Habari za Punde

Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa Zanzibar yakutana na wadau

 Afisa Mipango wa kamisheni ya Maafa Zanzibar  Haji Faki Hamdani   (wa tatu kulia ) akitoa muongozo wa mipango mikakati ya kazi kuhusiana na maafa huko Maruhubi Zanzibar.
Wajumbe kutoka Taasisi mbali mbali za Serikali na Binafsi walioshiriki katika kikao cha pamoja wakijadili mipango kazi ya  kuweka mikakati ya kukabiliana na maafa huko Maruhubi Zanzibar .

Picha na Khadija Khamis -Maelezo.

Na  Khadija  Khamis – Maelezo  

Mkurugenzi Mtendaji  Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa Zanzibar Shaaban Seif Moh’d  amewataka wadau mbali mbali kupanga mikakati ya pamoja ili kuweza kukabiliana na maafa pindi yakitokea na kupunguza adhari za maafa hayo kwa jamii.

 Hayo aliyasema katika ukumbi wa Kamisheni hiyo huko Maruhubi  wakati akifungua kikao cha siku moja kinachohusiana na  wadau mbali mbali kutoka taasisi za Serikali na binafsi kuhusu uimarishaji uratibu wa shuguli za maafa .

Alisema katika kutekeleza majukumu ya  ufanyaji  kazi lazima kuwepo mashirikiano ya pamoja katika utendaji mzima wa kazi ili kuhakikisha yanatekelezwa ipasavyo .

“Ufanyaji wa kazi ni kushirikiana na watu katika utendaji mzima wa kazi ili kuhakikisha kila mwenye jukumu lake anatekeleza kama utaratibu unavyotakiwa”, alisema Mkurugenzi  huyo.

Mkurugenzi huyo alifahamisha kuwa jukumu la kamisheni ni kuratibu masuala ya maafa yanayotokea ndani ya Zanzibar  na kuhakikisha wanakabiliana nayo ipasavyo na kuweza kuyadhibiti na kupunguza adhari za maafa hayo .

Nae Afisa  Operesheni wa Kamisheni wa Maafa  Makame Khatibu  Makame   akitoa mada inayohusiana na Dhana nzima ya Maafa alisema kuwa maafa ni tukio kubwa linalotokea katika jamii husika ambalo wanashindwa kukabiliana nalo na kuhitaji msaada kwa wengine.

Alieleza kuwa kuna maafa ya asili ambayo hutokea katika dunia ikiwemo mtetemeko wa ardhi kimbunga tsunami miripuko ya volcano na kadhalika jambo ambalo ni vigumu kukabiliana nalo kwa haraka kwani ni maumbile ya tabia ya nchi na baadhi ya maafa mengine husababishwa na binaadamu kwa bahati mbaya, makusudi au uzembe na kupelekea madhara kwa jamii.

Alifahamisha kuwa maafa huleta madhara makubwa kwa jamii ni vyema kuchukua tahadhari kwa kuepuka kuishi katika mazingira hatarishi ili kuweza kuinusuru jamii na mali zao pamoja na huduma za kijamii.  

 Aidha Afisa huyo alieleza changamoto zinajitokeza wakati wa maafa  ni pamoja na uwezo mdogo wa wa kukabiliana na maafa, ukosefu wa taarifa na urasimu katika upatikanaji wa taarifa, uhaba wa bajeti na upatikanaji wa fedha, ukosefu wa ramani zinazoonesha maeneo hatarishi kwa ujenzi,  kutotekeleza vyema baadhi ya sheria  pamoja na mwamko mdogo kwa wananchi .

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.