Habari za Punde

Maadhimisho ya ‘Siku ya Afya ya Meno’ duniani

MWAKILISHI wa jimbo la Tunguu Simai Mohammed Said, akizungumza na wanafunzi wa skuli ya msingi Unguja Ukuu, wakati wa zoezi la kupima afya ya kinywa na meno lililoendeshwa na jumuiya ya HIPZ kwa kushirikiana na Wizara ya Afya Zanzibar skulini hapo leo Machi 7, 2018. (Picha na Haroub Hussein).
 DAKTARI Feroz Jafferji ambaye ni mratibu wa jumuiya ya HIPZ, akimchunguza kinywa mwanafunzi wa skuli ya Unguja Ukuu Mkoa wa Kusini Unguja ili kujua iwapo ana ubovu wa meno, wakati jumuiya hiyo ilipotoa mafunzo ya kupiga mswaki vizuri. (Picha na Haroub Hussein-Zanzibar).
 Dk Najat Abdalla akimuangalia mwanafunzi Hafidh Ali wakati wataalamu wa afya ya kinywa na meno kutoka jumuiya ya HIPZ walipofika skuli ya msingi Unguja Ukuu kutoa mafunzo juu ya namna bora ya kupiga mswaki. (Picha na Haroub Hussein).

DAKTARI Anna Dilan Yildiz akionesha namna ya kupiga mswaki vizuri kwa wanafunzi wa shule ya msingi Unguja Ukuu katika jimbo la Tunguu Zanzibar ikiwa ni maandalizi ya kuadhimisha ‘Siku ya Afya ya Meno’ duniani ifikapo Machi 20, 2018. Kushoto ni Mwakilishi wa jimbo la Tunguu Simai Mohammed Said. (Picha na Haroub Hussein-Zanzibar).MACHI 7, 2018

KUELEKEA maadhimisho ya ‘Siku ya Afya ya Meno’ duniani, Jumuiya ya HIPZ leo Machi 7, 2018  ilikuwa katika skuli ya msingi Unguja Ukuu kutoa mafunzo kwa wanafunzi juu ya namna bora ya kupiga mswaki.

Jumuiya hiyo, kwa kushirikiana na madaktari wa Wizara ya Afya, pia iliwafanyia uchunguzi wanafunzi wa skuli hiyo ili kubaini watoto wenye matatizo ya meno na kuwapatia tiba.

Akizungumza katika zoezi hilo, daktari dhamana kanda ya Unguja Muhidin Abdalla Mohammed, alisema kutokana na umuhimu wa afya ya meno, wizara imaeamua kuufanya mwezi Machi kuwa wa kampeni ya usafi wa kinywa na meno.

Alisema, kampeni hiyo ni miongoni mwa maandalizi kuelekea ‘Siku ya Afya ya Meno’ kimataifa ambayo huadhimishwa tarehe 20 Machi ya kila mwaka, ambayo inafanywa ili kukuza uelewa wa watu katika afya ya meno ambayo alisema bado jamii haijaipa kipaumbele.

Dk. Abdalla alisema tayari zoezi kama hilo limefanyika jana (Machi 6) katika skuli ya Kivunge Mkoa wa Kaskazini Unguja, na kesho Machi 8 wamepanga kufika skuli ya Jambiani Mkoa wa Kusini Unguja, na wiki ijayo watakuwa skuli za Mwanakwerekwe, Mjini Magharibi.

“Afya ya meno ni muhimu lakini bado jamii haina mwamko wa kuyashughulikia wa uzito unaostahili kama wanavyofanya kwenye mambo mengine kiafya. Aidha ni vyema iwe tunawachunguza watoto mapema pamoja na kuwafunza namna bora ya kupiga mswaki ili kuepusha uharibifu,” alifahamisha Dk. Abdalla.

Alieleza kuwa hapa Zanzibar, tatizo la meno ni kubwa kwani yanawapata wananchi wengi kwa nama tafauti, ama kuugua meno kwa kutoboka au kuumwa ufizi, lakini akasema yanaweza kuepukwa kama jamii itafuata maelekezo ya kitaalamu katika kuyatunza.

Daktari huyo aliwataka wananchi waache kutumia dawa za kienyeji katika kutibu maradhi ya meno, ambazo alisema vipimo vyake si vya uhakika, bali wakiona dalili za na matatizo ya meno wafike hospitali mapema na kupata ushauri na tiba za kitaalamu. 

Aliishukuru jamii kwa kuwapa ushirikiano na kujitokeza kwa wingi katika kampeni hiyo, ambayo alisema ni  muhimu katika kuyapatia ufumbuzi matatizo ya meno.

Mapema, Mwakilishi wa jimbo la Tunguu Simai Mohammed Said, aliwashukuru wataalamu hao kwa kutoa elimu hiyo kwani usafi wa kinywa ni muhimu kwa kujenga heshima ya mtu na mapenzi mbele ya watu anaoishi pamoja nao.

Alieleza kufarijika kwa juhudi za walimu wa skuli hiyo katika kutoa elimu ya usafi kwa wananfunzi, mbali ya fursa kama hizo za huduma za kiafya zinazowafikia mara kwa mara.

Mwakilishi huyo aliwaahidi madaktari hao kwamba uongozi mzima wa jimbo utaendelea kutoa ushirikiano kwa taasisi za kiserikali na binafsi, kila zinapohitaji kuwapeleka wananchi huduma mbalimbali za kijamii.

Zoezi hilo litaendelea hadi Machi 20, mwaka huu, ambapo itakuwa kilele cha maadhimisho ya ‘Siku ya Afya ya Meno’ duniani, huku likijumuisha madaktari wengine wa kujitolea kutoka nchini Ujerumani na Umoja wa Falme za Kiarabu.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.