STATE
HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF
THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar
29.11.2017

RAIS wa Zanzibar
na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amemtumia salamu za
pongezi Rais wa Jamhuri ya Kenya Uhuru Muigai Kenyatta kwa kuapishwa kuwa Rais
na kuendelea kuiongoza nchi hiyo kwa kipindi cha pili.
Sherehe za kuapishwa kwa Rais Kenyatta
zilifanyika hapo jana Novemba 28, 2017 katika uwanja wa Kasarani Mjini Nairobi na
kuhudhuriwa na maelfu ya wananchi na viongozi mbali mbali wa Kimataifa wakiwemo
baadhi ya Marais kutoka nchi za Afrika ambapo kwa Tanzania Makamo wa Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Samia Suluhu Hassan alimuwakilisha Dk.
John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Katika salamu
hizo za pongezi Dk. Shein alimueleza Rais Kenyatta kuwa wananchi wa Zanzibar wanaungana
na ndugu zao wa Kenya katika kusherehekea ushindi wa kiongozi huyo pamoja na
kuahidi kuendelea kumuunga mkono kiongozi huyo ili aendelee kuiongoza vyema
nchi hiyo kwa amani na utulivu.
Salamu hizo zilieleza kuwa ushindi wa Rais
Kenyatta wa asilimia 98.2 ya wananchi waliomchagua katika uchaguzi wa marudio
uliofanyika nchini humo umeonesha wazi kuwa Rais Kenyatta anakubalika kwa
wananchi wa nchi hiyo kutokana na juhudi zake za maendeleo kwa nchi yake na
nchi zote za Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa jumla.
Aidha, Dk. Shein alimuhakikishia Rais Kenyatta
kuwa Zanzibar itaendeleza uhusiano na ushirikiano mkubwa uliopo kati yake na Kenya
sambamba na kuimarisha udugu uliopo kati ya wananchi wa nchi hiyo na wananchi
wa Zanzibar.
Sambamba na hayo, salamu hizo zilieleza kuwa
kuchaguliwa kwake Rais Kenyatta kwa mara ya pili ni fursa adhimu aliyopewa na
wananchi wa Kenya kwa ajili ya kuendeleza dhamira yake ya kulitafutia maendeleo
ya haraka Taifa hilo, kuimarisha Jumuiya ya Afrika Mashariki pamoja na Taasisi
mbali mbali za Kimataifa.
Hivyo, Dk. Shein alimtakia uongozi mwema, afya
njema kiongozi huyo wa Taifa la Kenya, pamoja na kuendeleza maendeleo endelevu
yaliopatikana nchini humo.
Rais Kenyatta
aliyezaliwa Oktoba 26 mwaka 1961 akiwa mtoto wa kwanza wa Rais Mzee Jomo
Kenyatta na mkewe Mama Ngina Kenyatta alichaguliwa tena kuwa Rais wa Kenya
baada ya kuibuka mshindi katika kinyanganyiro cha kuwania urais kwa silimia 98.2
ya Kura katika uchaguzi wa marudio
wa Oktoba 26 mwaka huu.
Katika hotuba
yake aliyoitoa hapo jana mara baada ya kuapishwa Rais Kenyata alitangaza kuwa
kuanzia sasa raia wa nchi za Afrika Mashariki kwa kutumia vitambulisho vyao vya
uraia wa nchi zao wataweza kufanya kazi, kumiliki mali, shamba, kuoa na kuolewa
sambamba na kuishi nchini humo.
Rajab
Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment