida kutokana na majeraha yaliokuwa yameenea mwilini mwake.
“Marehemu inaonyesha alipigwa kwa kitu chenye ncha kali, maana alikuwa na majereha mabegani, kichwani, kiunoni na miguuni, hivyo damu nyingi ilipotea, hali iliosababisha kifo chake”,alifafanua.
Aidha Kamanda Shehan alisema, baada ya kumalizika kwa taratibu za kisheri, Jeshi la Polisi liliingia mtaani na kufanikiwa, kuwakamata watu watatu na kuwahoji.
Aliwataja waliokama na kuhojiwa na sasa kupata dhamana na kipolisi ni Salum Sultan Salum (39), Ali Rashid Abdalla (53) na Juma Abdalla Ali (24) wote wakaazi wa Matuleni wilaya ya Chakechake.
Alieleza kuwa, watuhumiwa hao awali waliwekwa ndani na kisha baada ya kuamaliza mahojiano nao, waliwapa dhamana, ambapo moja ya sharti ni kuripoti Kituo cha Polisi kila baada ya siku mbili.
Aidha jengine walilolifanya kwa watuhumiwa hao, ni kuchukuliwa kwa alama zao za vidole na samba mba na kuwapiga picha, ili kama wakitoroka iwe rashisi kupatikana.
Hata hivyo alisema uchuguzi wa tukio hilo ukikamilika pamoja na taratibu nyengine na kama wakionekana wanahusika, watafikishwa mahakamani kujibu tuhuma hizo.
“Wananchi waache kujichukulia sheria mikononi mwao, maana sheria za nchi hazikubaliani na hilo, wakiwapata watu wanaowatuhumu kwa wizi, wasisite kuwafikisha mbele ya vyombo husika”,alieleza.
Baadhi ya wananchi ambao hawakupenda majina yao yaandikwe, walisema chanzo cha jamii kujichukulia sheria mikononi mwao, ni kutokana na sheria za wahalifu kuwa legelege.
Walisema kijana huyo kabla ya kupoteza uhai wake hapo juzi, alishapelekwa kituo cha Polisi kwa kosa la wizi wa karafuu, ingawa wiki moja alionekana mtaani na kisha kuripotiwa, kufariki kwenye mazingira yanayofanana na yale ya mwanzo.

Hili ni tukio la tatu kwa watu wanaodhaniwa kuwa ni wizi, kuuwawa wakiwa mikononi mwa wananchi, wanaodaiwa kuwa na hasira, ambapo kati ya hao wawili walitokea eneo hilo hilo la Chanjamjawiri.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.