Habari za Punde

Maandalizi ‘ZBC Watoto Mapinduzi Cup’ yaiva

MKURUGENZI wa ZBC Bi. Ayman Duwe akizungumza na waandishi wa habari pamoja na wawakilishi wa timu za soka wilaya za Unguja katika uzinduzi wa maandalizi ya michuano ya ‘ZBC Watoto Mapinduzi Cup’ 2018 uliofanyika leo Disemba 8, 2017 katika studio za ZBC TV mjini Zanzibar. Kushoto ni Mwenyekiti wa Kamati ya michuano hiyo Mzee Yunus.
MTAYARISHAJI wa vipindi vya michezo katika Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC) Khamis Mohammed ‘Mo 6’,  akiendesha droo ya timu zitakazoshiriki michuano ‘ZBC Watoto Mapinduzi Cup’ katika studio za ZBC TV leo Disemba 8, 2017. Kushoto ni mtangazaji Sadik a.k.a. DJ Flash.
MMOJA wa viongozi wa timu za wilaya zitakazoshiriki mashindano ya ‘ZBC Watoto Mapinduzi Cup’, akipokea fedha za maandalizi kutoka kwa Mkurugenzi wa ZBC Bi. Ayamna Duwe.

Na Salum Vuai, MAELEZO-ZANZIBAR

SHIRIKA la Utangazaji Zanzibar (ZBC), leo tarahe 8 Disemba, 2017, limezindua rasmi maandalizi ya mashindano ya pili ya mpira wa miguu kwa timu za watoto maarufu ‘ZBC Watoto Mapinduzi Cup’.

Uzinduzi huo uliofanyika katika studio za ZBC TV Mnazimmoja mjini Zanzibar, ulikwenda sambamba na upangaji makundi kwa timu za Wilaya saba za Unguja zitakazotoana jasho kwenye michuano hiyo maalumu kwa maadhimisho ya Mapinduzi ya Zanzibar ambayo mwakani yatakuwa yanatimiza miaka 54.

Akizungumza katika hafla hiyo mbele ya waandishi wa habari za michezo kutoka vyombo mbalimbali, Mkurugenzi wa ZBC Ayman Duwe alisema kufanyika kwa mashindano hayo ni kutimiza dhamira ya kuyaendeleza kama walivyoahidi wakati yakianza.

Duwe alieleza kuwa, mbali na kuongeza burudani kwa wapenzi wa soka nchini wakati wa sherehe za Mapinduzi, dhamira kuu ya michuano hiyo ni kuviendeleza vipaji vya wachezaji wadogo ambao ndio msingi wa timu imara za taifa pamoja na klabu zinazocheza ligi za madaraja ya juu ndani na nje ya nchi.

Aidha alisema baada ya kupata ushauri kutoka kwa wadau mbalimbali wa michezo, wameamua mashindano ya mwaka huu yachezwe kwa mtindo wa ligi badala ya kuanza hatua ya awali kwa mtoano.

Aliishukuru Serikali ya Mapinduzi Zanzibar chini ya Rais Dk. Ali Mohamed Shein, kwa kubariki michuano hiyo itumie jina la Mapinduzi kwa lengo la kuwapa watoto na vijana uelewa wa Mapinduzi ya Januari 12, 1964 yaliyoleta ukombozi wa visiwa vya Unguja na Pemba.

“Pamoja na shukurani kwa serikali, pia tunawashukuru wadau na taasisi mbalimbali zilizojitokeza kudhamini na kuchangia kwa namna tafauti mashindano ya kwanza wakati wa sherehe za miaka 53 ya Mapinduzi, pia tunaomba waendelee kutuunga mkono mara hii,” alieleza Mkurugenzi huyo.

Aidha alisema zawadi kwa washindi zimeboreshwa, na pia mchezaji bora, mwamuzi bora, mfungaji na mlinda mlango bora pamoja na chombo cha habari kitakachoripoti vizuri zaidi watazawadiwa pamoja na vyengine kutambuliwa japo kwa vyeti. 

Mapema, Mwenyekiti wa kamati ya mashindano hayo Mzee Yunus, alitaja viwanja vitakavyotumika kwa ajili ya ngarambe hizo, kuwa ni uwanja wa Amaan kwa timu za Wilaya ya Mjini, Maungani (Magharibi B) na Bububu Jeshini (Magharibi A).

Timu za Wilaya ya Kati zitatumia uwanja wa Uzini, Kusini (Kichaka nyuki Jambiani), Mahonda Kaskazini B na Wilaya ya Kaskazini A itacheza uwanja wa Mkwajuni.

Katika droo iliyofanyika, timu za Wilaya ya Kusini, Kaskazini B, Kaskazini A na Magharibi A zimepangwa katika kundi A, huku Mjini, Kati na Magharibi B zikiangukia kundi B.

Katika uzinduzi huo, Mkurugenzi wa ZBC pia alikabidhi fedha za maandalizi kwa wawakilishi wa timu hizo za Wilaya za Unguja.

Ubingwa wa michuano hiyo unashikiliwa na Wilaya ya Wete ambao waliibanjua Wilaya ya Mjini mabao 3-1 katika fainali ya mashindano ya kwanza mwaka jana uwanja wa Amani.
Fainali za mwaka huu zimepangwa kuanza kutimua vumbi Disemba 15 baada ya timu za 
Pemba nazo kupanga makundi na kukabidhiwa fedha za maandalizi.  

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.