Habari za Punde

Sekta Binafsi Yaridhishwa na Uhusiano Wake na Serikali

Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) akifungua mkutano wa tatu kati ya Sekta Binafsi na Serikali uliofanyika mjini Dodoma.
Makamu Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi nchini (TPSF), Bw. Salum Shamte, akizungumza wakati wa mkutano wa tatu kati ya Sekta Binafsi na Sekta ya Umma uliojadili namna ya kuboresha masuala ya biashara na uwekezaji nchini, mjini Dodoma.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji Prof. Elisante Ole-Gabriel, akionesha kabrasha lenye maelezo ya utekelezaji wa makubaliano mbalimbali yaliyotekelezwa na yanayoendelea kutekelezwa baada ya mikutano miwili ya awali kufanyika Mjini Dodoma na Jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya Wawekezaji na wageni kutoka Taasisi za Kimataifa walioshiriki Mkutano wa tatu wa majadiliano kati ya wadau wa Sekta Binafsi na Sekta ya Umma uliofanyika mjini Dodoma.

Baadhi ya Manaibu Mawaziri, Makatibu Wakuu na Manaibu Makatibu Wakuu na Maafisa wengine kutoka Wizara mbalimbali wakifuatilia mkutano kati ya Sekta Binafsi na Sekta ya Umma, Mjini Dodoma.


Baadhi ya wabunge wakifuatilia kwa makini mkutano wa tatu wa wadau wa Sekta Binafsi na Sekta ya Umma uliofanyika mjini Dodoma
Mbele, ni manaibu Makatibu Wakuu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, wakifuatilia mijadala mbalimbali iliyokuwa ikiendelea wakati wa mkutano kati ya Sekta Binafsi na Serikali, uliofanyika katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango, Mjini Dodoma.


Na Benny Mwaipaja, WFM, Dodoma
Sekta Binafsi nchini imekiri kuwa uhusiano kati yake na Serikali umezidi kuimarika kutokana na kuboreshwa kwa mazingira ya uwekezaji na ufanyajibiashara hapa nchini kuliko ilivyokuwa hapo awali na kwamba hatua hiyo itachochea ukuaji wa uchumi wa nchi.

Kauli hiyo imetolewa mjini Dodoma na Makamu Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi nchini (TPSF), Bw. Salum Shamte, wakati wa mkutano wa tatu kati ya Sekta Binafsi na Sekta ya Umma uliojadili namna ya kukuza ushiriki wa Sekta Binafsi katika kukuza uchumi wa viwanda nchini.

"Sekta binafsi imenituma kuleta pongezi kwa Serikali inayoongozwa na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kwa kutekeleza kwa vitendo utambuzi wa kwamba Sekta Binafsi ni mbia muhimu wa maendeleo ya Taifa letu" alisema Bw. Shamte.

Aliyataja baadhi ya mafanikio yanayo onekana bayana kuwa ni pamoja na kuinusuru Bandari ya Dar es Salaam kwa mabadiliko ya sheria ya fedha ya mwaka 2017 hasa kuondoa VAT kwenye biashara ya mizigo ya kimataifa na kuondokana na umoja wa forodha ambao ulipunguza kwa kiasi kikubwa kiwango cha biashara kati ya Tanzania na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Bw. Shamte alisema kuwa majadiliano hayo kati ya Serikali na Sekta Binafsi kumeikoa sekta ya utalii hasa kwa kuondokana na kodi ya ongezeko la thamani (VAT) kwenye leseni mbalimbali hatua ambayo imerejesha msisimko wa sekta hiyo.

"Serikali imepunguza pia  mlolongo wa kodi kwa wakulima, japokuwa - kazi haijakamilika lakini mwanzo ni mzuri" aliongeza Bw. Shamte

Alieleza kuwa jitihada mpya na nzuri za kutatua changamoto za kodi kwa kampuni zinazojihusisha na biashara kati ya Tanzania Bara na Visiwani, na kuanza kufanya malipo kwa wakandarasi na watoa huduma wa ndani hatua ambayo wanaamini itakuza matumizi ya ndani na mzunguko wa fedha.

Makamu mwenyekiti huyo wa TPSF alisema kuwa Serikali ya Awamu ya Tano ni sikivu na kwamba kwa mara ya kwanza, wanatarajia kushuhudia Bajeti Kuu ya Serikali ya mwaka 2018/2019 ikiwa bora zaidi kwa kubeba mapendekezo yao mengi yatakayosaidia kukuza sekta hiyo na pia kuboresha masuala ya kodi na mapato ya Serikali.

Wakizungumza kwenye mkutano huo, Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango, na Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Bw. Charles Mwijage, wamesema kuwa Serikali inathamini mchango wa Sekta Binafsi katika maendeleo ya uchumi wa viwanda na kwamba itaendelea kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili Sekta hiyo ikiwemo masuala ya kodi.

"Sekta Binafsi ndiyo mhimili wa uchumi kwa hiyo ni muhimu tuhakikishe upande wa Serikali tunafanya wajibu wetu kuiweesha Sekta hiyo iwe imara zaidi na iweze kukua kwa sababu tutapata ajira, bidhaa bora na huduma mbalimbali hatimaye kukuza uchumi wetu wa viwanda" alisisitiza Dkt. Mpango

Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji naye aliongeza kuwa Sekta Binafsi ndiyo itakayojenga viwanda wakati Serikali itakuwa mwezeshaji ndio maana wameamua kukaa  pamoja kujadili changamoto zinazozikabili pande zote mbili na kwamba baadae watajielekeza kujadili na kila Sekta ili kuharakisha maendeleo ya kiuchumi.

Wametoa wito kwa Sekta binafsi nchini kujenga uaminifu na kufuata sheria na kanuni za ufanyajibiashara na uwekezaji nchini ikiwemo kulipa kodi stahiki.

Akizungumza katika mkutano huo wa tatu uliojumuisha wadau mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi, Mkurugenzi wa Shirika la Maendeleo la Marekani (USAID) hapa nchini, Bw. Andy Karas, ameimwagia sifa Tanzania kwa kukuza uchumi wake kwa wastani wa asilimia 7 na kushauri kuwa uchumi huo sasa uelekezwe kutatua changamoto za wananchi hususan kukuza sekta ya kilimo inayoa ajiri idadi kubwa ya watanzania.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.