Habari za Punde

Sheria mpya adhabu ya makosa ya jinai Zanzibar yapitishwa

Na Ali Issa, MAELEZO-ZANZIBAR.13 FEBUARI, 2018
WAJUMBE wa Baraza la Wawakilishi leo wameupitisha mswada mpya wa sheria ya adhabu kwa makosa ya jinai.
Sheria hiyo mpya ya mwaka 2018, inafuta sheria ya adhabu kwa makosa ya jinai ya mwaka 2004.
Akisoma sheria hiyo mpya mbele ya wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, Waziri wa Nchi (OR) Katiba, Sheria, Utumishi wa Umma na Utawala Bora Haroun Ali Suleiman, alisema mswada huo umepitishwa kutokana na kuongezeka makosa ya jinai ambayo  sheria zake hazilingani na adhabu zinazotolewa kwa sasa.
Alieleza kuwa, ujio wa sheria hiyo mpya, kutatoa nafasi ya mahakimu kutoa adhabu zinazolingana na uzito wa makosa husika.
Aidha alisema sheria hiyo itafanya kazi mara baada ya kusainiwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein.
Kwa upande wake, Mwanasheria Mkuu wa serikali Said Hassan Said, alisema kwa mujibu wa sheria hiyo, ni Jaji Mkuu pekee ndiye mwenye uwezo wa kutoa dhamana kwa mshtakiwa wa  makosa ambayo kimsingi hayastahiki dhamana.
Aliyataja baadhi ya makosa yasiyokuwa na dhamana kuwa ni pamoja na ubakaji, kulawiti, kuua, uhaini, kuingiza nchini na kusambaza dawa za kulevya na mengineyo.
Mwanasheria Mkuu alieleza kuwa sheria hiyo ilijadiliwa kwa umakini mkubwa na wajumbe wamejiridhisha na kuipitisha wakiamini itapunguza kilio cha wananchi kwa kutoa hukumu za haki kwa watuhumiwa wa makosa ya jinai.
Kwa upande mwengine, Naibu Waziri wa Wizara hiyo Khamis Juma Maalim alisema adhabu ya kunyongwa itaendelea kuwepo kutokana na uzito wa makosa yatakayobainika kuwa washtakiwa wanastahiki hukumu hiyo.
Aidha alisema serikali itaendelea kutoa elimu kwa wananchi ili waielewe vyema sheria hiyo mpya itayo tumika mahakamani huku akiwasisitiza juu ya umuhimu wa kufuata sheria bila shuruti. 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.