STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Dodoma 11.12.2017

RAIS
wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amemtumia
salamu za rambi rambi Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Dk. Hussein
Ali Mwinyi kufuatia vifo vya wanajeshi 14 wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania
vilivyotokea tarehe 7 Disemba, 2017 katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo
ambako walikuwa katika shughuli za kusimamia amani.
Katika salamu hizo za
rambirambi Dk. Shein alimueleza Waziri Dk. Hussen Mwinyi kuwa amepokea kwa mshtuko na huzuni kubwa taarifa
hiyo ya vifo vya wanajeshi wa Jeshi la Wananachi wa Tanzania vilivyotokea
tarehe 7 Disemba, 2017 katika Jamhuri ya Kongo.
Kuufuatia tukio hilo Rais
wa Zanzibar alieleza kwua yeye binafsi, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
pamoja na wananchi wote wa Zanzibar wanawakumbuka wanajeshi hao kwa ujasiri na
uzalendo wao katika kuhakikisha amani inapatikana katika Jamhuri ya Kidemokrasia
ya Kongo na maeneo yote ya Maziwa Makuu.
Aidha salamu hizo za
rambirambi Dk. Shein alizitoa kwa Dk. Hussein Ali Hassan Mwinyi, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga
Taifa pamoja na Mkuu wa Majeshi ya
Ulinzi, familia za marehemu, ndugu, jamaa na marafiki pamoja na wananchi wote
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutokana na msiba huo.
Salamu hizo zilimuomba
MwenyeziMungu awape malazi mema mashujaa hao pamoja na kuwaombea wanajeshi
waliojeruhiwa wapate nafuu ya haraka na kurejea katika hali zao za kawaida.
Sambamba na hayo, salamu
hizo za rambirambi zilimuomba MwenyeziMungu awape Watanzania wote moyo wa
subira na uvumilivu katika kiipndi hiki kigumu cha msiba huu.
Tukio hilo limetoa katika
Kambi ndogo ya Semuliki iliyopo Kaskazini Mashariki mwa Wilaya ya Beni katika Jimbo la Kivu baada ya kuvamiwa na
waaasi wa kundi la ADF katika eneo hilo la Mashariki mwa nchi hiyo ya Kongo.
Tukio hilo limeelezwa kuwa
ni baya zaidi kuwahi kutokea kutekelezwa na waasi dhidi ya walinda amani wa
Umoja wa Mataifa (UN) katika historia ya miaka ya hivi karibuni.
Katika kipindi cha miezi
sita tukio hili ni la pili kutokea baada ya Oktoba mwaka huu wanajeshi wawili
wa JWTZ waliokuwa katika kundi la walinda amani kuripotiwa kuuwawa na wengine
18 kujeruhiwa.
Mbali na hao askari
wengine wawili pia, waliripotiwa kuuawa mwezi Mei 2015 katika eneo la Kivu
Mashariki mwa Kongo na mwengine wawili hawakujulikana walipo baada ya kuvamiwa na waaasi.
Katibu Mkuu wa Umoja wa
Mataifa (UN) Antonio Guterres
alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kulaani vikali shambulio hilo ambalo halijawahi
kutokea tokea JWTZ lianze kushiriki ulinzi wa amani nchini DRC mwaka 2011.
Rajab
Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address:
2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822
E-mail:
rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment