Habari za Punde

Balozi Seif atoa miezi mitatu kufanyiwa matengenezo Ukumbi wa Mikutano wa Salama.

 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif  aliyevaa Miwani akifanya ziara ya kulikagua Jumba la Biashara lilipo Darajani Maarufu Jumba la Treni kuangalia harakati za ujenzi wa Jengo hilo.

Kushoto ya Balozi Seif ni Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Mheshimiwa Ayoub Mohamed Mahmoud.

  Mkurugenzi Muendeshaji wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar {ZSSF} Bibi Sabra Issa Machano akimueleza Balozi Seif hatua zilizochukuliwa za Ujenzi wa Jumba la Treni ambalo litakuwa Kituo cha Baishara.
 Balozi Seif akikagua jengo la Hoteli ya Bwawani na kuagiza kufanyiwa matengenezo ya Haraka Ukumbi wa Salama ndani ya Miezi Mitatu ili urejee kutoa huduma za Kijamii kama kawaida.

Kushoto ya Balozi Seif  ni Mkurugenzi Uenezi na Huduma wa Mamlaka ya Uwekezaji vitega Uchumi Zanzibar {ZIPA} Bibi Nasra Mohamed Nassor.
 Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Ardhi na Mipango Miji Zanzibar Dr. Muhammad Juma akimuonyesha Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif  Ramani ya itakavyokuwa Kituo Kikuu cha Gari za Abiria kinachotaka kujengwa katika Mtaa wa Kijangwani.
 Msimamizi wa Mradi wa Ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Zanzibar kupitia SMZ Nd. Yassir De Costa akimpatia maelezo Balozi Seif hatua zilizoanza kuchukuliwa katika ukamilishaji wa Jengo Jipya la Abiria la Uwanja huo.
Balozi Seif akikagua Majengo mapya ya Nyumba za Makaazi zinazojengwa na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar {ZSSF} hapo Mbweni nje kidogop ya Mji wa Zanzibar.

Picha na – OMPR – ZNZ.

Na Othman Khamis, OMPR

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ameuagiza Uongozi wa Mamlaka ya Uwekezaji Vitega Uchimi Zanzibar {ZIPA} na Mamlaka ya Uhifadhi na Uendelezaji Mji Mkongwe wa Zanzibar kuhakikisha kwamba  Muwekezaji aliyepewa Mradi wa Hoteli ya Bwawani  anaufanyia matengenezo ya haraka Ukumbi wa Mikutano wa Salama.

Alisema agizo hilo lazima litekelezwe ndani ya kipindi cha Miezi mitatu kuanzia Mwezi huu  likizingatia kwamba Ukumbi wa Salama ni wa Kijamii na Wananchi wamekuwa wakiupigia kelele kutotoa huduma zake kama kawaida kwa kipindi kirefu sasa.

Balozi Seif Ali Iddi alitoa agizo hilo alipofanya ziara Maalum ya kutembelea miradi ya Uwekezaji  katika maeneo mbali mbali yaliyomo ndani ya Mkoa Mjini Magharibi ili kuona maendeleo  na Changamoto zake.

Alisema Wananchi wengi hivi sasa wanaendelea kuhoji kuchelewa kwa mradi huo ambao walitegemea kuleta matumaini kwa Jamii pam oja na kuongeza mapato ya Taifa yatayokwenda sambamba na kupunguza tatizo la ajira kwa vijana wengi Nchini.

Balozi Seif  alisema Ukumbi wa Salama wa Hoteli ya Bwani ndio pekee unatoa huduma za Kijamii kwa watu wenye kipato cha chini jambo ambalo kusitisha huduma zake kunaendelea kuwapa usumbufu wa maeneo ya kuendesha shughuli zao za Kijamii ikiwemo harusi.

Naye Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Mheshimiwa Ayoub Mohamed Mahmoud alisema wananchi wa Mitaa iliyomo ndani ya Wilaya ya Mjini hivi sasa wanalazimika kutafuta Ukumbi wa kufanya shughuli zao za Kijamii katika maeneo ya mbali ikiwemo Meli Nne Saccos.

Mh. Ayoub alisema kitendo hicho mbali ya kuleta kero na usumbufu lakini pia kinachangia na kuongeza gharama zisizo na tija ambazo zisingewakumba iwapo Ukumbi wa Salama ungekuwa ukiendelea kutoa huduma kama kawaida.

Mapema Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Uhifadhi na Uendelezaji Mji Mkongwe wa Zanzibar Nd. Issa Sarboko Makarani alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba Muwekezaji wa Mradi wa Hoteli ya Bwawani bado ana nia ya kuendelea na ujenzi wa Mradi huo wa Kitalii.

Nd. Sarboko alisema kwa mujibu wa Muongozo wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni {UNESCO} na Mamlaka ya Uhifadhi na Uendelezji wa Mji Mkongwe Muwekezaji huyo hawezi kuanza na ujenzi wa Majengo mapya katika eneo hilo.

 Hata hivyo Nd. Sarboko alisema Taasisi hizo mbili bado zinasubiri maombi ya Michoro yote ya Muwekezaji huyo jinsi anavyokusudia kuendesha Mradi huo wa Ujenzi katika eneo zima la Hoteli ya Bwawani Mjini Zanzibar.

Mapema Balozi Seif  akiambatana na Baadhi ya Mawaziri wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na  Watendaji wa Taasisi za Umma alikagua Jengo la Biashara liliopo Darajani Maarufu Jumba la Treni.

Mkurugenzi Muendeshaji wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar {ZSSF} unaosimamia ujenzi huo Bibi Sabra Issa Machano alimueleza Balozi Seif kwamba ujenzi wa Jengo hilo kwa sasa unaendelea vyema chini ya Mkandarasi wa Kampuni ya Kimataifa ya CRJ kutoka Nchini China.

Bibi Sabra alisema Jengo hilo la Ghorofa Mbili litakapomalizika litakuwa na  Milango ya Maduka ili kutoa huduma za kibiashara, huduma za Mawasiliano ya Mitandao ya Internet pamoja na sehemu ya Mazoezi.

Balozi Seif  na Ujumbe wake  baadae alifika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Aman Karume Kisauni kuangalia harakati za ukamilishaji wa Jengo Jipya la Abiria { Terminal Three } zilizoanza hivi karibuni.

Msimamizi  wa Mradi huo  kwa upande wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar  Ndugu Yaser De Costa aliishukuru na kuipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa juhudi ilizochukuwa za kuhakikisha mradi huo unakamilika kama ulivyokusudiwa.

Nd. De Costa alisema mradi huo umeanza tena kutekelezwa kuanzia Tarehe 20 Novemba 2017 baada ya Benki ya Kimataifa ya Exim ya Nchini Jamuhuri ya Watu wa  China kukubali na kuidhinisha Fedha za Mkopo za Ujenzi huo zinazokadiriwa kufikia Dola za Kimarekani Milioni 35.

Aliipongeza Wizara ya Kilimo, Mali asili na Mazingira Zanzibar kwa kutenda eneo maalum la upatikanaji wa Mchanga utakaosaidia ujenzi huo sambamba na ule unaletwa kutoka Bagamoyo Tanzania Bara.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alipata fursa ya kukagua eneo lililotengwa kwa ajili ya kuwa Kituo Kikuu cha Gari za Abiria zinazoingia Mkoa Mjini Magharibi kiliopo Kijangwani Mjini Zanzibar.

Balozi Seif  pia akapata wasaa wa kuzitembelea Nyuma za Mkopo nafuu zinazojengwa na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar {ZSSF} ziliopo Mbweni  nje kidogo ya Mji wa Zanzibar na kukagua hatua zilizofikia.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.