Habari za Punde

Waziri Mpina Akamata Meli ya Uvuvi Haramu na Kuitoza Faini ya Milioni Mia Saba Sabini.



Waziri wa Mifugo  na Uvuvi Luhaga Mpina akiangalia  mzigo wa mapezi  ya samaki aina ya papa wakati Kapteni Han Ming Chuan wa Meli ya Buah Naga 1 akifungua mfuko wenye Mapezi yaliyokamatwa kinyume na  Sheria yaUsimamizi  wa Bahari Kuu(DSFA) ya Mwaka 1998  kama ilivyorekebishwa Mwaka 2007.Meli hiyo ilitozwa faini ya shilingi milioni 770. Picha na John Mapepele
 Waziri wa Mifugo  na Uvuvi Luhaga Mpina akiangalia pezi  la samaki aina ya papa wakati alipokagua Meli ya Buah Naga 1 yenye Mapezi yaliyokamatwa kinyume na  Sheria yaUsimamizi  wa Bahari Kuu(DSFA) ya Mwaka 1998  kama ilivyorekebishwa Mwaka 2007.Meli hiyo ilitozwa faini ya shilingi milioni 770. Picha na John Mapepele
 Waziri wa Mifugo  na Uvuvi Luhaga Mpina akitoka kwenye Meli ya Buah Naga 1 baada ya kuikagua ambapo ilikutwa na mapezi ya samaki aina ya papa kinyume na  Sheria yaUsimamizi  wa Bahari Kuu(DSFA) ya Mwaka 1998  kama ilivyorekebishwa Mwaka 2007.Meli hiyo ilitozwa faini ya shilingi milioni 770. Picha na John Mapepele
Meli ya Buah Naga 1 iliyokamatwa eneo la Mtwara ikiwa na kilo 90 ya mapezi ya samaki aina ya papa yaliyokamatwa kinyume na  Sheria yaUsimamizi  wa Bahari Kuu(DSFA) ya Mwaka 1998  kama ilivyorekebishwa Mwaka 2007.Meli hiyo ilitozwa faini ya shilingi milioni 770. Picha na John Mapepele
Na John Mapepele, Mtwara
Waziri wa Mifugo  na Uvuvi Luhaga Mpina ameridhia utozwaji wa faini ya dola za kimarekani laki tatu na nusu sawa na shilingi milioni mia saba  na sabini iliyotozwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Bahari Kuu (DSFA)  kwa Meli ya Buah Naga 1 kutoka nchini Malaysia  kwa kosa la kukutwa  mapezi ya  samaki aina ya papa kilo 90 huku miili ya samaki hao kutupwa baharini kinyume na kanuni ya 66 ya kanuni za bahari kuu za mwaka 2009 na kifungu namba 18(2) cha  Sheria yaUsimamizi  wa Bahari Kuu(DSFA) ya Mwaka 1998 kama ilivyorekebishwa Mwaka 2007.

Akizungumza  baada ya kukagua meli hiyo leo mjini Mtwara, Waziri Mpina alisema kuwa  wamiliki  wa meli hiyo wanatakiwa kulipa faini hiyo ndani ya siku saba ambapo kama hawatalipwa watapelekwa mahakamani mara moja na kushtakiwa kwa mujibu wa sheria za nchi.

Aidha Mpina amesema Serikali imetaifisha tani nne na nusu za samaki ambazo zitauzwa mara moja kwa njia ya mnada na kwa kuzingatia taratibu mbalimbali za Serikali.

Akitoa taarifa ya kukamatwa kwa meli hiyo, kwa Waziri, Kiongozi wa Kikosi Kazi maalum cha kudhibiti uvuvi haramu, Kamishna  Frederick Milanzi wa Tume ya Kupambana na Madawa ya Kulevya nchini amesema kwamba Kapteni wa meli hiyo Han Ming Chuan raia wa Malaysia  alikutwa  na bastola  aina ya Bereta na risasi kumi ambayo alikuwa anaimiliki kinyume cha sheria.

Amesema kuvua na kutupa mizoga ya samaki baharini siyo tu kwamba wanahujumu  raslimali za uvuvi baharini bali pia wanachangia  katika uchafuzi wa mazingira ya baharini.
Pia Waziri Mpina amesisitiza kuwa Serikali haipo tayari kufanya kazi  na wawekezaji wababaishaji  kwenye sekta ya uvuvi na kwamba kuanzia sasa  hatua kali za kisheria zitachukuliwa kwa  yeyote atakayejaribu kuhujumu raslimali za uvuvi na kujihusisha na uvuvi haramu.

Aidha Waziri Mpina  ametoa onyo kali kwa wawekezaji wa uvuvi kwenye bahari ya Tanzania kuacha kutumia mwanya wa kupewa kibali cha kuvua na kujihusisha na  makosa mbalimbali.

Ameyataja  baadhi ya makosa  hayo kuwa ni pamoja na usafirishaji haramu wa silaha, binadamu, madawa ya kulevya na nyara za serikali ikiwemo meno ya tembo. Pia usafirishaji wa  mazao ya misitu na samaki.

Kwa upande wake, Bw. Wankyo Simon ambaye ni Wakili wa Serikali kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali Divisheni ya Mashtaka Makao Makuu Dar es Salaam na Mkuu wa Dawati linalohusiana na Makosa ya Mazingira, amesema makosa ya namna hii ni makubwa na endapo kiwango hicho cha pesa hakitalipwa kama ilivyoamriwa, taratibu za kiupelelezi zitakamilishwa na kapteni wa Meli hiyo atafikishwa mahakamani kwa makosa yaliyoainishwa ambapo anaweza kupewa adhabu ya kifungo na meli hiyo kutaifishwa na kuwa mali ya Serikali. 

Pia amependekeza kuwepo kwa mwongozo wa uendeshaji mashauri (Standard Operating Procedures) kwa makosa yanayofanyika baharini ili uweze kutumiwa na wadau mbali mbali kuanzia ukamataji wa chombo husika, upelelezi wake, namna bora ya kutunza chombo hicho na uendeshaji wa mashauri yanayotokana na operesheni zote zinazofanyika baharini. 

Alisema mwongozo utasaidia kuimarisha kesi zote zinazoenda mahakamani kuanzia inapofunguliwa mpaka kufikishwa mahakamani na wadau wote watajua kwa urahisi namna ya kusimamia utekelezaji wa majukumu yao.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa (DSFA) Hosea Mbilinyi amesema Mamlaka yake imegundua kuwepo kwa  baadhi ya wawekezaji wasiofuata taratibu na Sheria  za kufanya shughuli za uvuvi katika bahari ya Tanzana  ambapo amesema tayari Mamlaka imeshawapiga faini ya dola za kimarekani laki moja kwa meli tatu zilizofanya makosa katika sikuza hivi karibuni.

Katika siku za hivi karibuni Waziri wa Mifugo na Uvuvi ameunda  timu iliyoshirikisha  wataalam kutoka katika vyombo mbali vya Serikali kuendesha operesheni maalum ya kutokomeza uvuvi haramu nchini ambayo  licha ya kupata mafanikio makubwa imetoa hamasa kwa wavuvi  kuanza kusalimisha  zana haramu za uvuvi  na kuziteketeza.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.