Habari za Punde

Balozi Seif Atembelea Maonesho ya Tamasha la Nne la Biashara Viwanja Vya Maisara Zanzibar.

Balozi Seif akifurahia ubunifu wa kazi za wajasiri amali wa Zanzibar katika mbinu za kusarifu udongo na hatimae kuwa bidhaa zilizoingia kwenye soko linalokubalika na jamii.
Baadhi ya Wajasiri Amali walioshiriki Maonyesho ya Tamasha la Nne la Biashara Zanzibar  kusherehekea  Miaka 54 ya Mapinduzi ya Zanzibar Hapo Maisara Suleiman wakimpatia maelezo Balozi Seif jinsi ya mali ghafi ya ngozi wanavyoweza kutengeneza bidhaa za mikoba na Viatu.(Picha na – OMPR – ZNZ.
Balozi Seif akiridhika na taaluma kubwa iliyotumiwa na wajasiri amali wa Taasisi ya Waasili Asilia { WA } katika kutengeneza bidhaa zinazotokana na rasilmali ya ngozi.
Picha na – OMPR – ZNZ.


Na. Othman Khamis OMPR.
Serikali zote mbili Nchini Tanzania zimeombwa kupandisha kodi kwa bidhaa zinazotoka nje ya Nchini ambazo zinaweza kuzalishwa na Wajasiri amali wadogo wadogo hapa Nchini ili kutuoa fursa kwa viwanda vya ndani  kuingia vyema katika soko.

Ombi hilo limetolewa na baadhi ya wajasiri amali wa Tanzania mbele ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alipofanya ziara ya kukagua bidhaa na vitu mbali mbali kwenye maonyesha ya Biashara kutimia Miaka 54 ya Mapinduzi ya Zanzibar hapo Viwanja vya Maisara Suleiman Mjini Zanzibar.

Mjasiri  Amali Dedan Munisi wa Taasisi ya Watengenezaji bidhaa za Ngozi ya Waasisi Asilia  kutoka Dar es salaam alimueleza Balozi Seif  kwamba Wajasiri amali wa Ndani wana uwezo kamili wa kutengeneza vifaa na bidhaa uliotokana na jitihada zao za kujifunza kazi za amani kupitia mifumo tofauti.

Dedan alisema  ushahidi wa hao ni  ushiriki wao kwenye maonyesho tofauti yanayoandaliwa na Taasisi mbali mbali ndani ya Bara la Afrika ambao tayari umeshawaonyesha  njia  ya kuelekea kwenye Sekta hiyo ya ajira Binafsi.

Alifahamisha kwamba Waafrika wamebarikiwa kuwa na Rasilmali nyingi na adimu zinazopaswa kutumiwa na Waafrika wenyewe badala ya ule mfumo dume wa Rasilmali hizo kusafirishwa nje ya nchi na baadae kurejeshewa kwa malipo makubwa zaidi.

Alisisitiza kwamba wakati umefika kwa Serikali zote mbili licha ya juhudi kubwa zinazoendelea kuchukuwa za kuwajengea mazingira bora wajasiri Amali lakini bado jitihada hizo kwa sasa zilenge katika kuwapatia mafunzo ya ya Kisasa  Wajasiri Amali hao.

Naye kwa upande wake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema katika kuimarisha Uchumi wa Taifa kuelekea kwenye Viwanda vya Kati Serikali zimekusudia kuongeza Viwanda vidogo vidogo vitakavyoipa nguvu sekta hiyo muhimu kwa Umma.

Balozi Seif  alisema mpango huo umelenga kuongeza nafasi za ajira kwa kundi kubwa la Vijana wanaomaliza masomo yao sambamba na kupunguza ukali wa maisha  miongoni mwa Wananchi wake.

Aliwapongeza Wajasiri amali mbali mbali walioshiriki kwenye Maonyesho hayo pamoja na wengine Mitaani kwa juhudi wanazochukuwa katika kujiletea maendeleo yao bila ya kusubiri mkono wa Serikali Kuu.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar akiambatana na Baadhi ya Viongozi wa Serikali alipata wasaa wa kutembelea mabanda mbali mbali ya Maonyesho na kuridhika na ubora wa bidhaa zinazozalishwa na Wajasiri Amali Wazalendo.

Alisema katika Kuunga mkono jitihada za Wajasiri Amali hao pamoja na zile Taasisi za Uzalishaji za Umma Serikali Kuu kupitia Wizara ya Biashara, Viwanda na Masoko imekubali ombi la Wafanyabiashara hao la kuongeza siku za Maonyesho hayo.

Balozi Seif alisema kwa vile Tarehe ya kuanza kwa Maonyesho hayo ilichelewa kidogo kutokana na sababu zisizozuilika mwisho wa Maonyesho hayo sasa utakuwa Tarehe 25 Januari badala ya Tarehe 20 Januari iliyotangazwa awali.

Alisema hatua hiyo imechukuliwa kuwapa fursa Wajasiri amali na Wafanyabiashara kuuza bidhaa zao kwa vile muitiko wa Wananchi kufuata bidhaa hizo kwa sasa unaendelea kuongezeka.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.