Habari za Punde

Japan Yakabidhi Mradi wa Soko la Samaki la Kimataifa Kasenda Wilayani Chato Lenye Thamani ya Shilingi Milioni 320

Mhandisi Robert Gabriel Mkuu wa Mkoa wa Geita pamoja na Mheshimiwa Yoshida Masaharu Balozi wa Japan Nchini Tanzania wakisaini kitabu cha wageni baada ya kuwasili kijiji cha Kasenda kwa ajili ya Makabidhiano ya Mradi wa Soko la Samaki la Kimataifa na kusaini mkataba wa ukarabati wa barabara yenye urefu wa Kilometa 1 ya kutoka Mganza kwenda Kasenda.
 Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya Chato Bw;Joel Hari na Balozi wa Japan Nchini Tanzania Mheshimiwa  Yoshida Masaharu wakisaini mkataba wa ukarabati wa barabara ya Mganza hadi Kasenda Kilometa 1 huku wakishuhudiwa na viongozi mbalimbali wa Mkoa na Wilaya ya Chato. 
Waziri wa Nishati (Mb) Medard Kalemani wa kwanza kulia aliyevaa shati jeupe akijadili jambo pamoja na Mheshimiwa Balozi Yoshida Masaharu, Mhandisi Robert Gabriel Mkuu wa Mkoa wa Geita na Bathromeo manunga Mwenyekiti wa Halmashauri ya Chato
Balozi wa Japan Nchini Tanzania Mheshimiwa Yoshida Masaharu aliyevaa miwani na tai nyekundu pamoja na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chato bw; Joel Hari wakiweka jiwe la makabidhiano ya mradi wa Soko la Kimataifa la Samaki ambalo limefadhiliwa na Serikali ya Japan kwa Gharama ya Shilingi milioni 320 kijiji cha Kasenda Chato.
Balozi wa Japan Nchini Tanzania Mheshimiwa Yoshida Masaharu akifurahi na Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhandisi Robert Gabriel baada ya makabidhiano ya Soko la Samaki la Kimataifa lililopo kijiji cha Kasenda Kata ya Mganza Wilaya ya Chato.
Balozi wa Japan Nchini Tanzania Mheshimiwa Yoshida Masaharu aliye vaa miwani na tai nyekundu akiwa na Viongozi wa Mkoa wa Geita na Wilaya ya Chato baada ya makabidhiano ya mradi wa ujenzi wa Soko la Samaki la Kimataifa la Kasenda Wilayani Chato.Watatu kutoka kushoto kwa balozi ni Waziri wa Nishati (Mb) Mheshimiwa Medard Kalemani na Shaban Ntarambe Mkuu wa Wilaya ya Chato na Kulia kwa balozi aliyevaa miwani na suti ya kijivu ni Mkuu wa Mkoa wa Geita mhandisi Robert Gabriel pamoja na Bw; Joel Hari Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Chato.



Na.Magesa Jumapili. Geita RS
Serikali ya watu wa Japan imekabidhi mradi wa Soko la Samaki la kimataifa kwa Halmashauri ya Wilaya ya Chato wenye thamani ya shilingi milioni 320 na kusaini makubaliano ya ukarabati wa barabara ya Mganza - Kasenda ili kurahisisha usafirishaji wa mazao ya ziwani.

Akizungumza baada ya kukabidhi mradi huo kwa Serikali Balozi wa Japan nchini Tanzania Mheshimiwa Yoshida Masaharu amesema mradi huo umetolewa na Serikali ya Japan kwa watu wa Tanzania ikiwa ni mwendelezo wa urafiki wa siku nyingi katika utekelezaji wa miradi ya kilimo na uvuvi.

''Mradi wa huu ulitolewa baada ya kuona soko la Kasenda liko katika hali mbaya na samaki kuharibika kwa kukosa miundombinu ya kuhifadhi ndipo Japan ikachukua hatua za haraka kwa kutoa fedha dola za kimarekani 148,146 kwa ajili ya kujenga soko na kukarabati soko la zamani''. Utekelezaji wa mradi ulianza mwaka 2017 na sasa wananchi wanaendelea kunufaika.

Awali akisoma taarifa ya mradi huo kabla ya makabidhiano mkurugenzi wa Halmashauri ya Chato Joel Hari amesema mradi unahusisha ujenzi wa ghala kubwa la kuhifadhia samaki na ukarabati wa sokola zamani.Ameeleza kuwa soko lipo chini ya Halmashauri ya Chato likiwa na wanachama 241 huku likikasimiwa kukusanya shilingi milioni 140 kwa mwaka huku likitoa huduma kwa nchi za Rwanda,Burundi, Uganda na Congo DRC.

Kwa upande mwingine Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhandisi Robert Gabriel amemshukuru balozi wa Japan nchini kwa miradi hiyo na kumwomba kuangalia na Wilaya zingine za Mkoa wa Geita ili nazo zinufaike na miradi ya namna hiyo.

Aidha, ameutaka uongozi wa soko kwa kushirikiana na Halmashauri ya Chato kuhakikisha malengo yote yaliyokusudiwa kwa mradi huo yanatekelezeka na kuleta faida ili watu wote wanaofanya kazi katika soko hilo waongeze kipato kwa kuwa kazi ya Serikali ya awamu ya tano ni kujenga miundombinu bora na kuweka mazingira wezeshi ya kusaidia kuendesha biashara.Mhandisi Robert Gabriel ameahidi kuangalia namna ya kutafuta fedha kwa ajili ya kujenga vibanda vya pembeni mwa soko ili kuwe na mazingira mazuri ya kufanya biashara.

Mbunge wa Chato ambaye pia ni Waziri wa Nishati Mheshimiwa Medard Kalemani amemshukuru Balozi Yoshida kwa kutoa miradi hiyo Wilayani Chato na kuomba pia kusaidia ujenzi wa kiwanda cha kuunganisha magari.

Amewataka wananchi wa Chato na Kasenda kutumia fursa ya uwepo wa mradi huo kujenga biashara na kutoa wito kwa wenye mitaji midogo kuitunza ili ikuwe.Katika makabidhiano hayo Serikali ya Tanzania na Japan zimesaini mkataba wa ukarabati wa barabara yenye urefu wa Kilometa 1 kutoka Mganza hadi Kasenda ili kurahisisha usafirishaji wa bidhaa za kutoka ziwani.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.