Habari za Punde

Seleembe: Tutabeba Ubingwa wa Chalenji Mwaka HuuNa Abubakar Khatib Kisandu, Machakos Kenya.

Nahodha wa timu ya Taifa ya Zanzibar (Zanzibar Heroes), Suleiman Kassim (Seleembe), amesema hakuna wa kuwazuia kubeba Kombe la CECAFA SENIOR CHALLENGE CUP msimu huu kutokana na ubora wa kikosi chao.

Seleembe ametamba kuwa kasi waloanza kuonyesha haitosimama mpaka kubeba taji hilo kwenye Mashindano ambayo yanaendelea nchini Kenya.

Nahodha huyo aliuambia Mtandao huu kuwa, uwepo wa wachezaji vijana wanaotaka kufanikiwa itaongeza chachu kupata matokeo, kitu ambacho walikikosa misimu uliopita.

“Tuna damu changa ambayo inataka mafanikio, sasa itakuwa ngumu sana timu yoyote kutuzuia msimu huu, tuna kila sababu ya kutwaa taji, vijana wanahamasa ya kupata mafanikio katika maisha ya soka, hakuna wa kutuzuia katika hili,” alisema.

Zanzibar Heroes wanaongoza kundi A wakiwa na alama 6 baada ya kuwafunga Rwanda 3-1 na jana kuwapiga kaka zao Tanzania bara 2-1 na kesho Jumamosi watacheza mchezo wao wa tatu dhidi ya wenyeji Kenya, mchezo utakaopigwa saa 10:00 za jioni katika uwanja wa Kenyatta uliopo Machakos nchini Kenya.

Endapo Heroes wakibeba kombe mwaka huu itakuwa ni kombe lao la pili katika Mashindano hayo kufuatia kutwaa mara moja tu mwaka 1995, huku mabingwa watetezi Uganda ndiyo mabingwa wa kihistoria wa michuano hiyo tangu mwaka 1971, wakiwa wamelitwaa mara 14, wakifuatiwa na Kenya mara sita, Ethiopia mara nne na Tanzania bara mara tatu.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.