Habari za Punde

ELIMU YA MAANDALIZI ISIPUUZWE

Na Salum Vuai, MAELEZO

WALIMU wakuu wa skuli za Zanzibar wametakiwa kutambua hadhi ya elimu ya maandalizi badala ya kuipa kisogo na kuwatenga walimu wanaosomesha madarasa hayo.
Ofisa Mdhamini wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Elimu Pemba Salum Kitwana Sururu, amesema elimu hiyo ndio msingi mzuri wa kumjenga mtoto.

Akizungumza na washiriki wa kikao cha tathmini ya mradi wa ‘Watoto Kwanza’ uliolenga kuwaandaa walimu wa skuli za maandalizi unaohitimisha miaka minne kilichofanyika hoteli ya Mazson, Sururu alisema Serikali ya Mapinduzi Zanzibar mwaka 2006 ilitangaza sera ya ulazima wa elimu ya maandalizi kwa watoto kuanzia miaka minne hadi mitano.

Alifahamisha kuwa, ufahamu mzuri wa wanafunzi wa msingi na sekondari, hutokana na kupitia madarasa ya maandalizi ambako hufinyangwa na kuandaliwa njia njema ya kupata ufanisi katika masomo yao.

Sururu alisema si sifa njema pale walimu wakuu  wanaotegemewa kuwa washaajishaji wa sera ya elimu ya maandalizi, wawe mstari wa mbele kuwapuuza walimu waliofundishwa kwa ajili ya madarasa hayo.  

Alieleza masikitiko yake kwamba bado kuna kundi ambalo haliko tayari kuipa elimu ya maandalizi wala walimu wa madarasa hayo haki wanayostahiki kwa manufaa ya watoto ambao kimsingi ndio walimu, wataalamu na viongozi wa kesho.

Aidha ofisa huyo aliwataka walimu kubadilika na kushirikiana kwa pamoja ili kuhakikisha sera ya elimu ya maandalizi inapata mafanikio kama ilivyokusudiwa na serikali.

“Tufike pahala tujue thamani ya fedha zinazotolewa na wafadhili kwa mamilioni kwa ajili ya kuisaidia nchi yetu kuendeleza sekta ya elimu, tuoneshe  utayari wetu katika kuleta matokeo chanya,” alisisitiza.

Alieleza matumaini yake kuwa walimu waliopata mafunzo kwa ajili ya kufundisha skuli za maandalizi watatumia elimu waliyopata kuinua kiwango cha watoto wanaopewa dhamana ya kuwasimamia pamoja na kubuni vifaa mbalimbali vya kufundishia kutokana na rasilimali zinazowazunguka.

Alitumia fursa hiyo kuishukuru taasisi ya Dubai Cares iliyofadhili mradi huo pamoja na ‘Madrasa Early Childhood Programe-Zanzibar (MCEP-Z), kwa kuuhitimisha kwa mafanikio makubwa licha ya changamoto kadhaa zilizojitokeza. 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.