Habari za Punde

TRA Kuendelea Kuwachukulia Hatua Kali Wafanyabiashara Wanaojishughulisha na Biashara za Magendo.


Na: Veronica Kazimoto,Dar es Salaam. 

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), inatoa onyo kali kwa wafanyabiashara wote wanaojihusisha na Biashara za Magendo na aina mbalimbali za ukwepaji kodi kupitia Viwanja vya Ndege, Vituo vya Forodha Mipakani, Njia za panya pamoja na Bandari bubu kuacha mara moja vitendo hivyo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo na Kamishna Mkuu wa mamlaka hiyo Bw. Charles Kichere, hatua kali za kisheria zitaendelea kuchukuliwa dhidi ya mfanyabiashara yeyote atakayebainika kusafirisha bidhaa kwa kutumia njia za magendo na kukwepa kodi ikiwa ni pamoja na kutaifishwa mali zote zitakazokamatwa pamoja na chombo kilichotumika kusafirisha au nyumba iliyohifadhi bidhaa hizo.

Taarifa hiyo imesema kwamba, kukwepa kodi ni Kosa la Jinai kwa mujibu wa Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya Mwaka 2005 na Sheria  ya Usimamizi wa Kodi ya Mwaka 2015. 

Aidha, taarifa hiyo imesisitiza kuwa, ukwepaji kodi husababisha mambo mengi ikiwa ni pamoja na kuikosesha Serikali mapato yake halali ya kuimarisha uchumi ambayo yangeiwezesha Serikali kutoa huduma za jamii kwa wananchi wake na kuwepo kwa ushindani usio kuwa wa haki na usawa kati ya bidhaa zinazoingizwa nchini zikiwa zimelipiwa kodi na zile zinazouzwa bila kulipiwa kodi stahiki kutoka nje ya nchi.

Vilevile, ukwepaji kodi huhatarisha maisha ya walaji kwa kuingiza bidhaa ambazo hazijathibitishwa viwango vya ubora na usalama wake kupitia mamlaka husika ikiwa ni pamoja na Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) na Shirika la Viwango Tanzania (TBS). Pia, huhatarisha uchumi na usalama wa nchi kwa sababu ya uwezekano wa kuingiza vitu vya hatari kama vile silaha.

Taarifa hiyo ya Kamishna Mkuu wa TRA imewaomba wananchi kutoa taarifa ya mfanyabiashara au kampuni yoyote inayojihusisha na vitendo vya Biashara ya Magendo na ukwepaji kodi kwa kupiga simu namba +255 22 2137638 au +255 784 210209.

Hivi karibuni Mamlaka ya Mapato Tanzania ilikamata na kutaifisha bidhaa mbalimbali zikiwemo tani moja ya sukari na chumvi, majani ya chai mifuko 18, mirungi kilogramu 16, vifaranga vya kuku 5000 na mayai kasha 416 katika mpaka wa Namanga mkoani Arusha zikitokea nchini Kenya kupitia njia zisizo rasmi.

Wafanyabiashara hao walioingiza baadhi ya bidhaa hizo kwa kutumia vifungashio vya bidhaa nyingine za nchini Tanzania ili kuficha uhalisia wake huku wakiwa hawana vibali wala kulipa ushuru wa Serikali, watachukuliwa hatua kwa mujibu wa Sheria

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.