MAKAMU Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein
amewataka viongozi wote wa Chama Cha Mapinduzi kutekeleza majukumu yao ili
kuendelea kukipa ushindi chama hicho katika chaguzi zijazo na kuendeleza wimbi
la ushindi.
Makamu huyo wa
Mwenyekiti wa CCM Zanzibar aliyasema hayo leo huko katika ukumbi wa CCM Amani,
Mkoa wa Mjini katika hafla ya kumpokea na
kumpongeza baada ya kuchaguliwa kwa kura zote kuendelea kuwa Makamu Mwenyekiti
wa CCM Zanzibar katika mkutano Mkuu wa Tisa wa CCM Taifa uliomalizika hivi
karibuni huko mjini Dodoma.
Katika maelezo yake,
Dk. Shein alisema kuwa kuchaguliwa kwake kwa kura zote na kupata ushindi wa
asilimia mia moja ni deni ambalo malipo yake ni kuhakikisha anashirikiana
kikamilifu na viongozi wa CCM katika ngazi zote ili waweze kushinda kwa
kishindo katika uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 Tanzania Bara na Zanzibar.
Makamu Mwenyekiti huyo
aliahidi kuwa katika kutekeleza jukumu walilompa atahakikisha kwamba uchumi wa
Zanzibar unaendelea kuimarika sambamba na kudumisha amani, umoja na mshikamano
miongoni mwa wananchi wa Zanzibar na Tanzania kwa jumla.
Dk. Shein alisema kuwa
kazi hiyo anaiweza na ataifanya kwa bidii na kuongoza kwa uadilifu katika
kuhakikisha CCM kinazidi kuimarika hasa kutokana na ukongwe kwa chama hicho na
ndio maana watu walio wengi wanakipenda.
Alieleza kuwa kazi ya
uongozi wa achama hicho ni ya watu wote na kusisitiza haja kwa wale wote ambao
wan aharibu kutokana na wanayoyasema sio wanayoyatekeleza
“Naahidi kwa dhati ya
moyo wangu na kwa mapenzi niliyonayo kwa wananchi wote wa Tanzania na Chama
changu kwamba nitaendelea kulitekeleza jukumu hilo vizuri, kwa uadilifu na kwa
nguvu zangu zote’,alisema Dk. Shein.
Aidha,alisisitiza haja
ya kuwa imara katika kuyalinda Mapinduzi Matukufu ya Januari 12, 1964 ambayo
hivi karibuni yanatimia miaka 54 na kusisitiza kuwa kwa yeyote tule ambaye
atayabeza atashughulikiwa sambama na kudumisha Muungano uliopo.
Pamoja na hayo,
aliwataka viongozi waCCM kuhakikisha kwamba ratiba ya kazi za chama, mikutano
na ziara zinafanywa kama kalenda ya chama inavyoonesha na kusisitiza kuwa huu
si wakati wa kuyafunga kufuli Matawi ya chama hicho na wala sio wakati wa
kuwangojea viongozi wakuu wa CCM wafanye ziara na wao wafuate nyuma.
Sambamba na hayo,
aliwataka viongozi wa CCM wote kufuata taratibu zilizowekwa na chama hicho
katika kukosoana ikiwa ni pamoja na kuvitumia vikao vyao vya chama.
Alieleza kuwa kwa kila
aliepewa nafasi anapaswa aiweke mbele CCM, aipe heshima yake huku akiwataka
kuzingatia hotuba ya Mwenyekiti wa CCM Taifa Dk. John Pombe Magufuli aliyoitoa
wakati wa ufunguzi na ufungaji wa Mkutano Mkuu wa Tisa wa CCM uliofanyika
Disemba 18 mwaka huu huko Dodoma.
Sambamba na hayo, Dk.
Shein aliwaeleza wanaCCM waliohudhuria mkutano huo mipango ya Serikali ya
kujenga miji mipya ukiwemo mji wa Chumbuni na
Kwahani huku akieleza kuwa hivi karibuni ujenzi wa jengo la abiria
katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume, Zanzibar ujenzi wake
utaanza na kuchukua muda wa miezi 18 sambamba na hatua za ujenzi wa Bandari ya
Mpigaduri zinavyoendelea.
Pia, alieleza azma
yake ya kufanya ziara na kukutana na Mabalozi wa Wilaya zote za Unguja na Pemba
mara baada ya kumalizika sherehe za miaka 54 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Nao viongozi wa chama
hicho wakieleza kwa niaba ya viongozi wenzao wakiwemo Makatibu wa Mikoa,
Wenyeviti wanaCCM wote wa Zanzibar na wananchi kwa jumla walitoa pongezi kwa
Dk. Shein kwa mafanikio yaliopatikana sambamba na utekelezaji wake mzuri wa
Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2015-2020.
Aidha, viongozi hao
walimueleza Dk. Shein kuwa kutokana na uongozi wake uliotukuka ndani ya CCM
hapa Zanzibar umepelekea kuimarika kwa uchumi na kuongezeka kwa mapato ya chama
hicho huku wakimwagia sifa kutokana na uwamuzi wake wa kuwalipa Pencheni Jamii
wazee wote kuanzia miaka 70 bila ya kujali itikadi zao za kisiasa sambamba na
kuongeza mishahara.
Rajab
Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.u
No comments:
Post a Comment