Afisa Muelimishaji Mkuu wa Mamlaka ya Mapato
Tanzania (TRA), Bi. Rose Mahendeka akiwaelimisha Wafanyakazi wa Mamlaka ya
Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE) kuhusu Kodi na Mabadiliko ya Sheria
ya Fedha ya Mwaka 2017/18 katika ukumbi wa mikutano wa mamlaka hiyo 24 Januari,
2018.
Msaidizi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi toka
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bw. Chama Siriwa akiwasilisha mada mbele ya
Wafanyakazi wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE) kuhusu Kodi
ya Majengo, katika ukumbi wa mikutano wa mamlaka hiyo
Meneja wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi toka
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bi. Valentine Baltazar akiwasilisha mada
mbele ya Wafanyakazi wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE)
kuhusu Taratibu za Kiforodha, katika ukumbi wa mikutano wa mamlaka hiyo 24
Januari, 2018.
(Picha na Benedict Liwenga -TRA)
Na:
Veronica Kazimoto - Dar
es Salaam
Mamlaka ya Mapato
Tanzania (TRA) imepongezwa kwa kuendelea kutoa elimu ya kodi kwa wadau
mbalimbali wakiwemo wafanyakazi wa ofisi za Serikali na Asasi za Kiraia kwa
ajili ya kuongeza ufahamu na kuwa mabalozi wa masuala yanayohusu kodi.
Akizungumza wakati wa
ufunguzi wa mafunzo ya elimu ya kodi kwa wafanyakazi wa Mamlaka ya Maendeleo ya
Biashara (TANTRADE) yaliyofanyika leo ofisini hapo, Mkurugenzi Mkuu wa mamlaka hiyo Bw. Edwin
Rutageruka amesema TRA inastahili kupongezwa kwa kazi inayoifanya ambayo
imepelekea kuongezeka kwa ukusanyaji wa mapato.
"Ni dhahiri kwamba,
sasa hivi TRA inafanya kazi kubwa ya
ukusanyaji wa mapato na kutoa elimu ya kodi kwa vikundi na taasisi mbalimbali,
hivyo, fursa hii tuliyoipata tuitumie vizuri ili kuongeza uelewa wa kutosha
kuhusu kodi ili tuwe mabalozi wazuri kwa
wengine", amesema Rutageruka.
Kwa upande wake Afisa Mkuu
wa Elimu kwa Mlipakodi kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania Bi. Rose Mahendeka, akiwasilisha mada ya Kodi
na Mabadiliko ya Sheria ya Fedha ya mwaka 2017 amesema, kila mwananchi anajukumu la kudai risiti kila
anaponunua bidhaa na kila mfanyabiashara anatakiwa kutoa risti kila anapofanya
mauzo.
"Suala la kulipa
kodi lipo kwa mujibu wa sheria hivyo ni wajibu wa kila mwananchi kudai risiti
wakati wote anaponunua bidhaa na vivyo hivyo kwa upande wa wafanyabiashara wanapaswa
kutoa risiti kila wanapofanya mauzo", amesisitiza Mahendeka.
Muelimishaji mwingine
kutoka TRA aliyewasilisha mada kuhusu Kodi ya Majengo Bw. Chama Siriwa amewahimiza
wafanyakazi hao wa TANTRADE kuwahi kulipa kodi ya majengo ya mwaka huu wa fedha
2017/18 ili kuepuka usumbufu usio wa lazima na msongamano wa watu ambao mara
nyingi hujitokeza kulipa mwishoni.
"Watu wengi wana
tabia ya kusubiri tarehe za mwisho kulipia kodi ya majengo suala ambalo linasababisha
msongamano usio wa lazima na hivyo kuchelewa kupata huduma kwa wakati",
amefafanua Bw. Siriwa.
Siriwa ameongeza kuwa,
Kodi ya Majengo hulipwa kuanzia mwezi Julai Mosi ya mwaka wa fedha husika hadi
Juni 30 ya mwaka unaofuatia na kusisitiza kuwa muda huu ni muafaka kabisa wa
wananchi kuanza kulipia kodi ya majengo mpaka ifikapo tarehe 30 Juni, 2018.
Mamlaka ya Mapato
Tanzania, katika kipindi cha miezi 6 iliyopita imefanya jumla ya semina 137 kwa
wafanyakazi wa Serikali, Asasi za Kiraia, wafanyabiashara na vikundi mbalimbali
kwa lengo la kutoa elimu na kuongeza uhiari katika ulipaji wa kodi.
No comments:
Post a Comment