Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa
Baraza la Mapinduzi Issa Ussi Haji Gavu ameeleza azma ya Serikali ya Mapinduzi
ya Zanzibar katika kukuza na kuimarisha uhusiano kati yake na Morocco hasa
katika masuala ya kiuchumi, kijamii na kiutamaduni kwa faida ya nchi mbili hizo
pamoja na watu wake.
Waziri Gavu aliyasema
hayo leo katika mkutano maalum uliohudhuriwa na viongozi wa Taasisi za Serikali
ya Mapinduzi ya Zanzibar na Balozi wa Ufalme wa Morocco katika Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Abdelilah Benryane, mkutano uliofanyika Ikulu mjini
Zanzibar.
Katika mazungumzo
hayo, alimuhakikishia Balozi Benryane
kuwa Zanzibar itaimarisha zaidi uhusiano na ushirikiano kati yake na Morocco
huku akieleza kuwa Zanzibar ina mambo mengi ya kujifunza kutoka nchini humo.
Waziri Gavu alisema kuwa
ziara ya kiongozi wa nchi hiyo, Mfalme Mohammed VI aliyoifanya hapa nchini
mnamo mwezi Oktoba mwaka jana imeonesha dalili za uhusiano na ushirikiano mwema
kati ya Tanzania ikiwemo Zanzibar na Morocco sambamba na ziara iliyofanywa na
baadhi ya watendaji wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar aliowaongoza Waziri
Gavu nchini humo mnamo mwezi Agosti mwaka huu.
Aliongeza kuwa katika
ziara hiyo muhimu iliyofanywa na Mfalme huyo wa Morocco hapa nchini Tanzania iliweza
kusaini makubaliano takriban 22 ya ushirikiano kati yake na Morocco katika
sekta mbali mbali za maendeleo ikiwemo kilimo, gesi, mafuta, utalii na sekta nyenginezo.
Waziri Gavu alimueleza
Balozi huyo kuwa ziara hizo kutokana na umuhimu wake zimeweza kusaidia kwa
kiasi kikubwa kuimarisha mashirikiano na uhusiano kati ya Zanzibar na Morocco
na kuna kila sababu ya kuendelezwa kwa hatua hizo muhimu.
Aidha, Waziri Gavu alimueleza
kiongozi huyo juhudi zinazochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
katika kutekeleza makubaliano yaliofikiwa sambamba na kusisitiza haja ya kuwepo
kwa mashirikiano katika sekta mbali mbali za maendeleo hasa ikizingatiwa kuwa Morocco
ni miongoni mwa nchi za Bara la Afrika iliyopiga hatua kubwa katika sekta za
maendeleo ikiwemo sekta ya utalii.
Sambamba na hayo, Waziri
Gavu alitumia fursa hiyo kuwakaribisha wawekezaji wa Morocco kuja kuekeza
Zanzibar katika sekta mbali mbali ikiwemo sekta ya uvuvi hasa wa bahari kuu na
kumueleza balozi huyo wa Morocco haja ya kuitangaza Zanzibar nchini mwake
kiutalii.
Nae Balozi wa Ufalme wa
Morocco katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Abdelilah Benryane alieleza kuwa
Morocco inajivunia uhusiano na ushirikiano mwema uliopo kati yake na Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania ikiwemo Zanzibar.
Balozi Benryane alisema
kuwa Morocco iko tayari kushirikiana na Zanzibar katika kuendeleza miradi mbali
mbali ya maendeleo na kumuhakikishia Waziri Gavu pamoja na viongozi wengine wa
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuwa nchi yake itaendelea kuiunga mkono
Zanzibar katika kuimarisha sekta mbali mbali za maendeleo.
Pamoja na hayo, Balozi
huyo alimuhakikishia Dk. Shein kuwa juhudi za makusudi atazichukua katika
kuhakikisha anajenga mashirikiano mazuri nchini mwake kwa kuendeleza uhusiano
na ushirikiano na Zanzibar katika sekta muhimu za maendeleo zikiwemo elimu,
afya, kilimo, uvuvi, utalii na nyenginezo
Morocco imepiga hatua
kubwa katika sekta ya utalii ambapo hivi sasa inapokea watalii milioni 16 kwa
mwaka kufuatia program ijulikanayo ‘Azur Blue’ iliyoanzishwa na kiongozi wa
nchi hiyo Mfalme Momamed VI ambapo pia, katika programu ya pili wamejiwekea
hadi kufikia mwaka 2020 watapokea watalii wapatao milioni 20.
Hivyo, kuwepo kwa
mashirikiano na uhusiano kati ya Zanzibar na nchi hiyo hasa katika sekta ya
Utalii ambapo Zanzibar nayo imo katika mikakati ya kuiimarisha sekta hiyo
sambamba na mafanikio na kuwepo wka vivutio vingi hapa nchini kutasaidia
kuitangaza Zanzibar kiutalii.
Mkutano huo umeweza
kuzungumzia masuala mbali mbali ya kuimarisha uhusiano kati ya Morocco na
Zanzibar ambapo ujumbe kutoka nchini Morocco unatarajiwa kuzuru Zanzibar mapema
mwakani ikiwa ni katika kutekeleza ushirikiano baina ya pande mbili hizo.
Mkutano huo pia,
ulihudhuriwa na Balozi Mohamed Ramia Abdiwawa Mshauri wa Rais, Ushirikiano wa
Kimataifa, Fedha na Uchumi, Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza
la Mapinduzi Salum Maulid na Mohamed MA Elainine kutoka Ubalozi wa Morocco,
Dar-es-Salaam nchini Tanzania.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment