Habari za Punde

“Wanaofanya sulhu kesi za udhalilishaji wafungwe”


NA ZUHURA JUMA, PEMBA

BABA mwenye umri wa 42 mkaazi wa Kiungoni Wilaya ya Wete, ambae alidhalilishiwa watoto wake wawili wa miaka 14 na sita (6), amesema wanaofanya suluhu kwenye kesi za udhalilishaji, sasa wafunguliwa mashitaka,  kwani wanavipalilia vitendo vya udhalilishaji.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, baba huyo alisema kuwa, kwa mwaka huu ameshadhalilishiwa watoto wake wawili, ikiwemo wa miaka sita kwa kubakwa na wa miaka 14 kutoroshwa.

Alisema kuwa, wanaofanya suluhu kwa vitendo vya udhalilishaji wanahitaji kufungwa, kwani inasababisha kuongezeka kwa vvitendo siku hadi siku, katika jamii.

“Suala la udhalilishaji ni kubwa katika jamii na tunabeza kwa kufanya suluhu, hivyo wanaodhalilisha wanasonga mbele kuwadhalilisha watoto, kwa kweli linatuumiza hili”, alisema baba huyo.

Alieleza kuwa, Oktoba 27 mwaka huu saa 5:00 usiku alitoroshwa mtoto wake wa miaka 13, ambapo Rashid Ali Mbarouk (24) alimchukua mtoto huyo na kwenda nae katika nyumba anayolala na kumfanyia udhalilishaji.

Baba huyo alieleza kuwa, siku hiyo alikwenda hospitali kumpeleka mke wake kujifungua, ingawa aliporudi mtoto ndani hayupo, na ndipo alianza hatua ya kumtafuta.

“Nilipoanza kumtafuta nilimsikia akisema kwa ami yake, alikuwa akimwambia amlete nyumbani kwani anaogopa kuja kumpiga na ndipo nilipofika huko akatueleza kuwa alichukuliwa na mtuhumiwa”, alisema mzazi huyo.

Alieleza kuwa, aliambiwa na mtoto wake kuwa walipoondoka wao kwenda hospitali, alikwenda mtuhumiwa na kugonga mlango wa nyumba yao, ambapo baada ya kufungua alimkamata mikono na kumburuza hadi nyumba anayolala”, alisema.

“Aliniambia kuwa, aliposikia gari tuliyokwenda nayo hospitali inarudi akamuachia, ingawa aliwahi kumchezea katika sehemu zote za mwili wake, jambo ambalo liliniumiza sana”, alisema baba huyo.

Mzazi huyo alisema kuwa, tayari kesi hiyo ameshairipoti kituo cha Polisi, ingawa aliambiwa kuna uhaba wa askari wa kufanya upelelezi, jambo ambalo limemfanya mtuhumiwa kupita mitaani kwa kujigamba.

Alieleza tukio jengine alisema baba huyo kuwa, mtoto wake mwenye umri wa miaka sita (6) alibakwa na mtoto mwenzake mwenye miaka 15, ingawa kesi hiyo haikufika popote kutokana wazee kujikusanya pamoja na kusuluhisha.

“Alipobakwa mtoto wangu wa miaka mitano, wazee walikaa na kusuluhisha kumbe ndio wanapalilia hivi vitendo, mwaka huu huu tayari tena kashatoroshwa mtoto wangu mwengine”, alisema baba huyo.

Mratibu wa wanawake na watoto shehia ya Kiungoni Mchanga Said Hamad alisema kuwa, alimfuatilia baba huyo kuhusiana na kesi ya kutoroshwa kwa mtoto huyo hivi karibuni, ingawa hakutaka kutoa mashirikiano.

“Ile kesi ya kubaka wenyewe walifanya suluhu na hii ya kutorosha pia huyu baba kwanza hakuwa tayari kuifikisha kesi kwenye vyombo vya sheria na kutwambia tumuachie, ingawa tulimpa elimu na kuona umuhimu wake na kwenda kuripoti na kesi Polisi kwa sasa”, alisema Mratibu huyo.

Sheha wa Shehia hiyo Omar Khamis Othman alisema kuwa, shehia hiyo ni kitovu cha dini ya kiislamu, kutokana na kuwepo kwa masheikhe wengi na wakubwa na kubahatika kufikiwa na mradi wa GEWE.

Mkuu wa dawati la wanawake na watoto Wilaya ya Wete Khamis Faki Simai alisema tayari tukio hilo limeripotiwa katika dawati, ambapo Rashid Ali Mbarouk (24) wa Kiungoni anatuhumiwa kumtorosha mtoto wa kike mwenye umri wa miaka 14 na kumchukua kwenye nyumba yake ya kulala na kumdhalilisha kwa kumchezea mwili wake.


Alieleza kuwa, wanaendelea na uchunguzi wa tukio hilo na mara upelelezi utakapokamilika hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya mtuhumiwa huyo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.