Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Azungumza na Viongozi wa Timu ya Ujamaa na Kukabidhi Mchango Wake.

Balozi Seif akikabidhi Mchango wa Shilingi Milioni 3,000,000/- kusaidia  Timu ya Soka ya Ujamaa  ambayo aliwahi kuichezea alipokuwa mwanasoka wa Timu hiyo kwa  ajili ya ununuzi wa Vifaa vya Michezo.Mchango huo wa Fedha alimkabidhi  Mwenyekiti wa Ujamaa Sports Club Mohamed Makame.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akizungumnza na Uongozi wa Timu ya Soka ya Ujamaa kwenye Klabu yao iliyopo Mkabala na Jengo la ZBC Redio Rahaleo Mjini Zanzibar .Picha na – OMPR – ZNZ.


Na.Othman Khamis OMPR.
Uongozi wa Timu Kongwe ya Soka Zanzibar ya Ujamaa Sports Club umeagizwa kusimamia vyema  Vijana wao wanaosakata Kabumbu ili kuhakikisha kwamba  Timu yao inarejea katika hadhi yake ya kimichezo iliyokuwa nayo katika miaka ya nyuma.

Agizo hilo limetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar  Balozi Seif  Ali Iddi  ambae pia ni Mchezaji wa zamani wa Timu ya Ujamaa  wakati alipofanya mazungumzo na Uongozi wa Klabu hiyo uiliyopo Mtaa wa Rahaleo Mkabala wa ZBC Redio Mjini Zanzibar.

Balozi Seif alisema Ujamaa ni miongoni mwa Timu Kongwe ndani ya Visiwa vya Zanzibar  yenye Historia kubwa ya kufanya vyema kwenye mashindano ya Ligi Kuu ya Zanzibar na kujizolea sifa kubwa hatua iliyoifanya Timu hiyo kuwa na wanachama wengi kipindi hicho.

Alisema wakati umefika kwa Uongozi wa Klabu hiyo kutafuta mahali ambapo iliteleza na hatimae kufikia hatua ya kuteremka daraja ili mikakati itakayochukuliwa  sasa ijenge nguvu za kurudi katika daraja yake ya asili.

Balozi Seif ambae aliamua kuitembelea Klabu yake hiyo ya zamani aliyoiunga nayo tokea mwanzoni mwa Miaka ya 60 alisema walimu wa Timu hiyo hivi sasa wana kazi ya ziada ya kuwafinyanga Vijana wao ili itakapoingia uwanjani katika ushiriki wa mashindano mbali mbali wapenzi wa soka wafikie pahali pa kuuliza ni ile Ujamaa  sports Club ya Rahaleo.

Katika kuipa nguvu  za kiuendeshaji Timu hiyo ya Soka ya Ujamaa Sports Club Balozi Seif   alikabidhi mchango wa Shilingi Milioni 3,000,000/- ili zisaidie kutia nguvu za ununuzi wa vifaa mbali mbali vya Michezo vitakavyong’arisha Wachezaji wake.

Balozi Seif aliahidi kwamba yuko tayari kuendelea kuiunga Mkono Timu hiyo iliyomjengea Heshima kubwa katika ulimwengu wa soka wakati alipokuwa mlinda mlango mahiri wa Timu hiyo.

Naye Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Ayoub Mohamed Mahmoud alisema majibu ya mchango wa Balozi Seif  kwa Timu ya Ujamaa Sports Club unatarajiwa kuonekana na wapenda soka katika mashindano yajayo yatakayoishirikisha Timu hiyo.

Ayoub alisema Uongozi wa Mkoa unafarajika kuona uwepo na uthamini wa Viongozi katika kuchangia sekta ya Michezo unaosaidia kuhamasisha  Viongozi wengine kuunga mkono jitihada hizo zilizoanza kuonyesha mwanga hasa katika Mpira wa Soka.

Akitoa shukrani kwa Niaba ya Uongozi wa Klabu ya Ujamaa Mwenyekiti Mstaafu wa Timu hiyo Mzee Ahmed Mcheju alimpongeza Mchezaji huyo wa zamani wa Klabu hiyo Balozi Seif  kwa mchango wake  utakaokuwa chachu ya mafanikio kwa Timu hiyo katika mashindano yajayo.

Mcheju alisema Uongozi wa Ujamaa Sports Club utahakikisha kwamba nguvu zilizotolewa na Balozi Seif  katika kutoa msukumo wa Timu hiyo zitasimamiwa na kutekelezwa vyema katika misingi iliyokusudiwa.

Hata hivyo Mcheju aliwanasihi wapenda michezo wote nchini kujilazimisha kufanya kazi ya kujitolea ili kuona sekta ya Michezo inakua na kuifanya Zanzibar inarejea katika  hadhi yake Kimichezo.

Klabu ya Soka ya Ujamaa imeasisiwa Mnamo Mwaka 1957 kwa wakati huo ikijuilikana kwa jina maarufu la Wholves.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.