Habari za Punde

Msako wa kubaini wanaorundika karafuu kavu ndani wafanyika


NA HAJI NASSOR, PEMBA
MSAKO wa kawaida kwa wananchi na wakulima, wanaozihifadhi majumbani karafuu kavu kinyume na sheria, ulifanyika ghalfa, kwenye shehia ya Msuka wilaya ya Micheweni, ukiongozwa na kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa wa Kaskazini Pemba.

Akizungumza mara baada ya kumalizika msako huo, ambao haukubaini kuwepo kwa karafuu hizo, Mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama mkoani humo, Omar Khamis Othman alisema hilo ni zoezi la kawaida.

Alisema zoezi hilo halimlengi mtu mmoja, bali kila kamati inapoona inafaa na kwa shehia nyengine, humuarifu sheha wa shehia husika na kulifanya, ili kujiridhisha.

Alisema wananchi watakaobahatika kupitiwa na zoezi hilo, wasiwe na wasiwasi wala kujisikia vibaya, kwani ni sehemu ya kazi ya kamati ya ulinzi na usalama.

Mwenyekiti huyo wa kamati ya ulinzi ambae pia ni Mkuu wa Mkoa wa kaskazini Pemba, alisema kwa vile ni kinyume kuzihifadhi karafuu kavu ndani bila ya kuwa na nyaraka kutoka ZSTC, ndio maana kila wanapopata taarifa, huamua kujiridhisha.

“Msako huu hauna lengo la kumdhalilisha mwanchi yeyote, kwani ni sehemu ya kazi yetu kama walinzi wa wananchi na mali zao, maana pamoja na kwamba ni kosa kukaa na karafuu, lakini pia ni hatari kwa mwenye nyumba”,a lieleza.

Katika hatua nyengine Mkuu huyo wa Mkoa, alisema zoezi kama hilo walilifanya hivi karibuni shehia za Mtambwe na kukamata idadi kubwa ya gunia za karafuu, ambapo linalofuata ikiwa mmiliki huyo mali ni yake, huuzwa na kupewa fedha zake.

Kamanda wa Polisi Mkoa huo, Haji Issa Haji, alisema msako wa karafuu nyumba hadi nyumba, utafanyia kila wanapopokea taarifa za kuwepo kwenye shehia mbali mbali.

Kamanda huyo, aliwataka wananchi na viongozi wa shehia, kutoa ushirikiano wa hali ya juu, maana wapo wananchi wasiokuwa wema, huzitorosha kimagendo karafauu hizo.

Mdhamini wa Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na uhujumu wa uchumi ZAECA, Pemba, Suleiman Ame Juma, alisema ili zoezi kama hilo na jengine lifanikiwe, lazima wananchi washirikiane na taasisi nyengine.

“Sisi ZAECA na hata Polisi, tunahitaji ushirikiano na wananchi tena hasa wa kawaida kutoa taarifa kwetu, ili sisi tuangalie sheria zinasemaje”,alieleza.

Baadhi ya wananchi waliofanyiwa upekuzi huo, walisema wanashukuru kamati hiyo ya ulinzi na usalama, kutokana na kuwasafisha kwao na hata kwa wananchi wenzao.

Abdalla Ali Said (65), alisema sasa ameshatoka wasiwasi ambao pengine wananchi waliokuwa nao au hata serikalini, kutokana na kuhifadhi karafuu kinyume na sheria, jambo ambalo sio sahihi .

Nae Salma Said Salim, alisema mume wake ni kweli amekodi mikarafuu wilaya ya Chakechake, lakini amekuwa akiuza kila wiki mara moja na wala hajawahi kuhifadhi karafuu ndani mwake.

“Kama mnawasiwasi wa karafuu, Sheha piteni na watu wako mtafute, lakini humu hata za dawa hazimo, maana mume wangu anatabia kila mwisho wa wiki anaunza ZSTC”,alisema.

Zoezi la msako wa karafuu kavu kwa wananchi wanaoziweka ndani kwa muda bila ya kuziuza ZSTC, au kutokuwa na nyaraka,  umekuwa ukifanyika kwa mtindo wa kushitukia, ambapo hivi karibuni ulinasa gunia zaidi ya 100 shehia za Mtambwe.

                 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.